Table of Contents

Aya 221 – 227: Washairi Wanafuatwa Na Wapotofu

Maana

Qur’an inawapiga vita wabatilifu, lakini kabla ya chochote, kwanza inawapiga vita kwa mantiki ya kiakili iliyo salama na inawajadili kwa njia nzuri, huku ikiwalingania kwenye haki kwa hekima na mawaidha mazuri; ikifafanua kwa kila aina ya mfumo na kuwaomba, kwa upole na ulaini kabisa, walete hoja zao:

لَوْلَا يَأْتُونَ عَلَيْهِمْ بِسُلْطَانٍ بَيِّنٍ ۖ {15}

“Kwa nini hawawaletei dalili bayana?” Juz. 15 (18:15).

Wanapoleta hoja dhaifu, Qur’an huibatilisha na kubainisha udhaifu uliopo. Washirikina na watu wengi wanaojali masilahi yao tu, wamesema mengi kuhusiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Miongoni mwa madai yao ni kuwa Qur’an inatokana na shetani na pia kudai kuwa Muhammad (s.a.w.) ni mshairi. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawajibu kwa haya yafuatayo:

Je niwaambie ambao mashetani wanawashukia? Wanamshukia kila mzushi mkubwa, mwingi wa dhambi.

Hili ni jibu la kauli yao kuwa Qur’an ni katika wahyi wa shetani. Njia ya kujibu ni kuwa shetani anaingiza wasiwasi na ubatilifu kwa waongo na wenye madhambi mfano wao: “Mashetani watu na majini. Baadhi yao wanawapa wenzao maneno ya kupambapamba kuwahadaa.” Juz. 8 (6:112).

Shetani hana njia kwa wa kweli na waaminifu, kama vile mitume na viongozi wema. Zaidi ya hayo ni kuwa ni kuwa Qur’an ni haki na kheri na mawazo ya shetani ni shari na uzushi.

Wanawapa masikio na wengi wao ni waongo.
Makusudio ya kuwapa masikio hapa ni kuwasikiliza. Wanaosikilizwa ni makafiri. Maana ni kuwa wale ambao wanawasikiliza mashetani na kuchukua kutoka kwao uwongo na ubatilifu ndio makafiri. Na makafiri wengi ni waongo katika mazungumzo yao na kauli zao. Muhammad (s.a.w.) ni mkweli katika kauli zake zote na vitendo vyake vyote; vipi aambiwe amesikiliza na kupokea kutoka kwa shetani?

Na washairi ni wapotofu ndio wanaowafuata. Je huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde na kwamba wao wanasema wasiyoyatenda?

Hii ni kuwajibu washirikina waliosema kuwa Muhammad ni mshairi. Njia ya kubainisha ni kuwa kuna tofauti kubwa baina ya washairi na Muhammad kwa njia hizi zifuatazo:

Kwanza, wale waliomfuata Muhammad (s.a.w.) walimfuata kwa kumwamini na kumwadhimisha. Na pia kumwamini Mwenyezi Mungu wakitarajia biashara isiyofilisika.

Ndio maana walimfidia kwa roho zao na wakapigana na mababa zao na watoto wao kwa ajili yake. Lakini washairi wao wanaishi katika njozi na kufikirika tu. Wakale walisema: “ushairi ni njozi ” wala hakuna anayewafuata hawa isipokuwa wale wanaoelekeana nao.

Pili, washairi wengi hapo zamani walikuwa wakiwasaidia viongozi madhalimu. Mshairi alikuwa akitumia kipawa chake na akili yake kutunga shairi au nyimbo itakayoimbwa mbele ya viongozi madhalimu. Sasa hili ni wapi na wapi na risala ya Muhammad (s.a.w.) ambayo hiyo yenyewe ni mapinduzi dhidi ya dhulma na ufisadi?

Tatu, kwamba washairi wengi wanasema sana na kutenda kidogo, wala hakiwapi umuhimu kitu isipokuwa hawa na malengo yao tu ndio yanayowapa msukumo yakiwalekeza popote yanapoelekea. Lakini Muhammad (s.a.w.) yeye hatamki kwa hawa yake wala hafuati isipokuwa wahyi kutoka kwa Mola wake. Sasa vipi ataambiwa ni mshairi:

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنْبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُبِينٌ {69}

Wala hatukumfundisha mashairi, wala hayatakikani kwake. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur’an inayobainisha.” (36:69).

Unaweza kuuliza: Je hii haifahamishi kuwa Uislamu unapiga vita mashairi, kutokana na Qur’an kuyashutumu?

Jibu: Hapana! Qur’an haikushutumu shairi kama shairi au washairi kama washairi; isipokuwa imewashutumu washairi wanaoipinga haki na kufuata kombokombo. Ama washairi wanaoelezea matumaini ya wanyonge na kuwa pamoja na wanaodhulumiwa, kuusaidia uadilifu na uhuru wa binadamu na kupinga utaghuti, ujinga na kurudi nyuma, hawa wako katika safu ya wapigania jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliulizwa unasemaje kuhusu washairi? Akasema: “Hakika muumini ni mpigania jihadi kwa upanga wake na ulimi wake. Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, wao ni kama kwamba wanarusha mikuki.”

Aina ya mashairi ambayo ni mikuki katika nyoyo za madhalimu ndiyo aliyoikusudia Mtume (s.a.w.) katika kauli yake: “Hakika katika shairi kuna hekima.” Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Amemfundisha ubainifu.” (55:4).

Hakuna mwenye shaka kuwa ushairi ni fani ya hali ya juu ya ubainifu na fasihi, kama ambavyo ni utajiri wa lugha na hazina yake yenye thamani.

Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawavua washairi wema na wapigania jihadi kwa kusema:

Isipokuwa wale ambao wameaamini na wakatenda mema na wakamtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi na wakajitetea wanapodhulumiwa.
Yaani washairi wakiitetea haki na na watu wake kutokana na wachokozi na maadui na wakautetea uhuru wa ubinadamu na heshima yake.

Hii ni nukuu iliyo wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwamba shairi la kimapinduzi dhidi ya dhulma na uonevu ni katika umuhimu wa dini, imani na matendo mema.

Katika maana ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

لَا يُحِبُّ اللَّهُ الْجَهْرَ بِالسُّوءِ مِنَ الْقَوْلِ إِلَّا مَنْ ظُلِمَ ۚ {148}

“Hapendi Mwenyezi Mungu maneno ya kutangaza uovu ila kwa mwenye kudhulumiwa.”
Juz. 6 (4:148).

Na punde watajua waliodhulumu ni mgeuko gani watakaogeuka.

Huu ni ukemeo na kiaga cha mwisho mbaya kwa kila mwenye kudhlumu na kuonea.

Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote na rehema na amani zimshukie Muhammad na kizazi chake kitakatifu.