read

Aya 41 – 44: Kibadilini Kiti Chake

Maana

Akasema: Kibadilini kiti chake cha enzi, tuone ataongoka au atakuwa miongoni mwa wasioongoka?”

Suleiman aliwaambia baadhi ya watu wake: “Badilisheni kitu katika kiti chake cha enzi, tuone atakitambua au hatakitambua.”

Basi alipofika akaambiwa: Je kiti chako cha enzi ni kama hiki?

Walikibadilisha kiti kisha wakamuuliza.

Akasema: Kama kwamba ndicho hicho.

Hakukanusha kwa sababu ya kufanana sana nacho, wala hakukubali kwa sababu alikiacha kwenye kasri yake kikiwa na ulinzi mkali. Hivi ndivyo walivyo wanasiasa na viongozi, wanachunga sana maneno yao na majibu yao.

Nasi tulipewa ilimu kabla yake na tukawa waislamu.

Haya ni maneno ya Suleiman na watu wake. Maana ni kuwa waliijua haki kabla ya Bilqis.

Na yale aliyokuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia. Hakika yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.

Yaani kilichomzuia Bilqis kuijua haki na imani ni ile shirki yake na kuabudu kwake jua badala ya Mwenyzi Mungu.

Akaambiwa liingie jumba. Alipoliona alidhani ni lindi la maji, akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. Akasema: “Hakika limesakafiwa kwa vioo.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Suleiman alikuwa na kasri lililosakafiwa kwa vioo na kwamba maji yalikuwa yakipita chini yake. Bilqis aliingia kwenye kasr, hakutambua kioo kutokana na usafi wake.

Akasema: Mola wangu! Hakika nimedhulumu nafsi yangu na najisalimisha pamoja na Suleiman kwa Mola wa walimwengu.
Alidhulumu nafsi yake kwa ukafiri, kisha akatubia, akasilimu na akaufanya vizuri uislmu wake.

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّهَ فَإِذَا هُمْ فَرِيقَانِ يَخْتَصِمُونَ {45}

Na hakika tuliwapelekea Thamud ndugu yao Swaleh; kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi mara yakawa makundi mawili yakihasimiana.

قَالَ يَا قَوْمِ لِمَ تَسْتَعْجِلُونَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ ۖ لَوْلَا تَسْتَغْفِرُونَ اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ {46}

Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnahimiza uovu kabla ya wema? Mbona hamuombi maghufira kwa Mwenyezi Mungu mpate kurehemiwa?

قَالُوا اطَّيَّرْنَا بِكَ وَبِمَنْ مَعَكَ ۚ قَالَ طَائِرُكُمْ عِنْدَ اللَّهِ ۖ بَلْ أَنْتُمْ قَوْمٌ تُفْتَنُونَ {47}

Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe. Akasema: Kisirani chenu kiko kwa Mwenyezi Mungu. Lakini nyinyi ni watu mnaojaribiwa.

وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ {48}

Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi wala hawafanyi la maslahi.

قَالُوا تَقَاسَمُوا بِاللَّهِ لَنُبَيِّتَنَّهُ وَأَهْلَهُ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ {49}

Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu, tutamshambulia usiku yeye na ahli zake, kisha tutamwambia walii wake: Sisi hatukushuhudia maangamizi ya watu wake, na sisi bila shaka tunasema kweli.

وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ {50}

Na wakapanga hila nasi tukapanga hila na wao hawatambui.

فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ مَكْرِهِمْ أَنَّا دَمَّرْنَاهُمْ وَقَوْمَهُمْ أَجْمَعِينَ {51}

Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa hila yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao na watu wao wote.

فَتِلْكَ بُيُوتُهُمْ خَاوِيَةً بِمَا ظَلَمُوا ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ {52}

Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyodhulumu. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaojua.

وَأَنْجَيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ {53}

Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa na takua.