Table of Contents

Aya 213 – 220: Waonye Jamaa Zako Wa Karibu

Maana

Basi usimwombe Mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakaoadhibiwa.

Dhahiri ya mfumo wa maneno inaonyesha yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), lakini makusudio ni kutoa habari kuwa kila atakayemuomba Mungu mwingine zaidi ya Mwenyezi Mungu basi atakuwa ni mwenye kuadhibiwa kwa hali yoyote atakayokuwa.

Na uwonye jamaa zako walio karibu.

Mtume (s.a.w.) ni mwenye kuamrishwa kuwaonya watu wote:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ {1}

قُمْ فَأَنْذِرْ {2}

“Ewe uliyejigubika! Simama uonye.” (74:1 2),

عَجَبًا أَنْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ رَجُلٍ مِنْهُمْ أَنْ أَنْذِرِ النَّاسَ وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا{2}

“Kwamba tumempa wahyi mmoja wao, kuwa uwaonye watu na uwape bishara wale walioamini.” Juz. 11 (10:2).

Amehusisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja jamaa wa Mtume (s.a.w.), kwa sababu mwenye kutaka kutengeneza kwanza anajianza yeye mwenyewe, kisha jamaa zake, ndio wafuatie wengine. Jamaa zake wakimsadiki na kumwamini watamsaidia kueneza mwito wake.

Maneno ya Waislamu yamekuwa mengi kuhusiana na Aya hii. Jamaa katika Sunni wamesema kuwa iliposhuka Aya hii Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alisema: “Ewe Fatima bint Muhammad! Ewe Swafiya bint Abdul Muttwalib! Enyi wana wa Abdillah! Fanyeni amali, kwani mimi siwatoshelezei chochote kwa Mwenyezi Mungu.

Shia na jamaa wengie wa kisunni; akiwemo: Ahmad bin Hambal, An-Nasai, As-Suyutwi, Abu Na’im Al-Baghwi, Atha’alabi, mwenye kitabu Assiratul-halabiya, mwenye kitabu Kanzul-u’mmal na wengineo, wamesema kuwa, iliposhuka Aya hii, Mtume (s.a.w.) aliwaita watu wa ukoo wa Abdul-Muttwalib. Wakati huo walikuwa ni watu arobaini, wakiwemo maami zake: Abu Twalib, Hamza, Abbas na Abu Lahab.
Alikuwa amewaandalia karamu. Baada ya kula na kunywa, akasema: “Enyi wana wa Abdul-Muttwalib! Nimewaletea kheri ya duniani na Akhera na Mwenyezi Mungu ameniamrisha nitoe mwito wa hilo. Basi ni nani atakayenisaidia kwenye jambo hili, awe ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu?”

Wakanyamaza wote, isipokuwa Ali (a.s.) akasema: “Mimi ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu.” Basi akamshika shingoni na akasema: “Hakika huyu ni ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu. Basi msikilizeni na mumtii1.”

Tukio hili alilitaja Muhammad Haykal katika kitabu chake Hayatu Muhammad, chapa ya kwanza na akaliondoa katika chapa ya pili.

Abu Hayyan Al-Andalusi katika Bahrul-muhit, anasema: “Zimepokewa Hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kuhusiana na hilo.” Anaashiria Hadith zilizomtaja Imam Ali na zile ambazo hazikumtaja. Wala hakuna kupingana baina ya Hadith hizi.

Kwa sababu kuzichanganya pamoja ni jambo linalowezekana na la karibu sana. Mtume (s.a.w.) aliwaandalia chakula watu arobaini katika jamaa zake na kuwaambia ni nani atakayenisaidia … kisha pia akawaambia mimi siwatoshelezi lolote kwa Mwenyezi Mungu.

Na inamisha bawa lako kwa wanokufuata katika waumini.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (15:88).

Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyafanya.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), awaambie wale jamaa zake aliowaonya. ‘Aliye karibu na Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni yule aliyekurubishwa na takua. Na aliye mbali na Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni yule aliyewekwa mbali na maasi, kwa namna yoyote atakavyokuwa’

Na mtegemee Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu na uachane nao wakikuasi; wala roho isikutoke juu yao, na uelekee kwa Mwenyezi Mungu peke yake katika mambo yako yote.

Ambaye anakuona unaposimama kwenye tahajjud (Swala za usiku wa manane) na mageuko yako katika wale wanaosujudu.

Shia Imamiyya wanasema kuwa mababa wote wa Mtume walikuwa wakimpwekesha Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa dalili zao katika hilo ni Aya hii; walipofasiri mgeuko kwa maana ya mgeuko wake katika migongo ya wanaompwekesha Mungu; yaani kupitia mifupani mwao.

Tamko la Aya linakubaliana na maana haya na pia linakubaliana na tafsiri ya anayesema kuwa Mungu anakuona ukiwa pamoja na wanaoswali. Dhahiri ya mfumo wa maneno inafahamisha tafsiri hii zaidi kuliko ile.

Hakika yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

Anasikia kauli na anajua siri na vitendo vyote na kuvilipa. Vikiwa ni kheri basi ni kheri na vikiwa ni shari basi ni shari.

هَلْ أُنَبِّئُكُمْ عَلَىٰ مَنْ تَنَزَّلُ الشَّيَاطِينُ {221}

Je niwaambie ambao mashetani wanawashukia?

تَنَزَّلُ عَلَىٰ كُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ {222}

Wanamshukia kila mzushi mkubwa, mwingi wa dhambi.

يُلْقُونَ السَّمْعَ وَأَكْثَرُهُمْ كَاذِبُونَ {223}

Wanawapa masikio na wengi wao ni waongo.

وَالشُّعَرَاءُ يَتَّبِعُهُمُ الْغَاوُونَ {224}

Na washairi ni wapotofu ndio wanaowafuata.

أَلَمْ تَرَ أَنَّهُمْ فِي كُلِّ وَادٍ يَهِيمُونَ {225}

Je huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?

وَأَنَّهُمْ يَقُولُونَ مَا لَا يَفْعَلُونَ {226}

Na kwamba wao wanasema wasiyoyatenda?

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَذَكَرُوا اللَّهَ كَثِيرًا وَانْتَصَرُوا مِنْ بَعْدِ مَا ظُلِمُوا ۗ وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنْقَلَبٍ يَنْقَلِبُونَ {227}

Isipokuwa wale ambao wameaamini na wakatenda mema na wakamtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi na wakajitetea wanapodhulumiwa. Na punde watajua waliodhulumu ni mgeuko gani watakaogeuka.
  • 1. Tazama A’yanushia cha Amin Juz. 3 uk. 110 chapa ya 1960 na Dalailu-sswidq cha Mudhwaffar Juz. 2 Uk. 232 chapa ya 1954.