Table of Contents

Aya 176 – 191:Shua’yb

Maana

Kisa cha Shua’yb kimetangulia katika Juz. 8 (7: 85) na Juz. 12 (11:84 – 95).

Watu wa mwituni waliwakadhibisha mitume. Alipowaambia Shua’yb: Je, hamna takua?

Wafasiri wamesema kuwa watu wa mwituni ni watu waliokuwa karibu na Madyan kwenye miti mingi.

Alipowaambia Shua’yb: Je, hamna takua?

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakusema ndugu yao Shua’yb, kama alivyosema ndugu yao Hud, Swaleh na Lut, kwa sababu Shua’yb si mtu wa hapo kinasabu wala hana uhusiano wowote na watu wa mwituni, isipokuwa ujirani. Mwenyezi Mungu alimtuma kwao; kama alivyomtuma kwa watu wake wa Madyan.

Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Aya hizi zimetanguliwa kwa herufi zake kupitia mdomoni mwa Nuh, Hud, Swaleh na Lut. Hayo ni maneno ya kila Nabii.

Timizeni kipimo sawasawa wala msiwe miongoni mwa wanaopunja.
Na pimeni kwa mizani iliyo sawa. Wala msiwapunguzie watu vitu vyao, Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7: 85) na Juz. 12 (11:84)

Na mcheni aliyewaumba nyinyi na vizazi vilivyotangulia.

Yaani mhofie adhabu ya Mwenyezi Mungu aliyewaumba nyinyi na wale waliotangulia.

Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa tu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Aya 153 ya sura hii.

Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi, na kwa hakika tunakuona ni katika waongo.

Yaani wewe unakusudia uwongo katika madai yako ya utume, kwa dalili ya kuwa wewe ni mtu unayekula chakula na kutembea sokoni. Lau wahyi ungeliwashukia watu basi watu wote wangelikuwa Mitume.

Ibn Hisham katika kitabu Al-Mughni, katika kuelezea watu wasiofaliwa na maneno yoyote, anasema: “Mtu mmoja alimwambia mwengine: ‘Baba yako amemfanyaje punda wako?’ Akasema: ‘Amemuuzo’ akiwa na maana amemuuza. Yule muulizaji akasema kwa mshangao: kwa nini umeweka o kwenye herufi ya mwisho? yule akajibu: si wewe umeweka o kwenye herufi ya mwisho!” Mtu wa namna hii utamwambiaje?

Basi tuangushie kipande cha mbingu, ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

Aliwahadharisha na adhabu wakamdharau na wakasema iko wapi hiyo adhabu unayotutisha nayo, basi teremsha kipande cha mbingu kiwe ni adhabu, ukiwa ni mkweli wa madai yako.

Akasema: Mola wangu anajua zaidi mnayoyatenda na amri ni yake peke yake, akitaka ataileta haraka au ataicheleweshwa. Basi wakamkadhibisha, ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubainisha kivuli hicho. Wafasiri wanasema ni mawingu waliyoyafanya kivuli kutokana na joto lililowapata, kisha yakawanyeshea mvua ya moto iliyowaunguza wote.

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya Sura hii na pia sehemu iliyopita.

وَإِنَّهُ لَتَنْزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ {192}

Na hakika hiyo ni uteremsho wa Mola wa walimwengu wote.

نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ {193}

Ameiteremsha Roho mwaminifu.

عَلَىٰ قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنْذِرِينَ {194}

Juu ya moyo wako, ili uwe katika waonyaji.

بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُبِينٍ {195}

Kwa ulimi wa kiarabu ulio wazi.

وَإِنَّهُ لَفِي زُبُرِ الْأَوَّلِينَ {196}

Na hakika hiyo iko katika vitabu vya kale.

أَوَلَمْ يَكُنْ لَهُمْ آيَةً أَنْ يَعْلَمَهُ عُلَمَاءُ بَنِي إِسْرَائِيلَ {197}

Je haikuwa kwao ni ishara kwamba wanayajua haya maulama wa wana wa Israil?

وَلَوْ نَزَّلْنَاهُ عَلَىٰ بَعْضِ الْأَعْجَمِينَ {198}

Lau tungeliitermsha juu ya mmoja wa wasiokuwa waarabu.

فَقَرَأَهُ عَلَيْهِمْ مَا كَانُوا بِهِ مُؤْمِنِينَ {199}

Na akawasomea wasingelikuwa wenye kuiamini.

كَذَٰلِكَ سَلَكْنَاهُ فِي قُلُوبِ الْمُجْرِمِينَ {200}

Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.

لَا يُؤْمِنُونَ بِهِ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ {201}

Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.

فَيَأْتِيَهُمْ بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ {202}

Basi itawafikia ghafla na hali hawaitambui.

فَيَقُولُوا هَلْ نَحْنُ مُنْظَرُونَ {203}

Na watasema: Je sisi tutapewa muda?

أَفَبِعَذَابِنَا يَسْتَعْجِلُونَ {204}

Basi je wanahimiza adhabu yetu?

أَفَرَأَيْتَ إِنْ مَتَّعْنَاهُمْ سِنِينَ {205}

Unaonaje, kama tukiwastarehesha kwa miaka.

ثُمَّ جَاءَهُمْ مَا كَانُوا يُوعَدُونَ {206}

Kisha yawafikie waliyokuwa wakiahidiwa.

مَا أَغْنَىٰ عَنْهُمْ مَا كَانُوا يُمَتَّعُونَ {207}

Hayatawafaa yale waliyostareheshewa.

وَمَا أَهْلَكْنَا مِنْ قَرْيَةٍ إِلَّا لَهَا مُنْذِرُونَ {208}

Wala hatukuuangamiza mji wowote ila ulikuwa na waonyaji.

ذِكْرَىٰ وَمَا كُنَّا ظَالِمِينَ {209}

Kuwa ni ukumbusho wala hatukuwa sisi ni wenye kudhulumu.

وَمَا تَنَزَّلَتْ بِهِ الشَّيَاطِينُ {210}

Wala mashetani hawakuteremka nayo.

وَمَا يَنْبَغِي لَهُمْ وَمَا يَسْتَطِيعُونَ {211}

Wala haiwapasi wala hawaiwezi.

إِنَّهُمْ عَنِ السَّمْعِ لَمَعْزُولُونَ {212}

Hakika wao wametengwa na kusikia.