read

Aya 45 –53: Swaleh

Maana

Na hakika tuliwapelekea Thamud ndugu yao Swaleh, kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:73) na Juz. 12 (11:61).

Basi mara wakawa makundi mawili wakihasimiana.

Kundi moja liliamini haki na kundi jingine likaikadhibisha, kwa sababu inagongana na manufaa yao. Na hii hasa ndio sababu ya kuhasimiana; vinginevyo wangelisema, mna dini yenu na sisi tuna dini yetu

Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnahimiza uovu kabla ya wema? Mbona hamuombi maghufira kwa Mwenyezi Mungu mpate kurehemiwa?

Makusudio ya uovu hapa ni adhabu; na wema ni rehema.

Swaleh aliwaonya na adhabu wakadhibishaji kama watang’ang’ania upotevu na inadi yao. Wakasema kwa dharau kuwa tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni mkweli; kama ilivyoelezwa katika Juz. 8 (7:77).

Lakini bado akawajibu kwa upole, kuwa kwa nini mnaharakisha nakama ya Mwenyezi Mungu na hali Yeye amewapa muda mrefu ili mrejee kutoka kwenye upotevu wenu? Basi heri yenu ni kutubia na kutaka rehema kutoka kwake kwani Yeye ni mkarimu mwingi wa maghufira na mwenye kurehemu.

Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe.

Bada ya Swaleh kuwalingania kwa Mola wao na wakapinga, walipatwa na maradhi na wakaanza kumwambia kuwa umetutia dege wewe na wale walio pamoja nawe.

Akasema: Kisirani chenu kiko kwa Mwenyezi Mungu.

Hakika balaa liliowashukia ni kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu ambaye kwake zinakomea sababu zote. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:131). Mtume (s.a.w.) alikuwa akipenda mdomo wa kheri, kwa sababu ndani yake mna kumtegemea Mwenyezi Mungu na alikuwa akichukia kisirani, kwa sababu ndani yake mna kutarajia balaa.

Kuna Hadith ise- mayo: “Ukiona kisirani endelea, ukiwa na hasadi usiifanye na ukidhania usitafute uhakika.” Yaani ukiona jambo lina kisirani endelea nalo, na ukiona kijicho basi kibakie moyoni tu usidhihirishe na ukiwa na dhana mbaya basi usitafute uhakika.

Lakini nyinyi ni watu mnaojaribiwa.

Manajribiwa kwa mazuri na mabaya, ili vifichuke vitendo vyenu ambavyo mtastahikia thawabu na adhabu.

Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi wala hawafanyi la maslahi.

Walikuwako wapenda anasa wakijifakharisha kwa watu kwa utajiri wao na wakiufanya ni nyenzo ya kuwakandamiza na kufanya ufisadi katika nchi; wakimzuia kila kiongozi mwenye kutaka kuleta maslahi ya watu na anayependa heri.

Na hakukuwa na nafuu yoyote, bali kila jambo lao lilikuwa ni baya. Haya ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Wala hawafanyi maslahi.’

Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu, tutamshambulia usiku yeye na ahli zake, kisha tutamwambia walii wake: Sisi hatukushuhudia maangamizi ya watu wake na sisi bila shaka tunasema kweli.

Waliosema hivyo ni wale watu tisa wakimkusudia Nabii Swaleh. Waliambiana kuwa waape kumshambulia Swaleh na watu wake usiku, kisha wawaambie ndugu zake kuwa wao sio waliomuua na wala hawamjui aliyemuua.

Na wakapanga hila nasi tukapanga hila na wao hawatambui.

Mipango ya wale tisa ni njama za kumshambulia Swaleh na watu wake usiku; na mipango ya Mwenyezi Mungu ni kuwawahi kuwaangamiza kabla ya kumfikia Swaleh bila ya wao kutambua. Tazama Juz. 3 (3: 54) kifungu “Mwenyezi Mungu ni mbora wa wapanga hila.”
Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa hila yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao na watu wao wote.

Walitaka kumwangamiza Swaleh, lakini Mwenyezi Mungu akawaangamiza wao. Katika hilo kuna mazingatio kwa kila mwenye kumpangia njama mwingine.

Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyodhulumu nafsi zao.

Mwenyezi Mungu aliwahadharisha akawapa muda, lakini wakang’ang’ania ufisadi na upotevu.

Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaojua.

Makusudio ya kujua hapa ni kule kunakokwenda pamoja na matendo na mazingatio. Ama kujua tu bila ya matendo basi ni afadhali ujinga. Kwa sababu kutaleta maangamizi na balaa.

Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa na takua.

Hii ni desturi ya Qur’an; inapowataja madhalimu na adhabu yao inafuatishia kuwataja wenye takua na thawabu zao. Makusudio ni kuhadharisha na kupendekeza.

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ وَأَنْتُمْ تُبْصِرُونَ {54}

Na Lut alipowaambia watu wake: Je mnafanya uchafu nanyi mnaona?

أَئِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ شَهْوَةً مِنْ دُونِ النِّسَاءِ ۚ بَلْ أَنْتُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ {55}

Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake! Bali nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.

فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَنْ قَالُوا أَخْرِجُوا آلَ لُوطٍ مِنْ قَرْيَتِكُمْ ۖ إِنَّهُمْ أُنَاسٌ يَتَطَهَّرُونَ {56}

Na halikuwa jibu la watu wake isipokuwa kusema: Watoeni mjini mwenu, maana hao ni watu wanaojitakasa.

فَأَنْجَيْنَاهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَاهَا مِنَ الْغَابِرِينَ {57}

Tukamwokoa yeye na ahli zake isipokuwa mkewe, alikuwa miongoni mwa waliobakia nyuma.

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ مَطَرًا ۖ فَسَاءَ مَطَرُ الْمُنْذَرِينَ {58}

Na tukawamiminia mvua, ni mbaya mno mvua hiyo ya wale walioonywa.