Table of Contents

Aya 23 – 37: Majibizano Baina Ya Musa Na Firauni

Maana

Akasema Firauni: Na ninani huyo Mola wa walimwengu wote?

Ewe Musa! Wewe unadai kuwa ni Mtume wa Mola wa walimwengu wote; hebu tubainishie jinsi yake na hakika yake huyo Mola?

Akasema: “Ni Mola wa mbingu na ardhi ikiwa nyinyi mna yakini.”

Musa alisema: Mwenyezi Mungu hajulikani isipokuwa kwa sifa zake na athari zake; zikiwa ni pamoja na huku kuumbwa ulimwengu huu wa ajabu katika mpangilio wake na nidhamu yake. Basi fikirini na mzingatie ikiwa mna akili zinazoweza kutambua kuwa nidhamu hii haiwezekani ila kwa uweza wa ujuzi na hekima.

Firauni akawaambia waliomzunguuka: Je, hamsikii?

Yaani mnasikia maajabu hayo. Hatujawahi kusikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.

Akasema: Ni Mola wenu na Mola wa baba zenu wa kwanza.

Musa alisema kwa kusisitiza kwamba Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa ulimwengu, muumba wenu na muumba wa baba zenu wa mwanzo na pia ndiye muumba wa huyu Firauni mnayemfanya mungu na kumwabudu.

Akasema: Hakika mtume wenu huyu mliyetumiwa ni mwenda waz- imu.

Musa ni mwendawazimu katika mantiki ya Firauni, kwa nini? Kwa sababu amesema Firauni si mungu bali ni kiumbe. Mantiki haya ya kifirauni anayo kila anayedai asichokuwa nacho. Yeyote anayedai kuwa na elimu naye ni mjinga, ikhlasi naye ni mhaini au ukweli naye ni mrongo, basi yeye yuko katika mila ya Firauni na desturi yake. Lau atapata wanaomwamini atasema: Mimi ndiye mola wenu au simjui mungu mwingine kwenu zaidi ya mimi; kama alivyosema Firauni.

Akasema: Ni Mola wa mashariki na magharibi na viliomo baina yake, ikiwa nyinyi mna akili.

Musa aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu. Akaashiria kuchomoza jua na kuchwa kwake, ambapo Firauni hawezi kujasiri kusema kuwa yeye ndiye anayelichomoza jua mashariki na kulipeleka magharibi.

Kwa hiyo alipigwa na butwaa aliposikia maneno haya kutoka kwa Musa; sawa na alivyopigwa na butwaa Namrud kabla yake, pale Ibrahim (a.s.) alipomnyamazisha kwa kusema:

فَإِنَّ اللَّهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ {258}

“Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi.”
Juz. 3 (2:258).

Firauni alipoishiwa, alikereka, akawa anatoa vitisho na akasema: Kama ukimfanya mungu mwingine asiyekuwa mimi basi bila shaka nitakufanya miongoni mwa wafungwa.

Jela na kutesa ndio silaha pekee ya utawala muovu wa mabavu dhidi ya haki uadilifu na uhuru, tangu zamani. Lakini jihadi ya wakombozi na ukakamavu wao, unaifanya silaha ya mataghuti ishindwe kwenye shingo zao na vifua vyao; kama ilivyoshindwa silaha ya Firauni.

Walisema wa kale: Mwenye kuchomoa upanga wa dhulma atauliwa nao.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

فَكُلًّا أَخَذْنَا بِذَنْبِهِ ۖ فَمِنْهُمْ مَنْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِ حَاصِبًا وَمِنْهُمْ مَنْ أَخَذَتْهُ الصَّيْحَةُ وَمِنْهُمْ مَنْ خَسَفْنَا بِهِ الْأَرْضَ {40}

“Kila mmoja tulimtesa kwa makosa yake. Kati yao wapo tuliowapelekea kimbunga cha changarawe, na kati yao wapo walionyakuliwa na ukelele na kati yao wapo ambao tuliwadidimiza katika ardhi.” (29:40).

Akasema: Ijapokuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?” Akasema: Kilete basi kama wewe ni katika wakweli.

Musa hakuogopa vitisho vya Firauni na akamwambia kwa kujiamini kuwa utanifanya mfungwa hata kama ni mwenye haki, kwa kukuletea dalili isiyo na shaka kwako na kwa mwingine?

Atajibu nini Firauni? Je, amwambie ndio nitakufunga hata kama ni mwenye haki? Hawezi kumwambia hivi, kwa sababu itakuwa ni kukubali ukweli kuwa Musa ni Mtume wa Mola wa viumbe wote na kwamba yeye ni mzushi katika madai yake ya uungu. Kwa hiyo ndio akalazimika kusema lete hiyo dalili kama wewe ni mkweli.

Akaitupa fimbo mara ikawa nyoka dhahiri. Na akautoa mkono wake. Mara ukawa mweupe kwa watazamao. Akasema kuwaambia wakuu waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi mjuzi. Anataka kuwatoa katika ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani? Wakasema: Mwache kidogo yeye na ndugu yake, na uwatume wakusanyao watu mijini. Wakuletee kila mchawi mkubwa, mjuzi.

Aya hizi sita zimetangulia katika Juz. 9 (7:107 - 112) zikifanana kiutaratibu, kimpangilio na hata herufi; isipokuwa katika mambo mawili:

Hapa imesemwa: ‘mchawi mkubwa’ na kule ikasemwa ‘mchawi’ hakuna tofauti katika maneno haya isipokuwa kutilia mkazo.

Hapa imesemwa: ‘Akasema kuwaambia wakuu waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi mjuzi,’ na kule imesemwa: ‘Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.’ Tofauti hapa ni kubwa kama inavyojionyesha.

Kwa sababu hapa aliyesema ni Firauni kuwaambia wakuu na kule wakuu ndio waliosema kumwambia Firauni. Sasa je, kuna wajihi gani wa kuunganisha baina ya Aya mbili hizi?

Jibu: Sikupata ishara yoyote ya hilo katika tafsiri nilizonazo, wala sijui sababu yake. Kwa vyovyote iwavyo, jibu ninaloliona ni kuwa Firauni ndiye aliyeanza kuwaambia jamaa zake kuwa huyu ni mchawi; kisha jamaa zake nao wakaanza kuambiana kuwa ni kweli Musa ni mchawi; kama ilivyo kwa wanaoongozwa, wanaigiza kiongozi wao na kutolea ushahidi kauli zake.

Hapo basi hakuna kupingana baina ya Aya mbili. Firauni aliwaambia jamaa zake nao wakamwambia yeye kwa kumwigiza.

فَجُمِعَ السَّحَرَةُ لِمِيقَاتِ يَوْمٍ مَعْلُومٍ {38}

Basi wakakusanywa wachawi wakati wa siku maalum.

وَقِيلَ لِلنَّاسِ هَلْ أَنْتُمْ مُجْتَمِعُونَ {39}

Na watu wakaambiwa: Je, mtakusanyika?

لَعَلَّنَا نَتَّبِعُ السَّحَرَةَ إِنْ كَانُوا هُمُ الْغَالِبِينَ {40}

Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakaoshinda.

فَلَمَّا جَاءَ السَّحَرَةُ قَالُوا لِفِرْعَوْنَ أَئِنَّ لَنَا لَأَجْرًا إِنْ كُنَّا نَحْنُ الْغَالِبِينَ {41}

Basi walipokuja wachawi wakamwambia Firauni: Je, tutapata ujira ikiwa tutashinda?

قَالَ نَعَمْ وَإِنَّكُمْ إِذًا لَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ {42}

Akasema: Ndio, hapo nanyi hakika mtakuwa miongoni mwa wanaokurubishwa.

قَالَ لَهُمْ مُوسَىٰ أَلْقُوا مَا أَنْتُمْ مُلْقُونَ {43}

Musa akawaambia: Tupeni mnavyotaka kutupa.

فَأَلْقَوْا حِبَالَهُمْ وَعِصِيَّهُمْ وَقَالُوا بِعِزَّةِ فِرْعَوْنَ إِنَّا لَنَحْنُ الْغَالِبُونَ {44}

Wakatupa kamba zao na fimbo zao na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi bila shaka ni wenye kushinda.

فَأَلْقَىٰ مُوسَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ تَلْقَفُ مَا يَأْفِكُونَ {45}

Musa akatupa fimbo yake, mara ikavimeza walivyovibuni.

فَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سَاجِدِينَ {46}

Wachawi wakapomoka kusujudu.

قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ الْعَالَمِينَ {47}

Wakasema: Tumemwamini Mola wa Walimwengu.

رَبِّ مُوسَىٰ وَهَارُونَ {48}

Mola wa Musa na Harun.

قَالَ آمَنْتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ ۖ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ فَلَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ۚ لَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ مِنْ خِلَافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ {49}

Akasema Firauni: Je, mmemwamini kabla sijawaruhusu. Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi, lakini punde mtajua. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu nyote.

قَالُوا لَا ضَيْرَ ۖ إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا مُنْقَلِبُونَ {50}

Wakasema: Haidhuru, hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu.

إِنَّا نَطْمَعُ أَنْ يَغْفِرَ لَنَا رَبُّنَا خَطَايَانَا أَنْ كُنَّا أَوَّلَ الْمُؤْمِنِينَ {51}

Hakika sisi tunatumai Mola wetu atughufirie makosa yetu kwa kuwa ndio wa kwanza kuamini.