Table of Contents

Aya 41 – 44: Ati Huyu Ndiye Mtume?

Maana

Baina Ya Isa Na Muhammad

Na wanapokuona hawakufanyii ila kejeli tu, ati huyu ndiye Mwenyezi Mungu aliyemtuma kuwa Mtume?

Kwa muda wa miaka 13, Mtume (s.a.w.) alikuwa akiwalingania watu wake kwenye imani ya Mungu mmoja, akiamrisha uadilifu na kukataza dhulma. Mbele yake mweusi na mweupe walikuwa sawa. Vile vile tajiri na fukara. Hakuna kuzidiana isipokuwa kwa takua.

Si ajabu kuwa hili liliwafanya vigogo wa kikuraishi kumpa dhiki Muhammad (s.a.w.) na kumkejeli kutokana na mwito wake huo. Mada ya usawa ndiyo waliyoitumia sana kumkejelia: Bilal, mtumwa fukara anawezaje kuwa sawa na Abu Jahl, mungwana na mwenye mali; tena ati awe bora zaidi yake kwa Mungu kwa vile ni mwenye takua! Ilikuwa ni ajabu hilo kwao.

Mtume (s.a.w.) alivumilia maudhi yao, akaendelea na mwito wake. Kwa sababu yale anayoyapigania yanamfanya asijali lolote. Hivi ndivyo anavyokuwa imara mtu adhimu kwa wapumbavu na washari walio wapotevu; anategemea kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye na kwamba kesho ni yake, kwa sababu batili itaisha tu hata kama muda utarefuka.

Mustafa Sadiq Rafi, analinganisha baina ya Isa (a.s.) alipokejeliwa na wana wa Israil na Muhammad (s.a.w.) alipokejeliwa na makuraish. Miongoni mwa aliyoyasema ni: “Walimkejeli Bwana Masih hapo zamani, akawaambia: Hakuna Mtume asiyetukuzwa isipokuwa mjini na nyumbani kwake. Hivi ndivyo alivyowajibu wale waliomdharau.

Lakini Mtume (s.a.w.) hakuwajibu waliomkejeli hata pale alipokuwa na nguvu za uarabuni kote. Alikuwa hasemi isipokuwa lile analolifanyia kazi. Kunyamaza kwake kulikuwa na maneno mengi katika falsafa ya utashi, uhuru na maendeleo. Na kwamba hapana budi kuweko na mageuzi ya watu.

Na mti uchipue na utoe majani mapya yatakayoendeleza maisha. Yeye hakuchukia wala hakusema kitu. Alikuwa kama mtengenezaji ambaye hachukii wala kukata tamaa kwa kosa la kifaa, bali hupeleka mkono wake kurekebisha.”

Ni juu yetu sisi waislamu katika somo hili kupata funzo la uthabiti, ukakamavu na kujitolea muhanga kwenye haki. Tusikate tamaa ya haki kuishinda batili hata kama watu wake ni wengi.

Kwa sababu miongoni mwao wamo waliodanganyika na uongo ambao utafichuka na kuyeyuka siku zikipita; kuna wale walioghafilika dhamiri zao na Mola wao, kisha watarejea na kutubia dhambi zao.

Vile vile haitakikani tumwamini kila anayedai ni mtetezi wa haki, kwa sababu wadanganyifu na wafanya biashara ya dini ni wengi.

Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza kwa miungu yetu, kama tusingelikazana juu yao.

Haya ni maneno ya makuraishi ambao walimdharau Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Wanasema haya kwa kujipinga wenyewe bila ya kujitambua. Wanakubali kuwa Muhammad alikurubia kuwatia shaka kwenye masanamu yao kutokana na dalili, hoja na miujiza iliyodhihiri mikononi mwake.

Vilevile walikubali kuwa akili zao walizisimamisha kwa hawa na matamaanio yao. “Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza kwa miungu yetu, kama tusingelikazana juu yao,” hiyo ni fedheha na kupingana na kejeli zao kwa Muhammad. Walimkejeli na wakati huo huo wanakubali kuwa ana nguvu ya hoja. Hivi ndivyo alivyo kila mbatilifu; maneno yake yanagongana bila ya kujitambua. Siri katika hilo ni kuwa haki inaelea haizami.

Na karibu watajua watakapoiona adhabu, ni nani aliyepotea njia.

Walisema kuwa Muhammad anakurubia kuwapoteza, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akawajibu kuwa kesho mtakapokabiliana na vituko vikubwa ndio mtajua kuwa nyinyi ndio mliopotea na mlio na hasara, sio Muhammad na waliomwamini.

Je, umemuona aliyeyafanya matamanio yake kuwa ndio Mungu wake?

Kila ambaye matamanio yake yanashinda dini yake, atakuwa ameyafanya ndio mungu wake, atake asitake. Anayekuwa hivyo, hakuna matumaini ya kuongoka kwake. Kwa sababu kila hoja kwake ni upuzi, kwa vile inapingana na matamanio na matakwa yake.

Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?

Utakayemtetea na ufisadi na upotevu wake? Achana naye hana kheri yoyote. Umekwisha muonya. Basi ni juu yetu hisabu yake.

Wamepotea Zaidi Kuliko Wanyama

Au unadhani kwamba wengi wao wanasikia na wanafahamu? Hao hawakuwa ila ni kama wanyama howa; bali wao wamepotea zaidi njia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema wengi wao, kwa sababu baadhi yao walipinga mwanzoni, kisha wakarejea, wakaelekea kwenye uongofu na wakaifuata. Mwenyezi Mungu akaondoa usikizi na akili kwa wale waliong’ang’ania upinzani, kwa sababu hawakunufaikia na usikizi wao wala akili zao. Kila ambalo halitumainiwi kupatikana ni sawa na kuwa haliko.

Mwenyezi Mungu, imetukuka hekima yake, amewafananisha na wanyama, kwa sababu wao hawakuzingatia dalili wala kuwaidhika na hekima na mazingatio; bali ni afadhali wanyama kuliko wao. Kwa sababu wanyama howa (wakufugwa) wanatekelza wajibu wao kulingana na maumbile yao; wanafuata amri na makatazo ya wachungaji wao; wanajua yanayowadhuru na kuayaacha na yanayowanufaisha wakayafanya.

Lakini wao wafisadi hawamfuati Muumba wao, hawaogopi adhabu yake wala hawatarajii thawabu zake. Zaidi ya hayo, wanyama hawamdhuru yoyote aliye jinsi yake na asiyekuwa jinsi yake; bali watu wananufaika nao kwa kuwapanda, maziwa na sufu zao. Ama wafisadi na wapotevu, wao ni balaa kwa jamii yao na ndio sababu ya majanga na chimbuko la kutoendelea.

Kwa hakika wasifu huu hauhusiki na yule anayemkufuru Mwenyezi Mungu au kumshirikisha tu. Kila anayeipinga haki pamoja na kuweko dalili na hoja, huyo atakuwa amepotea zaidi kuliko mnyama; ni sawa awe amepinga kwa kiburi na inadi au kwa uzembe na kupuuza dalili za haki na rejea zake.

أَلَمْ تَرَ إِلَىٰ رَبِّكَ كَيْفَ مَدَّ الظِّلَّ وَلَوْ شَاءَ لَجَعَلَهُ سَاكِنًا ثُمَّ جَعَلْنَا الشَّمْسَ عَلَيْهِ دَلِيلًا {45}

Je, umeona jinsi Mola wako alivyokitandaza kivuli? Na angelitaka angelikifanya kitulie. Kisha tukalifanya jua ni dalili yake.

ثُمَّ قَبَضْنَاهُ إِلَيْنَا قَبْضًا يَسِيرًا {46}

Kisha tukakivutia kwetu kidogo kidogo.

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ لِبَاسًا وَالنَّوْمَ سُبَاتًا وَجَعَلَ النَّهَارَ نُشُورًا {47}

Yeye ndiye aliyewafanyia usiku kuwa ni vazi na usingizi kuwa ni mapumziko na akaufanya mchana kuwa ni wa matawanyiko.

وَهُوَ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ ۚ وَأَنْزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً طَهُورًا {48}

Naye ndiye anayezituma pepo kuwa bishara kabla ya rehema yake na tunayateremsha kutoka mbinguni maji twahara.

لِنُحْيِيَ بِهِ بَلْدَةً مَيْتًا وَنُسْقِيَهُ مِمَّا خَلَقْنَا أَنْعَامًا وَأَنَاسِيَّ كَثِيرًا {49}

Ili kwayo tuihuishe nchi iliyokufa na tuwanyweshe miongoni mwa wanyama tuliowaumba na watu wengi.

وَلَقَدْ صَرَّفْنَاهُ بَيْنَهُمْ لِيَذَّكَّرُوا فَأَبَىٰ أَكْثَرُ النَّاسِ إِلَّا كُفُورًا {50}

Na hakika tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka, lakini watu wengi wamekataa ila kukufuru.

وَلَوْ شِئْنَا لَبَعَثْنَا فِي كُلِّ قَرْيَةٍ نَذِيرًا {51}

Na kama tungetaka tungepeleka katika kila mji muonyaji.

فَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَجَاهِدْهُمْ بِهِ جِهَادًا كَبِيرًا {52}

Basi usiwatii makafiri na pambana nao kwayo kwa jihadi kubwa.

وَهُوَ الَّذِي مَرَجَ الْبَحْرَيْنِ هَٰذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ وَهَٰذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ وَجَعَلَ بَيْنَهُمَا بَرْزَخًا وَحِجْرًا مَحْجُورًا {53}

Yeye ndiye aliyezichanganya bahari mbili , hii ni tamu mno na hii ni chumvi sana, na akaweka kinga kati yake na kizuizi kizuiacho.

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ مِنَ الْمَاءِ بَشَرًا فَجَعَلَهُ نَسَبًا وَصِهْرًا ۗ وَكَانَ رَبُّكَ قَدِيرًا {54}

Naye ndiye aliyemuumba mwanadamu kutokana na maji na akamjaalia kuwa na nasaba na ukwe. Na Mola wako ni mwenye uwezo.