read

Aya 20 – 26: Mbona Simwoni Hud-Hud

Maana

Na akawakagua ndege na akasema: Mbona simwoni Hud-hud au amekuwa miongoni mwa walio ghaibu. Kwa yakini nitamwadhibu kwa adhabu kali au nitamchinja, au aniletee hoja iliyo wazi.

Suleiman alikuwa na aina ya ndege wanaofuata amri yake, wakiwa wako huru sio ndani ya tundu. Siku moja alipokuwa anawakaguakagua, kama anavyokagua kamanda jeshi lake, akamkosa Hud-hud, na hakuwa amemruhusu kundoka. Akatishia – mbele ya ndege wengine - kumwadhibu; kama kumtia jela n.k. Au kumuua, ikiwa hatakuwa na hoja wazi ya udhuru wa kutoweka kwake.

Basi hakukaa sana mara akasema: Nimegundua usiloligundua.

Haukupita muda wa kutishia Suleiman ila alikuja Hud-hud na akasema: Nimegundua kitu muhimu usichokijua pamoja na upana wa elimu yako na nimekujia na habari za yakini kutoka Sabai.

Hakika nimemkuta mwanamke anayewatawala na amepewa kila kitu na anacho kiti cha enzi kikubwa.

Makusudio ya Sabai (Sheba) ni watu wanaonasibika na Sabai bin Yashjab bin Ya’rub bin Qahtan. Mwanamke (Malkia wa Sheba) alikuwa ni Bilqis bint Sharahil, aliyekuwa mfalme na kurithiwa na binti yake huyo, aliyekuwa akimiliki utajiri na starehe zote.

Alikuwa akikaa kwenye kiti cha hali ya juu na cha thamani, kikiwa kimepambwa na nyoyo za maskini na kupakwa jasho lao na damu zao. Ajabu ni kauli ya baadhi ya wafasiri waliosema kuwa kilikuwa kimeezekwa na kwamba upana wake ulikuwa ni futi 80 za mraba na kimo chake pia ni futi 80.

Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia njia. Kwa hivyo hawakuongoka.
Unaweza kuuliza: Ndege, wanyama na wadudu kwa maumbile yao wanajua chakula chao, kinywaji chao, kinachowadhuru na kinachowanufaisha. Wanajua hivyo na vinginevyo kwa sababu ndio nyenzo za kuishi kwao, kuhifadhi maisha yao na kuendela kuwepo.

Lakini kumtambua mume na mke katika binadamu, kujua kuwa kabila hili ni la wasabai na lile ni la Thamud, kujua hawa wanamuamini Mwenyezi Mungu na wale ni makafiri, haya yote hayalingani na maisha yao kwa umbali wala karibu.

Basi Hud-hud aliwezaje kujua jina la kabila, mwanamke anayewatawala na kwamba wao wanaabudu jua? Sisi wanadamu tu, hatuwezi kutambua baina ya mume na mke katika aina nyingi za ndege, wadudu na wanyama?

Jibu: Aya imethibitisha sifa hizi kwa Hud-hud wa Suleiman tu, jambo ambalo halilazimishi kuthibiti katika ndege wote au kwa Hud-hud wote; kama ambavyo kujua kiingereza kwa mtu fulani hakulazimishi kujua kiingereza kwa watu wote. Ama maarifa ya Hud-hud wa Suleiman kwa aliyoyatolea habari, sisi hatuna tafsiri yake isipokuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu.

Kwamba hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyofichikana katika mbingu na ardhi na huyajua mnayoyaficha na mnayoyadhihirisha.

Makusudio ya yaliyofichikana hapa ni kheri za ulimwengu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) huzitoa kwa waja wake kwa sababu zake za kimaumbile; kama mimea inayotoka ardhini kwa sababu ya mvua, kuzaana kwa sababu ya kupandishwa au kwa nyenzo nyingine za kielimu anazozitoa Mwenyezi Mungu kupitia mikononi mwa wataalamu na vifaa vyao.

Sababu na nyenzo zote hizi, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameziletea ibara ya mkono wa Mungu pale aliposema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُمْ مِمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ {71}

“Je, hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki?” (36:71).

Mwenyezi Mungu hapana Mola ila Yeye Mola wa arshi tukufu, ambaye haufananishwi ufalme wake wala ukuu wake na wa yeyote.

قَالَ سَنَنْظُرُ أَصَدَقْتَ أَمْ كُنْتَ مِنَ الْكَاذِبِينَ {27}

Akasema: Tutatazama, umesema kweli au uko katika waongo.

اذْهَبْ بِكِتَابِي هَٰذَا فَأَلْقِهْ إِلَيْهِمْ ثُمَّ تَوَلَّ عَنْهُمْ فَانْظُرْ مَاذَا يَرْجِعُونَ {28}

Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini.”

قَالَتْ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ إِنِّي أُلْقِيَ إِلَيَّ كِتَابٌ كَرِيمٌ {29}

Akasema: Enyi waheshimiwa! Hakika imeletwa kwangu barua tukufu.

إِنَّهُ مِنْ سُلَيْمَانَ وَإِنَّهُ بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ {30}

Imetoka kwa Suleiman, nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

أَلَّا تَعْلُوا عَلَيَّ وَأْتُونِي مُسْلِمِينَ {31}

Kwamba msinifanyie jeuri na fikeni kwangu mkiwa waislamu.

قَالَتْ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَفْتُونِي فِي أَمْرِي مَا كُنْتُ قَاطِعَةً أَمْرًا حَتَّىٰ تَشْهَدُونِ {32}

Akasema: Enyi waheshimiwa! Nipeni ushauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri lolote mpaka muhudhurie.

قَالُوا نَحْنُ أُولُو قُوَّةٍ وَأُولُو بَأْسٍ شَدِيدٍ وَالْأَمْرُ إِلَيْكِ فَانْظُرِي مَاذَا تَأْمُرِينَ {33}

Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali wa vita, na amri iko kwako, basi tazama nini unaamrisha.

قَالَتْ إِنَّ الْمُلُوكَ إِذَا دَخَلُوا قَرْيَةً أَفْسَدُوهَا وَجَعَلُوا أَعِزَّةَ أَهْلِهَا أَذِلَّةً ۖ وَكَذَٰلِكَ يَفْعَلُونَ {34}

Akasema: Hakika wafalme wanapouingia mji wanauharibu na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge, na hivyo ndivyo watendavyo.

وَإِنِّي مُرْسِلَةٌ إِلَيْهِمْ بِهَدِيَّةٍ فَنَاظِرَةٌ بِمَ يَرْجِعُ الْمُرْسَلُونَ {35}

Na mimi ninawapelekea zawadi ningoje watakayorudi nayo wajumbe.