Table of Contents

Aya 21 – 29: Hakuna Furaha Kwa Wakosefu

Maana

Na walisema wale wasiotarajia kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu.

Bado maneno yanaendelea kuwahusu washirikina, wasiotarajia kukutana na Mola wao, wala kuhofia adhabu yake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.), katika Aya hii, amewazungumzia kwamba wao wamependekeza washuke Malaika ili wawape habari kuwa Muhammad ni Nabii au aje Yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu atoe habari hiyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:92) .

Hakika wametakabari katika nafsi zao na wameasi uasi mkubwa.

Kuna kiburi gani kikubwa zaidi kuliko jeuri yao hii ya kutaka kumuona Mungu na kuzungumza naye ana kwa ana? Hawa hawana tofauti na wale waliosema kuwa hatumwamini Mungu mpaka tumuone, wakati huo wanaamini vitu ambavyo haviingii katika hisia yoyote.

Watu wa kimaada wanadai kuwa hakuna kitu chochote isipokuwa asili pofu ambayo ilijileta yenyewe au ilipatikana kwa sadfa, na ndiyo iliyoupangilia ulimwengu huu wa ajabu na iliyoumba usikizi na uoni. Katika mantiki yao ni kwamba asili ndiyo iliyo na uwezo wa kila kitu, lakini hiyo yenyewe haitambui kitu.

Wao wanajipinga wenyewe, kwa sababu kukubali kwao kupatikana nidhamu, ni kukiri kuweko nguvu yenye uwezo na ujuzi; na kusema kwao kuwa hakuna chochote isipokuwa asili pofu ni kuikana nguvu hiyo. Maana yake ni kuwa asili ina utambuzi na haina utambuzi, inajua na haijui.

Siku watakayowaona Malaika, haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu.

Washirikina walipendekeza washukiwe na malaika, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawajibu kuwa kutakuwa na siku ambayo watawaona malaika, Siku ya Kiyama, lakini hakutakuwa na jambo la kuwafurahisha , bali ni majanga juu ya majanga yatakayowapata:

يَوْمَ يَغْشَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ فَوْقِهِمْ وَمِنْ تَحْتِ أَرْجُلِهِمْ وَيَقُولُ ذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {55}

“Siku itakapowafunika adhabu kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema: Onjeni hayo mliyokuwa mkiyatenda” (29:55).

Na watasema: Kuwe na kizuizi kizuiacho.

Watakaosema ni malaika. Maana ni kuwa malaika watawaambia wakosefu, leo ni haramu mtazuiwa kuona mnayoyataka.

Imesemekana kuwa watakaosema ni wakosefu kuwaambia malaika kuwa haifai nyinyi leo kutuudhi na kutuadhibu.

Tafsiri zote mbili zinafaa na zinarejea kwenye maana moja ambayo ni kuhofia wakosefu shari ya siku ya Kiyama na vituko vyake.

Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo, waliyodhani kuwa yatawafaa leo, kisha tutayafanya mavumbi yaliyotawanyika.

Kwa sababu yalikuwa kwenye misingi isiyokuwa ya imani wala ikhalsi: “Mfano wa wale ambao wamemkufuru Mola wao vitendo vyao ni kama majivu yanayopeperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya kimbunga. Hawana uwezo wa chochote juu ya walichokichuma. Huko ndiko kupotelea mbali.” Juz. 13 (14:18).

Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makazi bora na mapumziko mazuri zaidi.

Makusudio ya bora na zaidi sio uzaidi wa mengine, isipokuwa makusudio ni kuwa makazi na mapumziko hayo yenyewe ni bora na mazuri; ni kama kusema Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi, kwa maana ya kuwa ni mkubwa zaidi katika dhati yake na sifa zake.

Siku itakapopasuka mbingu kwa mawingu.

Makusudio ya siku hapa ni Siku ya Kiyama; na mawingu ni sayari ambazo zitakuwa chembechembe zisizoweza kuonekana hata kwa macho, zitaijaza anga, kama vile mawingu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameashiria kuharibika kwa Siku hiyo, kwenye Aya nyingi; kama vile:

إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ {1}

“Jua litakapokunjwa.” (81:1),

وَإِذَا الْكَوَاكِبُ انْتَثَرَتْ {2}

“Na nyota zitakapotawanyika.” (82:2).

Yaani jua litakapozimika na nyota zitakapoanguka.”

Na watateremshwa malaika kwa wingi, wakiwa na ya kuwafurahisha wema na kuwachukiza wakosefu.

Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Mwingi wa rehema Yeye tu peke yake, hakuna atakayekuwa na lolote.

Na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.

Hakuna siku ngumu zaidi kwa mkosefu kuliko siku ya kuhukumiwa kwake, kuhisabiwa makosa yake na kutolewa hukumu ya haki na uadilifu? Lau angelihukumiwa kunyongwa ingelikuwa mambo yamekwisha, lakini ni hukumu ya kudumu:

كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُمْ بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا لِيَذُوقُوا الْعَذَابَ ۗ {56}

“Kila zitakapoiva ngozi zao, tutawabadilishia ngozi nyingine ili waonje adhabu.” Juz.5 (4:56).

Na siku dhalimu atajiuma mikono yake akisema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume!

Hiki ni kinaya cha majuto na masikitiko. Hapo ndio ukomo wa kila mwenye kughurika, mzushi na muongo. Miongoni mwa dua zilipokewa kutoka kwa Nabii (s.a.w.) ni: “Ewe Mola wangu! Najilinda kwako na madhambi yanayoleta majuto.”

Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki.

Makusudio ya fulani hapa ni kila mwenye kufuatwa aliyempoteza mfuasi wake na kumwongoza kwenye maangamizi. Kuna Hadith isemayo: “Mtu atafufuliwa kwenye dini ya rafiki yake.”

Jamaa katika wafasiri wamesema kuwa Aya hii ilimshukiwa Uqba bin Mu’it na Ubayya bin Khalaf. Kwamba dhalimu atakayeuma mikono yake ni huyo wa kwanza na fulani ni huyo wa pili. Hata kama tukikadiria usahihi wa riwaya, ni kuwa sababu ya kushuka Aya haizuwii kuenea kwa wengine.

Hakika amenipoteza nikaacha dhikri baada ya kunijia, na shetani ndiye anayemtupa mtu.

Makusudio ya dhikri hapa ni Qur’an, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amelitumia neno hili kwa kukusudia Qur’an katika Aya kadhaa; kama vile:

ص ۚ وَالْقُرْآنِ ذِي الذِّكْرِ {1}

“Naapa kwa Qur’an yenye dhikri.” (38:1).

Aya inafahamisha kuwa wale walioisikiza Qur’an walikinai kwenye nafsi zao, lakini mashetani-watu waliwadanganya na wakawaepusha na haki, ikawa mwisho wao ni kufedheka. Na huu ndio mwisho wa kila mwenye kufanya kwa maelekezo ya watu wa hawa, si kwa maelekezo ya imani yake na dhamiri yake.

وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا {30}

Na Mtume alisema: Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’an ni mahame.

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِنَ الْمُجْرِمِينَ ۗ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ هَادِيًا وَنَصِيرًا {31}

Na hivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu. Na Mola wako anatosha kuwa mwenye kuongoza na mwenye kunusuru.

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَةً ۚ كَذَٰلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ ۖ وَرَتَّلْنَاهُ تَرْتِيلًا {32}

Na walisema wale ambao wamekufuru: Mbona haikuteremshwa kwake Qur’an yote mara moja? Ndivyo hivyo, ili tuuimarishe kwayo moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا {33}

Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyonzuri.

الَّذِينَ يُحْشَرُونَ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ إِلَىٰ جَهَنَّمَ أُولَٰئِكَ شَرٌّ مَكَانًا وَأَضَلُّ سَبِيلًا {34}

Wale watakaokusanywa kifudifudi kwenye Jahannam, hao watakuwa mahali pabaya na ndio wenye kupotea njia sana.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَجَعَلْنَا مَعَهُ أَخَاهُ هَارُونَ وَزِيرًا {35}

Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamuweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri.

فَقُلْنَا اذْهَبَا إِلَى الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَدَمَّرْنَاهُمْ تَدْمِيرًا {36}

Tukawaambia nendeni kwa watu waliozikadhibisha Ishara zetu, basi tukawaangamiza kabisa.

وَقَوْمَ نُوحٍ لَمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ وَجَعَلْنَاهُمْ لِلنَّاسِ آيَةً ۖ وَأَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ عَذَابًا أَلِيمًا {37}

Na watu wa Nuh walipowakadhibisha mitume, tuliwagharikisha na tukawafanya ni ishara kwa watu. Na tumewaandalia madhalimu adhabu chungu.

وَعَادًا وَثَمُودَ وَأَصْحَابَ الرَّسِّ وَقُرُونًا بَيْنَ ذَٰلِكَ كَثِيرًا {38}

Na kina Ad na Thamud na watu Rass na vizazi vingi vilivyokuwa baina yao.

وَكُلًّا ضَرَبْنَا لَهُ الْأَمْثَالَ ۖ وَكُلًّا تَبَّرْنَا تَتْبِيرًا {39}

Na wote tuliwapigia mifano na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.

وَلَقَدْ أَتَوْا عَلَى الْقَرْيَةِ الَّتِي أُمْطِرَتْ مَطَرَ السَّوْءِ ۚ أَفَلَمْ يَكُونُوا يَرَوْنَهَا ۚ بَلْ كَانُوا لَا يَرْجُونَ نُشُورًا {40}

Na kwa hakika wao walifika kwenye mji ulionyeshewa mvua mbaya, basi je hawakua wakiuona? Bali walikuwa hawatarajii kufufuliwa.