Table of Contents

Aya 30 – 40: Wameifanya Qur’an Ni Mahame

Na Mtume alisema: Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’an ni mahame.

Yaani wameachana nayo na wakakataa kuiamini au kuipa mtazamo wa kutafuta haki ili kuwa na yakini nayo. Vigogo wa kikuraishi waliukadhibisha unabii wa Muhammad (s.a.w.) na yaliyosemwa na Qur’an kwa kuhofia uchumi wao na kupupia vyeo vyao.

Ndipo Mtume akapeleka mashtaka yake kwa Mola wake ambaye mambo yote yako mikononi mwake. Hivi ndivyo afanyavyo mwenye akili, hashtakii haja yake isipokuwa kwa yule ambaye hukumu ya mashtaka hayo iko mikononi mwake.

Ndio, inawezekana mtu kumshtakia rafiki yake atakayemliwaza na kumpa moyo. Imam Jafar Sadiq (a.s.) amesema: “Mwenye kumshtakia ndugu yake amemshitakia Mwenyezi Mungu, na mwenye kumshtakia mwingine atakuwa amemshtaki Mungu.” Anakusudia ndugu wa kiimani, na kwamba muuminii akimshtakia muuminii kama yeye humwombea Mungu ampe faraja na kumwamrisha awe na subira, kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutokata tamaa na rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini akimshitakia asiyekuwa muumini humshakizia au kumshauri kuepukana na Mungu.

Na hivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu.

Mkombozi anaweza akamwambia taghuti, ewe mkosefu, na kumlaumu kwa ufisadi, upotevu na kuvunja haki za binadamu na mengineyo, lakini taghuti ametulia tu, wala hajali. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:112).
Huko tumejibu swali la: Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye aliyewajaalia Manabii wawe na maadui, kama inavyoonyesha Aya, kwa nini basi awaadhibu kwa kuwafanyia uadui Mitume?

Na Mola wako anatosha kuwa mwenye kuongoza na mwenye kunusuru.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume (s.a.w.) yakiwa na ahadi kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kumsaidia Mtume wake kutokana na maadui zake; kama alivyomsadia kumuongoza kwenye haki na kuidhihirisha dini yake kuliko dini zote, wajapochukia washirikina.

Na walisema wale ambao wamekufuru: Mbona haikuteremshwa kwake Qur’an yote mara moja?

Qur’an ilishuka kwa vipindi kulingana na haja ya watu. Mwanzo wa kushuka kwake ulikuwa pale Mtume (s.a.w.) alipokuwa na miaka arubaini ya umri wake mtukufu. Ukaendelea wahyi kushuka polepole mpaka pale Mtume alipohama kwenda mahali pa hali ya juu akiwa na miaka 63.

Washirikina walijaribu kila mbinu kuwaepusha watu na Qur’an. Wakasema ni vigano vya watu wa kale, lakini hawakuendelea na mbinu hii, kwa sababu ilikuwa ikijipinga yenyewe. Wakatafuta propaganda nyingine, wakasema mbona Qur’an isiteremshwe mara moja, kwani Mungu anahitaji kufikiria, kama wafanyavyo watunzi?

Hata kama ingeliteremka mara moja wasingelikosa la kusema, kama kawaida ya wapinzani, kuwa mbona isingeliteremka kidogo kidogo ili tuweze kuifahamu, kuathirika nayo na kuizowea. Lakini ukweli hujitokeza, hata wakiupinga.

Ndivyo hivyo, ili tuuimarishe kwayo moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.

Yaani tumeiteremsha Qur’an kwa mpangilio wa moja baada ya nyingine, ili moyo wake uwe na nguvu ya kuuhifadhi, kufahamu maana yake na kudhibiti hukumu zake.

Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyo nzuri, wale watakaokusanywa kifudifudi kwenye Jahannam, hao watakuwa mahali pabaya na ndio wenye kupotea njia sana.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume (s.a.w.). Watakaoleta mfano na kufufuliwa kifudifudi ni washirikina. Makusudio ya mfano wowote ni kila wanalomtaaradhi nalo Mtume mtukufu.

Katika Aya ya 5, ya Sura hii kwenye Juzuu iliyopita, wanapinga kwa kusema kuwa ni ngano za watu wa kale, katika Aya ya 7, wanasema kwa nini anakula na kutembea sokoni, katika Aya 8, wanasema amerogwa, katika Aya ya 21, iliyo kwenye Juzuu hii, wanasema kwa nini hakuteremshiwa malaika au tumuone Mungu na katika Aya 32 wanasema kwa nini isiteremshwe mara moja.

Baada ya kuyabatilisha madai yao haya ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hapa anamwambia Mtume wake: Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyo bora’

Yaani washirikina watakujadili kwa batili na sisi tutakuunga mkono kwa haki iliyo wazi na hoja ambayo itavunja kauli zao na kufedhesha batili zao. Hiyo ni hapa duniani. Ama malipo yao huko akhera, ni kuwa mazabania watawavuta kwenye nyuso zao.

Ambaye atakuwa katika hali hii huyo ndiye muovu wa viumbe vya Mungu na mwenye makazi mabaya zaidi.

Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamuweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri. Tukawaambia nendeni kwa watu waliozikadhibisha Ishara zetu, basi tukawaangamiza kabisa.

Kisa cha Musa na Firauni kimekwishatangulia kwenye Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz.9 (7:103 – 145). Katika Juz. 16 (20:9), tumezungumzia sababu za kukaririka kisa cha Musa (a.s.).

Na watu wa Nuh walipowakadhibisha mitume, tuliwagharikisha na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia madhalimu adhabu chungu.

Pia kisa cha Nuh kimekwishapita mara kadhaa. Tazama Juz.12 (11:25 – 49).

Na kina Ad na Thamud na watu a Rass.

Rass ni jina la kisima na watu wake ni kaumu ya Shu’ayb. Imetangulia mifano katika Juz. 12 (11:50 – 61 na 84 – 95).

Na vizazi vingi vilivyokuwa baina yao.

Yaani, vile vile tuliangamiza kaumu nyingi zilizokuwa baina ya kina Ad na watu wa Rass, kwa sababu wao waliwakadhibisha manabii na mitume.

Na wote tuliwapigia mifano na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.

Tuliwaangamiza baada ya ubainifu, onyo, mawaidha ya visa na kupiga mifano, lakini wao waling’ang’ania ukafiri na upotevu. Ikawa malipo yao ni kuangamizwa.

Na kwa hakika wao walifika kwenye mji ulionyeshewa mvua mbaya, basi je hawakua wakiuona? Bali walikuwa hawatarajii kufufuliwa.

Makusudio ya mji hapa ni mji wa kaumu ya Lut kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَلُوطًا آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَتْ تَعْمَلُ الْخَبَائِثَ {74}

“Na Lut tukampa hukumu na elimu na tukamwokoa na ule mji uliokuwa ukifanya maovu.” Juz. 17 (21:74).

na pia kauli yake:

فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِنْ سِجِّيلٍ مَنْضُودٍ {82}

“Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini. Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana.” Juz. 12 (11:82).

Maana ni kuwa washirikina walipokuwa kwenye misafara yao wakipitia mji wa Lut na kuona athari ya maangamizi na kubomoka, walitakiwa wapate funzo na waamini utume wa Muhammad, lakini wakapinga na kuwa na inadi, kwa sababu hawana yakini na ufufuo, hisabu na malipo.

وَإِذَا رَأَوْكَ إِنْ يَتَّخِذُونَكَ إِلَّا هُزُوًا أَهَٰذَا الَّذِي بَعَثَ اللَّهُ رَسُولًا {41}

Na wanapokuona hawakufanyii ila kejeli tu, ati huyu ndiye Mwenyezi Mungu aliyemtuma kuwa mtume?

إِنْ كَادَ لَيُضِلُّنَا عَنْ آلِهَتِنَا لَوْلَا أَنْ صَبَرْنَا عَلَيْهَا ۚ وَسَوْفَ يَعْلَمُونَ حِينَ يَرَوْنَ الْعَذَابَ مَنْ أَضَلُّ سَبِيلًا {42}

Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza kwa miungu yetu, kama tusingelikazana juu yao. Na karibu watajua watakapoiona adhabu, ni nani aliyepotea njia.

أَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَٰهَهُ هَوَاهُ أَفَأَنْتَ تَكُونُ عَلَيْهِ وَكِيلًا {43}

Je, umemuona aliyeyafanya matamanio yake kuwa ndio Mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?

أَمْ تَحْسَبُ أَنَّ أَكْثَرَهُمْ يَسْمَعُونَ أَوْ يَعْقِلُونَ ۚ إِنْ هُمْ إِلَّا كَالْأَنْعَامِ ۖ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلًا {44}

Au unadhani kwamba wengi wao wanasikia na wanafahamu? Hao hawakuwa ila ni kama wanyama howa; bali wao wamepotea zaidi njia.