read

Aya 15 – 19: Suleiman

Maana

Na hakika tulimpa Daud na Suleiman elimu, iliyowaongoza kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu na manufaa ya watu. Wala hawakujivuna nayo kwa waja wa Mungu au kuvumbua nayo silaha za maangamizi ili kuwakandamiza wanyonge wawanyonye nyenzo zao.

Bali hawa wawili walimtii Mwenyezi Mungu katika maamrisho yake na makatazo yake na wakamshukuru kwa neema ya elimu ambayo hailinganishwi na chochote na wakasema: Sifa njema zote (alhamdu lillah) ni za Mwenyezi Mungu ambaye ametufadhilisha kuliko wengi katika waja wake waumini.

Makusudio ya kufadhilishwa (kufanywa bora) hapa, ni kufadhilishwa kwa elimu yenye manufaa. Maana ya kuiliko wengi katika waumini ni wale wasiofikia cheo chao cha elimu.

Hapo kuna ishara kuwa katika waumini wako waliofadhilishwa zaidi yao. Na hivyo ndivyo ilivyo.

Kwa vyovyote iwavyo ni kuwa ubora mbele ya Mwenyezi Mungu haupimwi kwa elimu wala kwa kuupeleka upepo au kulainisha chuma; isipokuwa ni kwa manufaa ya watu na masilahi yao.

Na Suleiman alimrithi Daud.

Daud (a.s.) ni katika kizazi cha Ya’qub bin Is-haq bin Ibrahim. Mwenyezi Mungu alimtukuza kwa utume, akamteremshia Zabur, akamfanya ni khalifa katika ardhi, akamuhusisha kuwa na sauti nzuri zaidi na akamlainishia chuma. Yeye ni mfalme wa pili wa dola ya kiyahudi.

Alipewa jina la Mfalme Daud. Mfalme wa kwanza alikuwa ni Talut, kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

إِنَّ اللَّهَ قَدْ بَعَثَ لَكُمْ طَالُوتَ مَلِكًا ۚ {247}

“Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia Talut kuwa mfalme.” Juz. 2 (2:247).

Mwanawe Suleiman (a.s.) alikuwa ni mtume vile vile. Naye Mwenyezi Mungu alimpa neema nyingi, zikiwemo kurithi ufalme wa baba yake. Historia inasema kuwa ufalme wao uliendelea kwa miaka sabini.

Baada ya kufa Suleiman, mayahudi waligawanyika dola mbili zinazopigana: Dola ya Israil na dola ya Yahudha. Alipokuja Nebuchadnezzar aliwafyeka na hakukua na dola tena ya kiyahudi, mpaka pale ukoloni wa Anglo America ulipoanzisha kambi ya kijeshi kulinda masilahi yake mashariki ya kati, ukaipa jina la dola Israil kwenye ardhi ya Palestina mnamo mwaka 1948.

Mayahudi wanamzungumza vibaya mfalme wao Daud, kwamba alikuwa akiwapora wanawake na kuwaua waume zao na mwanawe Suleman alikuwa ni jabari mkandamizaji na mwenye israfu.

Baadhi ya wafasiri wanasema kuwa makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na Suleiman alimrithi Daud” ni kuwa alirithi elimu tu kutoka kwa baba yake. Lakini ilivyo hasa ni kuwa Aya inafahamisha urithi wa ufalme; kama ilivyotokea hasa. Ama elimu haiwi kwa kurithi, bali ni kwa juhudi au kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kuna tofauti katika Hadith ya “Sisi Mitume haturithiwi,” baina ya Waislamu. Kuna walioithibitisha na walioikanusha.

Na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege.

Uislamu umethibitisha fikra ya muujiza mikononi mwa mitume. Mwenye kuikana si Mwislamu, kwa sababu ukanusho huo ni sawa na kumkadhibisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ni kwa muujiza pekee yake ndio tunaweza kufasiri kauli ya Nabii Suleiman: ‘Na tumefunzwa usemi wa ndege.”

Na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhahiri.

Makusudio ya neno ‘kila’ hapa ni wingi sio kuenea kwenye kila kitu; ni sawa na kusema fulani ana kila kitu, kwa kuelezea kuwa ana vitu vingi.

Aya inafahamisha kuwa ndege wana utambuzi na lugha inayofahamika. Hilo linasisitizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا مِنْ دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا طَائِرٍ يَطِيرُ بِجَنَاحَيْهِ إِلَّا أُمَمٌ أَمْثَالُكُمْ ۚ {38}

Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake, ila ni umma kama nyinyi. Juz. 7 (6:38).

Na alikusanyiwa Suleiman majeshi yake kutokana na majini na watu na ndege, nayo yakapangwa kwa nidhamu.
Neno ‘kutokana’ ni baadhi; yaani baadhi ya majini, watu na ndege. Tumesema mara nyingi kwamba sisi tunaamini kuweko majini, kwa sababu Qur’an inathibitisha hilo na akili haikatai.

Suleiman alikuwa na jeshi la majini, watu na ndege. Kila moja ya makundi haya matatu lilikuwa na kamanda wake anayechunga nidhamu ya kutembea n.k. Hii ndio maana ya kupangwa kwa nidhamu.

Somo Na Mazingatio Katika Chungu Wa Suleiman

Hata walipofikia kwenye bonde la chungu, alisema chungu mmoja: Enyi chungu, ingieni maskani zenu, asije akawaponda Suleiman na jeshi lake na hali wao hawatambui.

Wafasiri wametofautiana kuhusu bonde hili. Kuna waliosema ni Taif na wengine wakasema ni Sham. Vyovyote iwavyo ni kuwa Aya inafahamisha kuwa wadudu chungu wana utambuzi, lugha na nidhamu. Haya yamethibitishwa na elimu. Ama Suleiman kujua lugha ya chungu, hilo halina tafsiri isipokuwa ni muujiza.

Unaweza kuliza: Vipi Suleiman aliweza kusikia maneno ya chungu na yaye alikuwa mbali nao kiasi ambacho anayejua ni Mungu tu; kama tunavyojua kuwa lau mmoja wetu ataingiwa na chungu sikioni hawezi kusikia?

Jibu: Baadhi ya riwaya zinasema kuwa upepo ulichukua maneno ya chungu kwa Suleiman. Haya yanatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

فَسَخَّرْنَا لَهُ الرِّيحَ تَجْرِي بِأَمْرِهِ {36}

“Basi tukamtiishia upepo ukienda kwa amri yake.” (38:36).

Basi akatabasamu akicheka kwa kauli yake, akasema: Ewe Mola wangu! Nizindue niishukuru neema yako uliyonineemesha na wazazi wangu na nipate kutenda mema unayoyaridhia na uniingize kwa rehe- ma yako katika waja wako wema.

Suleiman alipoomba ufalme ambao hataupata yeyote baada yake, alikusudia kuwatumia majini, upepo, ndege n.k. Kwa sababu ni wengi waliomakinika katika ardhi.

Suleiman alipofika kwenye bonde la chungu na upepo kuchukua maneno ya chungu hadi masikioni mwake na kufahamu maana yake, alitambua kuwa haya ni katika ambayo hatakuwa nayo yeyote baada yake.

Basi aliihisi raha kwa neema hii na akatekeleza haki yake ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kutambua tu, kwamba neema hii inatoka kwa Mwenyezi Mungu ni aina ya shukrani. Na shukrani kubwa zaidi ni kufanya kheri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Kama ambavyo Aya inafahamisha kuwa Suleiman ana dola na jeshi lake na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa elimu ya kujua lugha ya chungu; vile vile Aya inafahamisha kuwa chungu naye ana dola yake na raia zake na kwamba Mwenyezi Mungu naye amempa elimu ya kuwajua baadhi ya binadamu na majina yao. Kama si hivyo alijuaje kuwa huyu anayekuja na msafara wa jeshi ni Suleiman bin Daud?

Hakika mdudu huyo aliyewaambia wenzake, alikuwa mkubwa katika ulimwengu wake, kama alivyokuwa Suleiman katika ulimwengu wake. Na kwamba alikuwa akiwafanyia uadilifu raia wake, akiwahurumia, kujali masilahi yao na kutekelza haki kamili ya uongozi, kama anavyofanya Suleiman na viongozi wengineo waadilifu na wa haki.

Mwenye kuchunguza na kutaamali tukio la chungu na Suleiman atafikia kwenye somo na mazingatio yafuatayo:-

1. Nidhamu na mpangilio uko kwenye viumbe vyote; kuanzia kidogo, kama chunguchungu, hadi kikubwa, kama sayari. Hakuna tafisiri ya nid- hamu hii ya hali ya juu na mpangilio huu wa ajabu isipokuwa kuweko Muweza aliye Mjuzi: “Na ameumba kila kitu na akikadiria kipimo.” Juz. 18 (25:2).

2. Ushirikiano na kutambua majukumu, hakuhusuki na watu tu, bali hata kwa wanyama, ndege, wadudu n.k. Kijichembe hiki ambacho mara nyingine hata hakionekani kwa macho, kilipohisi hatari kwa jamaa zake, kilisimama kuwahadharisha kikisema: ‘ingieni maskani yenu, asije akawaponda Suleiman na jeshi lake.’ Wataalamu wameleta ushahidi mwingi wa hakika hii ya maisha ya wanyama.

3. Mtu ni lazima ashukuru anaponeemeshwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa elimu, utawala au mengine. Amshukuru Mwenyezi Mungu na awanyenyekee watu; sio kujivuna na kujiona kwa wengine kwa sababu ya neema ya Mwenyezi Mungu.

Pia, mtu akineemeka, inatakikana ajue kwamba Mwenyezi Mungu amekwishaitoa neema kama hiyo au kushinda hiyo kwa kiumbe kilicho dhaifu zaidi; na binadamu sio peke yake anayeneemeshwa na Mwenyezi Mungu.

Uvumbuzi wa elimu umegundua kuwa kuna maumbile makubwa zaidi ya haya tuyaonayo; hakuna hata mmoja anayeweza kujua hakika yake isipokuwa Muumba. Binadamu si chochote katika maumbile hayo. Hayo yanaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ {57}

“Bila shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu.” (40:57).

Kwa hiyo basi, Aya:

وَاللَّهُ يَخْتَصُّ بِرَحْمَتِهِ مَنْ يَشَاءُ ۚ {105}

“Na Mwenyezi Mungu humhusisha kwa rehema zake amtakaye.” Juz. 1 (2:105),

تُؤْتِي الْمُلْكَ مَنْ تَشَاءُ {26}

“Humpa ufalme umtakaye.” Juz. 3 (3:26)

وَإِنْ مِنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ {24}

“Na hapana umma wowote ila ulipata muonyaji.” (35:24)

Zote hizi, na mfano wake, zinaenea kwa binadamu na wasiokuwa binadamu.

Ikumbukwe kwamba Mwenyezi Mungu amelitumia neno umma kwa wasiokuwa binadamu; kama kauli yake: Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake, ila ni umma kama nyinyi.” Juz. 7 (6:38).

وَتَفَقَّدَ الطَّيْرَ فَقَالَ مَا لِيَ لَا أَرَى الْهُدْهُدَ أَمْ كَانَ مِنَ الْغَائِبِينَ {20}

Na akawakagua ndege na akasema: Mbona simwoni Hud-hud au amekuwa miongoni mwa walio ghaibu.

لَأُعَذِّبَنَّهُ عَذَابًا شَدِيدًا أَوْ لَأَذْبَحَنَّهُ أَوْ لَيَأْتِيَنِّي بِسُلْطَانٍ مُبِينٍ {21}

Kwa yakini nitamwadhibu kwa adhabu kali au nitamchinja, au aniletee hoja iliyo wazi.

فَمَكَثَ غَيْرَ بَعِيدٍ فَقَالَ أَحَطْتُ بِمَا لَمْ تُحِطْ بِهِ وَجِئْتُكَ مِنْ سَبَإٍ بِنَبَإٍ يَقِينٍ {22}

Basi hakukaa sana mara akasema: Nimegundua usiloligundua na nimekujia na habari za yakini kutoka Sabai.

إِنِّي وَجَدْتُ امْرَأَةً تَمْلِكُهُمْ وَأُوتِيَتْ مِنْ كُلِّ شَيْءٍ وَلَهَا عَرْشٌ عَظِيمٌ {23}

Hakika nimemkuta mwanamke anayewatawala na amepewa kila kitu na anacho kiti cha enzi kikubwa.

وَجَدْتُهَا وَقَوْمَهَا يَسْجُدُونَ لِلشَّمْسِ مِنْ دُونِ اللَّهِ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ فَهُمْ لَا يَهْتَدُونَ {24}

Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia njia. Kwa hivyo hawakuongoka.

أَلَّا يَسْجُدُوا لِلَّهِ الَّذِي يُخْرِجُ الْخَبْءَ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُخْفُونَ وَمَا تُعْلِنُونَ {25}

Kwamba hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyofichikana katika mbingu na ardhi na huyajua mnayoyaficha na mnayoyadhihirisha.

اللَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ۩ {26}

Mwenyezi Mungu hapana Mola ila Yeye Mola wa arshi tukufu.