Table of Contents

Aya 141 – 159: Swaleh

Maana

Kisa cha Swaleh kimetangulia katika Juz. 8 (7: 73 – 79) na Juz. 12 (11: 61 -68).

Thamud waliwakadhibisha mitume. Alipowaambia ndugu yao Swaleh: Je, hamna takua? Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Zimetangulia Aya hizi kwa herufi zake katika sura hii Aya 105 – 110, na pia katika sehemu iliyopita bila ya mabadiliko yoyote isipokuwa jina tu la Thamud na Swaleh. Tumesema huko kuwa siri ya hilo ni kuwa risala ya mitume wote ni moja.

Je, mtaachwa salama katika haya yaliyopo hapa katika mabustani na chemchem na mimea na mitende yenye makole yalioiva? Na mna chonga majumba mlimani kwa ustadi

Kabila la Thamud lilizama katika anasa na strehe – matunda, mito, makasri, wanyama n.k. Wakiwa wameghafilika na kila kitu isipokuwa matamanio yao na ladha zao. Ndipo ndugu yao Swaleh akawaonya na mwisho mbaya na akawaambia, Je, mmemsahau Mwenyezi Mungu na yeye hajawasahau? Je, mmejiaminisha na matukio ya ghafla?

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini wala msitii amri za waliopituka mipaka ambao wanafanya ufisadi katika ardhi wala hawaitengenezi.

Makusudio ya waliopituka mipaka, walio wafisadi, ni viongozi ambao ndio chimbuko la balaa zote; isipokuwa wachache sana. Hakuna dini wala misimamo, katika ufahamu wao, isipokuwa masilahi yao na masilahi ya jamaa zao.

Wafisadi hawa, katika kaumu ya Swaleh, walikuwa tisa; kama ilivyoelezwa katika Aya nyingine: kwenye juzuu hii. “Na walikuwako mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi wala hawafanyi la masilahi” (25:48).

Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa tu.

Umerogwa na mchawi mpaka umekuwa hujui unalolisema. Hivi ndivyo wasemavyo vijana wengi wa kileo wanapoambiwa swalini na fungeni.

Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi, unakula chakula na kutembea sokoni, sasa vipi unateremshiwa wahyi zaidi yetu sisi?

Basi lete ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

Walisema haya wakiwa wameazimia kuendelea na ukafiri wao na inadi yao, hata kama wataletewa dalili elfu na moja; vinginevyo maombi yao yangelikuwa ya haki na ya sawa.

Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalum. Wala msimguse kwa ubaya isije ikawashika adhabu ya siku kubwa.

Walimuomba awaletee muujiza unaofahamisha utume wake, akawaletea ngamia kwa njia isiyo ya kawaida na akawawekea sharti la maji kwa zamu; siku moja yao na siku moja ya ngamia na kwamba wasimdhuru isije ikawafikia adhabu, lakini wakamuua wakawa wenye kujuta.
Basi ikawashika adhabu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7: 77 – 78).

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ الْمُرْسَلِينَ {160}

Kaumu ya Lut waliwakadhibisha mitume.

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ لُوطٌ أَلَا تَتَّقُونَ {161}

Alipowaambia ndugu yao Lut: Je, hamna takua?

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ {162}

Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ {163}

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ {164}

Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

أَتَأْتُونَ الذُّكْرَانَ مِنَ الْعَالَمِينَ {165}

Je, katika viumbe wote mnawaendea wanaume?

وَتَذَرُونَ مَا خَلَقَ لَكُمْ رَبُّكُمْ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ ۚ بَلْ أَنْتُمْ قَوْمٌ عَادُونَ {166}

Na mnaacha alichowaumbia Mwenyezi Mungu katika wake zenu? Bali nyinyi ni watu mnaoruka mipaka.

قَالُوا لَئِنْ لَمْ تَنْتَهِ يَا لُوطُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمُخْرَجِينَ {167}

Wakasema: Kama hutakoma ewe Lut bila shaka utakuwa miongoni mwa wanaotolewa.

قَالَ إِنِّي لِعَمَلِكُمْ مِنَ الْقَالِينَ {168}

Akasema: Hakika mimi ni katika wanaokichukia hiki kitendo chenu.

رَبِّ نَجِّنِي وَأَهْلِي مِمَّا يَعْمَلُونَ {169}

Mola wangu! Niokoe na ahli zangu kwa wayatendao.

فَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ أَجْمَعِينَ {170}

Basi tukamuokoa na ahli zake wote.

إِلَّا عَجُوزًا فِي الْغَابِرِينَ {171}

Isipokuwa kikongwe katika waliokaa nyuma.

ثُمَّ دَمَّرْنَا الْآخَرِينَ {172}

Kisha tukwaangamiza wale wengine.

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ مَطَرًا ۖ فَسَاءَ مَطَرُ الْمُنْذَرِينَ {173}

Na tukawanyesheza mvua, basi ni uovu mno wa mvua ya waliyoonywa.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُمْ مُؤْمِنِينَ {174}

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ {175}

Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.