Table of Contents

Aya 192 – 212: Ameitermsha Roho Mwaminifu

Maana

Na hakika hiyo ni uteremsho wa Mola wa walimwengu wote. Ameiteremsha Roho mwaminifu juu ya moyo wako, ili uwe katika waonyaji.

Hiyo ni Qur’an. Roho mwaminifu ni Jibril (a.s.) na maneno yanelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.).

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja visa vya mitume katika Aya zilizotangulia, sasa anamtaja Muhammad na Qur’an na kwamba Jibril ameitermsha kwa Mtume mtukufu ili apambane na makafiri na wapinzani kwa Aya zake na ubainifu wake. Jibril ameitwa roho kwa sababu ameiteremsha Qur’an ambayo ni uongofu na ponyo kwa roho:

هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ۖ {44}

“Hiyo ni uwongofu na ponyo kwa wenye kuamini.” (41:44).

Na ameitwa mwaminifu kwa sababu ni mtiifu kwa Mwenyezi Mungu, akiwa na biidii ya kuufikisha ujumbe wake kwa mitume, kama ulivyo. Yeye vile vile anaujua huo ujumbe na malengo yake.

Kwa ulimi wa kiarabu ulio wazi.

Katika Juz. 12 (12:2) tumebainisha sababu za kushuka Qur’an kwa lugha ya kiarabu, tazama huko.

Na hakika hiyo iko katika vitabu vya kale.

Yaani vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyotangulia, vilimbashiria Muhammad (s.a.w.) na Qur’an. Huko nyuma tulithibitisha dalili za kiakili na kinakili kwamba Qur’an ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Katika dalili za kiakili ni kwamba Qur’an iliwashinda wapinzani hata kuleta mfano mmoja tu wa Sura zake. Walijaribu wakashindwa. Na kwamba inatolea habari mambo ya ghaibu na yakatokea. Pia hiyo Qur’an inachukua njia nyingi za tafsiri. Wala hakuna siri ya hili ila ni kwa kuwa inatoka kwa ambaye amekizunguka kila kitu kwa ujuzi. Tazama Juz. 1 (2: 23) Juz. 5 (4:53 na 82) na Juz. 18 (24:55).

Ama dalili za kinukuu, miongoni mwazo ni Tawrat na Injili za asili, zilizoleta bishara ya Muhammad. Tazama Juz. 9 (7: 157). Vile vile vitabu vingine vya mbinguni vilitoa habari ya kuja Muhammad. Tazama Juz. 1 (2:46).
Je, Haikuwa kwao ni ishara kwamba wanayajua haya maulama wa wana wa Israil?

Maulama wa kiyahudi, kabla ya kutumwa Mtume (s.a.w.), walikuwa wakimbashiria Muhammad; wakiwazungumzia waarabu kuhusiana naye na kutaja sifa zake kwa makuraishi na wengineo. Alipokuja wakasilimu baadhi ya Mayahudi waliokuwa wakimzungumzia; kama vile Abdallah bin Salaam na wenzake. Vile vile wakasilimu jamaa katika waarabu na wakampinga mayahudi wengine na vigogo katika makuraishi.

Aya hii inawaambia wale waliomkadhibisha Muhammad (s.a.w.) baada ya kusikia hadith ya mayahudi kumhusu. Inawaambia, vipi mnamkadhibisha na hali mmewasikia maulama wa kiyahudi kabla, wakimtolea habari, wakikiri kuwa ametajwa katika Tawrat? Ushahidi wao huo hauwatoshi kuwa ni dalili ya ukweli wa Muhammad (s.a.w.)?

Hakuna mwenye shaka kwamba dalili hii ni tosha kwa mwenye kuitafuta haki kwa njia ya haki, lakini vigogo ambao walipinga utume wa Muhammad (s.a.w.) walifanya hivyo kwa sababu ya masilahi yao; sio kwa sababu ya udhaifu wa hoja na dalili:

وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَنْ قَوْمٍ لَا يُؤْمِنُونَ {101}

“Na dalili na maonyo hayawafai watu wasioamini.” Juz. 11 (10:101).

Lau tungeliiteremsha juu ya mmoja wa wasiokuwa waarabu na akawasomea, wasingelikuwa wenye kuiamini.

Wao hawaiamini haki na ubainifu wake, iwe imekuja na mwarabu au asiyekuwa mwarabu. Kwa sababu haki na elimu kwao ni masilahi; vinginevyo si chochote kwao. Tumelikariri hilo mara nyingi pamoja na uwazi wake.

Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.

Yaani wakosefu wanapoisikia haki au Qur’an wanaipinga na kuikanusha. Kwa maneno mengine ni kuwa mbengu inaota vizuri kwenye ardhi iliyo na rutuba, lakini ikiwa ardhi si nzuri, basi uotaji wake utakuwa hauna manufaa:

وَالْبَلَدُ الطَّيِّبُ يَخْرُجُ نَبَاتُهُ بِإِذْنِ رَبِّهِ ۖ وَالَّذِي خَبُثَ لَا يَخْرُجُ إِلَّا نَكِدًا ۚ {58}

“Na mji mzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake. Na ule ulio mbaya hautoi ila kwa taabu tu.” Juz. 8 (7:58).

Kadhalika haki inaleta matunda na athari ikisadifu kuwa kwenye nafsi safi na haileti chochote ikiwa kwenye nafsi chafu. Maana ni kuwa Qur’an haina athari yoyote katika nafsi zao isipokuwa upinzani na kukadhibisha.

Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu. Basi itawafikia ghafla na hali hawaitambui.

Wakosefu hawaiamini Qur’an. Yaani wao hawaiamini haki hata ikiwa na dalili kiasi gani ila ikiwafikia adhabu kwa ghafla. Na wakionywa kabla wanaifanyia masihara. Ilivyo ni kwa kunyenyekea wakati wa kuona adhabu ni unafiki na ni kulazimishwa sio hiyari.

Na watasema: Je sisi tutapewa muda?

Waliiharakia adhabu kabla ya kuiona na wakamwambia Mtume wao ilete ukiwa ni katika wakweli. Walipoiona kwa macho walijuta na wakatamani lau wangelipewa muda ili waamini na watii. Ndivyo alivyo mpotevu; anatamani kurudi au kupewa muda baada ya kupita wakati.

Basi je wanahimiza adhabu yetu?
Haya ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwajibu wale waliomwambia Mtume wao. Tuangushie kipande cha mbingu na tuletee yale uliyotuahidi. Maana yake ni kuwa vipi mnaiharakia adhabu na ikiwafikia hamuiwezi wala kuikwepa.

Unaonaje, kama tukiwastarehesha kwa miaka, kisha yawafikie waliyokuwa wakiahidiwa, hayatawafaa yale waliyostareheshewa?

Wakosefu watatamaani kupewa muda watakapoiona adhabu, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawajibu kwamba kupewa muda hakufai kitu hata kama muda utakuwa mrefu kiasi gani. Bali kila muda unavyokuwa mrefu ndio madhambi yanazidi na kuongezeka na kuzidi adhabu yao.

Wala hatukuuangamiza mji wowote ila ulikuwa na waonyaji.

Aya hii iko katika maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا {15}

Wala sisi hatuadhibu mpaka tupeleke Mtume.” Juz. 15 (17:15).

Kuwa ni ukumbusho wala hatukuwa sisi ni wenye kudhulumu katika kuangamiza miji, wakati ambapo tulituma waonyaji wa hiyo adhabu, na wakumbushaji wa twaa ya Mwenyezi Mungu wakiwa na dalili. Wakawakadhibisha ndio ikastahiki adhabu.

Wala mashetani hawakuteremka nayo wala haiwapasi wala hawaiwezi.

Watu wa wakati wa ujahili walikuwa wakiitakidi ukuhani; kwamba kila kuhani ana shetani wake anayemletea habari za ghaibu. Iliposhuka Qur’an wakasema kuwa inatoka kwa shetani kwenda kwa makuhani ambao nao wanampelekea Muhammad (s.a.w); au yeye mwenyewe ni kuhani anayeteremkiwa na shetani.

Ndipo Mwenyezi Mungu akayajibu madai haya, kuwa Qur’an ni uongofu, mwanga na ni ubainifu ulio wazi. Ni wapi na wapi ukuhani na ushetani kulinganisha na uongofu na ubainifu? Wao ni dhaifu na ni duni zaidi. Zaidi ya hayo ni kuwa hakika wao wametengwa na kusikia.

Wamezuiliwa kusikia Qur’an pale Mwenyezi Mungu anapompa Jibril kuileta kwa Muhammad (s.a.w.). Ikiwa mashetani wameshindwa kuleta hata Aya moja mfano wake na pia kusikiliza japo tamko moja, basi watainukuu vipi kwa makuhani na kuitolea habari?

فَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ فَتَكُونَ مِنَ الْمُعَذَّبِينَ {213}

Basi usimwombe Mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakaoadhibiwa.

وَأَنْذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ {214}

Na uwonye jamaa zako walio karibu.

وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ {215}

Na inamisha bawa lako kwa wanokufuata katika waumini.

فَإِنْ عَصَوْكَ فَقُلْ إِنِّي بَرِيءٌ مِمَّا تَعْمَلُونَ {216}

Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyafanya.

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ {217}

Na mtegemee Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ {218}

Ambaye anakuona unaposimama.

وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ {219}

Na mageuko yako katika wale wanaosujudu.

إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {220}

Hakika yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.