read

Aya 36 – 40: Kiti Cha Enzi Cha Bilqis

Maana

Alipokuja mjumbe kwa Suleiman, alisema: Hivi nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyonipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyowapa nyinyi, lakini nyinyi mnaifurahia zawadi yenu.

Ujumbe wa malkia ulifika kwa Suleiman ukiwa na zawadi ya thamani kubwa. Alipoiona alimwambia yule aliyekuja nayo kuwa mimi ninawaita kwa Mwenyezi Mungu na nyinyi mnanipa mali nami nina mali nyingi kama uonavyo; bali Mwenyezi Mungu amenineemesha kwa makubwa zaidi kuliko mali, ambayo ni: utume, elimu na kuutumia upepo majini na ndege. Hivi mnanikisia kuwa ni katika waabudu mali?

Kisa hiki kinatukumbusha makuraishi, wakati walipomtaka mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aachane na jambo lake hili, wakamwambia: “Ukiwa, kwa jambo hili, unataka mali basi sisi tutakukusanyia mali mpaka uwe ni tajiri zaidi kuliko sisi, na kama unataka ufalme tutakupa.“

Waliposhindwa naye wakakimbilia kwa ami yake Abu Talib ili amkinaishe mwana wa nduguye akubali mali, vinginevyo atapigwa vita. Mtume (s.a.w.) akasema maneno yake mashuhuru: “Wallah! Ewe Ami yangu! Lau wataliweka jua kuumeni kwangu na mwezi kushotoni kwangu kwamba niliache jambo hili sitaliacha mpaka alidhihirishe Mwenyezi Mungu au niangamie.”

Rejea kwao! Kwa yakini tutawajia na majeshi wasiyoweza kuyakabili na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.

Maneno haya anaambiwa kiongozi wa msafara uliokuja na zawadi. Maana yake ni rejea wewe na wenzako na hiyo mliyokuja nayo. Wambie watu wako kuwa mimi nitakuja na jeshi langu la watu majini na ndege ambalo hamtaliweza si nyinyi wala wengene.

Hud-hud alikuwa amemwambia walivyosema: ‘Hakika wafalme wanapouingia mji wanauharibu na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge.’ Kwa hiyo Suleiman akasisitiza kauli ya malkia kwa kusema: ‘Tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.’

Akasema: Enyi wakuu wa baraza! Ni nani kati yenu atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwishasalimu amri.

Msafara uliporeja kutoka kwa Suleiman na wakampa habari Malkia kwa waliyoyaona na kuyasikia, aliona hapana budi isipokuwa kusikiliza na kutii. Akaelekea kwa Suleiman pamoja na wapambe wake. Akakiacha kiti cha enzi kikilindwa na askari.

Suleiman alipojua kufika Bilqis alipendelea kumuonyesha miujiza ya kufahamisha utume wake na ukuu wake; na kwamba muujiza huo uwe ni kukichukua kiti chake ambacho ndicho kinachoonyesha enzi yake na umalkia wake. Ndipo akauliza wale waliokuwapo mbele yake, ni nani atakayeniletea?
Akasema afriti katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka mahala pako. Na mimi hakika nina nguvu, mwaminifu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimtiishia Suleiman upepo ukienda kwa amri yake. Bila shaka huu ni mujiza. Akamtiisha ndege wakifuata amri yake.

Nao pia ni muujiza. Vile vile Mwenyezi Mungu alimuhusisha na baadhi ya askari binadamu na majini, wakifanya maajabu kulingana na wakati wo. Walikuwa wakiandamana na jeshi la Suleiman, wakisaidiana kumshinda adui; kama wafanyavyo wataalamu wa kiufundi hivi sasa.

Hilo linaashiriwa na matakwa ya Suleiman kwao kuwaletea kiti cha enzi cha Bilqis katika muda mchache na hali anajua kuwa kiko masafa ya mbali sana. Mmoja wa majini akamwambia nitakuletea kikiwa salama, kama kilivyo ukiwa wewe umekaa hapa.

Lakini akasema mwenye elimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako.

Ikawa ushindi ni wa huyu ambapo, kwa uweza wa elimu alio nao, aliweza kukileta kiti wakati uliotakiwa.

Haya ndiyo yaliyofahamishwa na dhahiri ya Aya. Ama maswali ya kuwa ni nani huyo aliyekuwa na elimu ya kitabu? Je, alikuwa ni Malaika, Khidhr au mja mwema katika binadamu aliyeitwa Asif bin Barkhiya Na kwamba je yeye alikuwa akijua jina kuu la Mwenyezi Mungu au ni elimu gani hiyo aliyoitumia?

Maswali yote haya na mengineyo mengi, jibu lake liko kwa Mola wangu. Kwa sababu Aya haikuweka wazi hilo, wala hakuna Hadith sahih iliyothibiti.

Uwezekano wa karibu, tunaoweza kusema ni kuwa yeye hakuwa katika majini, kwa sababu alimzidi jini Afrit, kama ilivyoweka wazi Aya, kwamba yeye alikileta kiti kabla ya kupepesa jicho. Miujiza inayodhihiri kwa mitume, pia inadhihiri kwa wale ambao wamechaguliwa na mitume kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

La muhimu kujua, katika tukio hili, ni kwamba Bilqis aliyekuwa na madaraka makubwa na neema, alimnyenyekea Suleiman.

Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, alisema: Haya ni katika fad- hila za Mola wangu, ili anijaribu, nitashukuru au nitakufuru.

Makusudio ya kukufuru hapa ni kukufuru neema, sio kumkufuru Mwenyezi Mungu. Suleiman hawezi kuzikufuru neema za Mola wake, kwa sababu yeye ni maasum. Alisema haya kama utangulizi wa kusema:

Na mwenye kushukuru kwa hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake na mwenye kukufuru kwa hakika Mola wangu ni Mkwasi, Mkarimu.

Katika maana ya Aya hii ni ile isemayo:

إِنْ أَحْسَنْتُمْ أَحْسَنْتُمْ لِأَنْفُسِكُمْ ۖ وَإِنْ أَسَأْتُمْ فَلَهَا ۚ {7}

“Mkifanya uzuri mnajifanyia wenyewe na mkifanya ubaya mnajifanyia wenyewe.” Juz. 15 (17:7).

قَالَ نَكِّرُوا لَهَا عَرْشَهَا نَنْظُرْ أَتَهْتَدِي أَمْ تَكُونُ مِنَ الَّذِينَ لَا يَهْتَدُونَ {41}

Akasema: Kibadilini kiti chake cha enzi, tuone ataongoka au atakuwa miongoni mwa wasioongoka?

فَلَمَّا جَاءَتْ قِيلَ أَهَٰكَذَا عَرْشُكِ ۖ قَالَتْ كَأَنَّهُ هُوَ ۚ وَأُوتِينَا الْعِلْمَ مِنْ قَبْلِهَا وَكُنَّا مُسْلِمِينَ {42}

Basi alipofika akaambiwa: Je kiti chako cha enzi ni kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hicho. Nasi tulipewa ilimu kabla yake na tukawa waislamu.

وَصَدَّهَا مَا كَانَتْ تَعْبُدُ مِنْ دُونِ اللَّهِ ۖ إِنَّهَا كَانَتْ مِنْ قَوْمٍ كَافِرِينَ {43}

Na yale aliyokuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia. Hakika yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.

قِيلَ لَهَا ادْخُلِي الصَّرْحَ ۖ فَلَمَّا رَأَتْهُ حَسِبَتْهُ لُجَّةً وَكَشَفَتْ عَنْ سَاقَيْهَا ۚ قَالَ إِنَّهُ صَرْحٌ مُمَرَّدٌ مِنْ قَوَارِيرَ ۗ قَالَتْ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي وَأَسْلَمْتُ مَعَ سُلَيْمَانَ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ {44}

Akaambiwa liingie jumba. Alipoliona alidhani ni lindi la maji, akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. Akasema: Hakika limesakafiwa kwa vioo. Akasema: Mola wangu! Hakika nimedhulu- mu nafsi yangu na najisalimisha pamoja na Suleiman kwa Mola wa walimwengu.