read

Aya 27 – 35: Nenda Na Barua Yangu Hii

Maana

Akasema: Tutatazama, umesema kweli au uko katika waongo.

Hud-hud alimpa habari Suleiman kuhusu watu wa Sabai, akamwambia tutachunguza maneno yako tuone kama yana ukweli.

Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini.

Suleiman aliwaandikia barua watu wa Sabai akiwaita kwenye twaa yake na akampatia Hud-hud akamwamabia ifikishe hii kwa njia yoyote, kisha ujitenge nao sehmu ambayo utaweza kujua au kusikia wanasema nini na wanaafikiana nini, kisha urudi uniletee habari.

Akasema: Enyi waheshimiwa! Hakika imeletwa kwangu barua tukufu, imetoka kwa Suleiman, nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu, kwamba msinifanyie jeuri na fikeni kwangu mkiwa waislamu.

Hud-hud alichukua barua na akaitupa mahali kwenye kasri ya malkia kwa namna ambayo inaweza kuonekana bila ya kujulikana aliyeileta, kama linavyojulisha neno ’imeletwa.’ Kisha Hud-hud akajiweka kando kuchunguza harakati za watu na mazungumzo yao; sawa na mwandishi wa habari.

Malkia alipoiona na akajua kilichoandikwa, aliwakusanya mawaziri na washauri, akawaonyesha na akaisifu kwa utukufu, kwa sababu mwenye barua hiyo ni mwenye cheo kikubwa cha heshima.

Bismillah ilikuwa ni sehemu ya barua hiyo ambayo aliifupisha kwa kutoa mwito wa utiifu bila ya utangulizi wala kuzidisha maneno. Hii ndio desturi ya mitume katika barua zao kwenda kwa wafalme. Mtume (s.a.w.) alikuwa akifupiliza barua zake kwa wafalme kwa kusema: “Silimu utasalimika” baada ya bismillah na Alhamdu.

Akasema: Enyi waheshimiwa! Nipeni ushauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri lolote mpaka muhudhurie.

Nipeni ushauri, maana mimi sipitishi jambo mpaka nipate rai yenu. Hii inaashiria kuwa demokrasia ya serikali ina mizizi yake katika historia ya mbali; kisha ikakua hadi ilivyo hivi sasa.
Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali wa vita, na amri iko kwako, basi tazama nini unaamrisha.

Walisema hivi kwa njia ya kujishasha, kutangaza nguvu zao na kumwachia majukumu yote malkia hata kama uamuzi wake utakuwa na mwisho mbaya.

Akasema: Hakika wafalme wanapouingia mji wanauharibu na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge, na hivyo ndivyo watendavyo.

Mfasiri mmoja wa kisasa akifafanua Aya hii anasema: “Inajulikana kuwa ni tabia ya kimaumbile ya wafalme wanapoingia mji wanaeneza ufisadi na wanawaangusha viongozi na kuwafanya ni watu wa chini. Haya ndio mazowea yao wanayoyafanya.”

Ukweli ni kuwa ufisadi unaenea ardhini kwa kiasi cha nguvu za mfisadi, na unazidi kadiri nguvu zao zinavyozidi, wawe wafalme au si wafalme. Aya imewahusu kuwataja wafalme kwa sababu wao wanakuwa na nguvu zaidi kuliko wengine.

Uhakika wa mhalifu unajificha kwenye unyonge wake, na unajitokeza anapokuwa na guvu. Kwa hiyo ni makosa kuuweka uhakika wa mtu anapokuwa mnyonge.

Kuna badhi ya watu tunaowajua ambao walikuwa ni mashuhuri kwa takua wakati walipokuwa hohehahe, lakini mara tu walipopata madaraka wakaandamwa na tuhuma ambazo hazifutiki hata siku zikipita. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe hidaya sisi na wao.

Kwa hiyo inatubainikia kuwa sifa ya ufisadi haihusiki kwa wafalme tu wala si tabia yao ya kimaumbile, vinginevyo ingelikuwa ni muhali kupatikana uadilifu na utengeneo kwao. Isipokuwa hiyo ni tabia ya wahalifu wenye nguvu; ni sawa iwe nguvu ya mali, cheo, akili au utawala na, kidini au kidunia. Wala hakuna wa kumzuia mkosefu mwenye nguvu isipokuwa dini tu.

Imam Ali (a.s.) anasema: Mwenye uzowefu wa maisha na uelewa wa mambo anaweza akaona ujanja wa kukwepa amri ya Mwenyeezi Mungu akaachana nao; lakini asiyejilinda (na dini) anaitumia fursa hiyo (Nahjul balagha khutba 41).

Na mimi ninawapelekea zawadi ningoje watakayorudi nayo wajumbe.

Mawaziri na washauri walimwachia malkia amri ya vita au usalama. Kabla ya kuamua chochote aliona kwanza ampelekee Suleiman zawadi ya thamani kubwa, kisha aangalie, je, ataikubali au ataikataa. Akiikubali basi atakuwa anatafuta dunia sio dini. Kwa hiyo ataweza kumtengeneza kwa mali na kama ataikataa na kung’ang’ania kuwa tumwendee tukiwa wanyenyekevu, basi atakua ni katika wenye misingi ya risala na misimamo ya itikadi yao wakijitolea muhanga kwa kila hali. Watu wa namna hiyo haifai kuwapiga vita.

فَلَمَّا جَاءَ سُلَيْمَانَ قَالَ أَتُمِدُّونَنِ بِمَالٍ فَمَا آتَانِيَ اللَّهُ خَيْرٌ مِمَّا آتَاكُمْ بَلْ أَنْتُمْ بِهَدِيَّتِكُمْ تَفْرَحُونَ {36}

Alipokuja kwa Suleiman, alisema: Hivi nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyonipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyowapa nyinyi, lakini nyinyi mnaifurahia zawadi yenu.

ارْجِعْ إِلَيْهِمْ فَلَنَأْتِيَنَّهُمْ بِجُنُودٍ لَا قِبَلَ لَهُمْ بِهَا وَلَنُخْرِجَنَّهُمْ مِنْهَا أَذِلَّةً وَهُمْ صَاغِرُونَ {37}

Rejea kwao! Kwa yakini tutawajia na majeshi wasiyoweza kuyakabili na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.

قَالَ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَيُّكُمْ يَأْتِينِي بِعَرْشِهَا قَبْلَ أَنْ يَأْتُونِي مُسْلِمِينَ {38}

Akasema: Enyi wakuu wa baraza! Ni nani kati yenu atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri.

قَالَ عِفْرِيتٌ مِنَ الْجِنِّ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَنْ تَقُومَ مِنْ مَقَامِكَ ۖ وَإِنِّي عَلَيْهِ لَقَوِيٌّ أَمِينٌ {39}

Akasema afriti katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka mahala pako. Na mimi hakika nina nguvu, mwaminifu.

قَالَ الَّذِي عِنْدَهُ عِلْمٌ مِنَ الْكِتَابِ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَنْ يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ ۚ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرًّا عِنْدَهُ قَالَ هَٰذَا مِنْ فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ ۖ وَمَنْ شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ {40}

Akasema mwenye elimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, alisema: Haya ni katika fadhila za Mola wangu, ili anijaribu, nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru kwa hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake na mwenye kukufuru kwa hakika Mola wangu ni Mkwasi, Mkarimu.