Table of Contents

Aya 45 – 54: Dhahiri Ya Maumbile

Maana

Mwenyezi Mungu (s.w.t.), katika Aya hizi, ametaja badhi ya neema alizozieneza kwa waja wake, ambazo zinafahamisha kuweko kwake na ukuu wake. Anatuzindua nazo Mungu Mtukufu ili tumwamini na tumwabudu kwa kumfanyia ikhlasi. Ufafanuzi ni kama ufuatavyo:-

Je, umeona jinsi Mola wako alivyokitandaza kivuli?

Makusudio ya kutaja kivuli, ni kukumbusha neema ya kivuli ambacho kinampatia mtu mapumziko na raha na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayekiweka na kukiondoa.

Na angelitaka angelikifanya kitulie.

Yaani angeliifanya ardhi ikatulia, na kwa kutulia ardhi ndio kingetulia kivuli na kuwa katika hali moja. Kwa sababu kivuli hakina uhuru, kinamfuata mwenye kivuli hicho, akitaharaki nacho hutaharaki na akitingishika nacho hutingishika.
Kisha tukalifanya jua ni dalili yake.

Lau si kuweko jua, ardhi isingelikuwa na kivuli. Kwa hiyo kupatikana kwa jua kunajulisha kupatikana kivuli; sawa na kuweko sababu kunakofahamisha kuweko kinachosababishwa.

Kisha tukakivutia kwetu kidogo kidogo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anakitandaza kidogo kidogo, kisha anakiondoa kidogo kidogo kulingana na harakati za ardhi.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amenasibisha kwake kivuli na kukitandaza na kukiondoa, pamoja na kuwa hilo linategemea ardhi moja kwa moja, kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu ndiye muathiri wa kwanza wa kupatikana kwake na dhahiri ya maumbile ni nyenzo tu.

Yeye ndiye aliyewafanyia usiku kuwa ni vazi.

Hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameusifu usiku kuwa ni vazi na katika Juz. 7 (6:96) ameusifu kuwa ni utulivu. Maana zote mbili zinakurubiana. Kwa sababu kivazi kinazuia macho na utulivu hauna sauti itakayofikia masikio.

Na usingizi kuwa ni mapumziko.

Neno subata liliofasiriwa mapumziko, lina maana ya kustarehe na kuacha kufanya kazi.

Na akaufanya mchana kuwa ni wa matawanyiko ya harakati na kufanya kazi. Tafsiri iliyo wazi zaidi ya Aya hii ni ile Aya isemayo: “Na katika rehema zake ni kuwafanyia usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake na ili mpate kushukuru.” (28:73).

Naye ndiye anayezituma pepo kuwa bishara kabla ya rehema yake na tunayateremsha kutoka mbinguni maji twahara.

Makusudio ya rehema zake hapa ni mvua. Maana ni kuwa upepo unaleta habari njema ya kushuka maji kutoka mbinguni, ambayo ni twahara na yanatwaharisha; kama wasemavyo mafaqihi.

Ili kwayo tuihuishe nchi iliyokufa na tuwanyweshe miongoni mwa wanyama tuliowaumba na watu wengi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwenye neno lililofasiriwa nchi ametumia ‘Balda’ na kwenye Juz. 8 (7:58) ametumia neno ‘Balad’ maneno yote hayo yana maana moja.

Na hakika tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka.

Inawezekana kuwa iliyosarifiwa ni Qur’an na maana yawe kama Juz. 15 (17:41): “Hakika tumekwishasarifu katika Qur’an hii ili wapate kukumbuka, lakini haiwazidishii isipokuwa kuwa mbali.”

Pia inawezekana iliyosarifiwa ni mvua. Maana yawe ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaipeleka mvua kutoka sehemu moja hadi nyingine, kwa vile kama ingelibakia sehemu moja tu ingeleta uharibifu, pia kama ingelikatika kabisa wangelikufa na kiu.

Kila mwenye akili inampasa afikirie vizuri hekima na neema hii, ili amshukuru, lakini watu wengi wamekataa ila kukufuru. Yaani kumkana Mungu na kukufuru neema zake.

Na kama tungetaka tungepeleka katika kila mji muonyaji.

Kabla ya kutumwa Muhammad (s.a.w.) Mwenyezi Mungu alituma Mtume kwa kila umma. Mwenyezi Mungu anasema:

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَسُولٌ ۖ {47}

“Na kila Umma una Mtume.” Juz. 11 (10:47).

Kuanzia zama za Muhammad (s.a.w.) mpaka siku ya mwisho, Mwenyezi Mungu amefunga kupeleka mitume kwa viumbe na akatosheka na Mtume mmoja kwa viumbe wote ambaye ni Muhammad bin Abdillah (s.a.w.). Dini yake ndiyo dini ya mwisho kwa watu wote.

Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akachukua ahadi kwa kila Mtume kumtolea habari Muhammad na sifa zake:

“Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi kwa manabii. Nikiwapa kitabu na hekima; kisha akawajia mtume msadikishaji wa yale yaliyo pamoja nanyi, ni juu yenu kumwamini na kumsaidia. Akasema: Je, mmekubali na mmechukua ahadi yangu kwa hayo? Wakasema: ‘Tumekubali.’ Akasema: basi shuhudieni, na mimi ni pamoja nanyi katika mashahidi.” Juz. 3 (3:81).

Hakuna aliye juu zaidi ya cheo hiki, isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na amemkumbusha mwenye cheo hiki kwa kumwambia: ‘Na kama tungetaka tungepeleka katika kila mji muonyaji.’ Lakini hatukufanya; tumekuwakilisha wewe uzionye umma zote kwa kukuadhimisha, kwa sababu taadhima ina kiwango chake na uzito wake.

Qur’an Na Idhaa

Basi usiwatii makafiri na pambana nao kwayo kwa jihadi kubwa.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Inafaa kukataza jambo, hata ikiwa inajulikana mwenye kukatazwa halifanyi kabisa; hasa ikiwa mkatazaji ni Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwayo ni kwa hiyo Qur’an.

Maana ni kuwa ewe Muhammad! Usiwaitikie makafiri kwa jambo lolote watakalokuitia; wala usiwache fursa yoyote ya kuitangaza Qur’an; uwasomee kwenye masikio yao, wapende wasipende. Na uvumilie maudhi yatakayokupata katika njia hii. Maudhi yao yasiwe ni kikwazo cha kui- tangaza; kwani kutangaza Aya za Mwenyezi Mungu ni jihadi kubwa katika njia ya haki na ya ubinadamu.

Lengo la msisitizo huu sio kuwanyamazisha wapinzani na mataghuti tu; isipokuwa ni kuwaamsha wanaokandamizwa na wasiofahamu na kuwaongoza kwenye uhuru wao ambao wameuchukua wenye nguvu; kwamba uadilifu na usawa ni haki ya kila mtu itokayo kwa Mungu; na kwamba hakuna mwenye nguvu wala tajiri au mtukufu isipokuwa kwa takua na amali njema.

Qur’an ndiyo inayodhamini haki hii. Hakuna dini wala sharia itakayoweza kutekeleza hilo ila ikiwa itasimamia uadilifu na usawa.

Hapa ndio tunajua siri iliyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنْصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ {204}

“Na isomwapo Qur’an isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemiwa.” Juz. 9 (7:204).

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha Mtume wake mtukufu kufanya juhudi kubwa ya kusoma Qur’an na kuitangaza, kwa sababu kwayo sauti ya haki na uadilifu itainuka na kuenea elimu na mwamko kwa watu. Hapo kila mtu atahisi heshima yake na kuilinda. Hapa inatubainikia kuwa kuisoma Qur’an katika idhaa zote za ulimwengu, sio kubainisha ufasaha kama wanavyodhani; isipokuwa umuhimu wa kwanza ni kuleta uadilifu na usawa kwa watu wote.

Yeye ndiye aliyezichanganya bahari mbili , hii ni tamu mno na hii ni chumvi sana, na akaweka kinga kati yake na kizuizi kizuiacho.
Makusudio ya bahari mbili katika Aya sio bahari mbili hasa; isipokuwa ni aina mbili za maji: moja ni tamu na nyingine ni chumvi. Neno bahari hutumiwa pia kwa maji mengi yawe chumvi au tamu.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameyajaalia maji ya chumvi kwenye ardhi iliyoinama (pwani) na akajaalia maji tamu kwenye ardhi iliyo juu ya maji-chumvi (bara); kwa namna ambayo maji-tamu ya bara, yanaminika kwenye maji-chumvi ya pwani na maji-tamu yanabaki na utamu wake na maji-chumvi yanabaki na chumvi yake. Kama ingelikuwa kinyume, pwani ikawa juu na bara ikawa chini na maji yachanganyike, basi maji yote yangelikuwa chumvi na watu kuwa na matatizo.

Haya yote hayakutokea kisadfa; bali ni kwa makadirio ya mwenye hekima mjuzi. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:’ na akaweka kati yake kinga na kizuizi kizuiacho’ ni kuwa aina mbili hizi za maji hata zikikutana hakuna moja inayozidi nyingine, bali kila moja inabakia na athari yake. Ametukuka ambaye ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo.

Naye ndiye aliyemuumba mwanadamu kutokana na maji na akam- jaalia kuwa na nasaba na ukwe.

Makusudio ya nasaba ni udugu wa kuzaliwa na ukwe ni udugu unaotokana na kuoana. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemumba mtu, ambaye ni kiumbe wa ajabu, kutokana na manii na akajaalia udugu na kuhurumiana baina yao. Tazama Juz. 18: (23:12-14).

Na Mola wako ni mwenye uwezo.

Miongoni mwa uweza wake ni kumfanya mke na mume kutokana na chembe moja.

وَيَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَنْفَعُهُمْ وَلَا يَضُرُّهُمْ ۗ وَكَانَ الْكَافِرُ عَلَىٰ رَبِّهِ ظَهِيرًا {55}

Na wanaabudu wasiowadhuru wala kuwanufaisha badala ya Mwenyezi Mungu. Na kafiri daima ni msaidizi wa mpinzani wa Mola wake.

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا مُبَشِّرًا وَنَذِيرًا {56}

Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na muonyaji.

قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِلَّا مَنْ شَاءَ أَنْ يَتَّخِذَ إِلَىٰ رَبِّهِ سَبِيلًا {57}

Sema: Siwaombi ujira juu yake, isipokuwa mwenye kutaka ashike njia iendayo kwa Mola wake.

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ وَسَبِّحْ بِحَمْدِهِ ۚ وَكَفَىٰ بِهِ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا {58}

Na mtegemee aliye hai ambaye hafi na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kuwa yeye ni mwenye habari za dhambi za waja wake.

الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ الرَّحْمَٰنُ فَاسْأَلْ بِهِ خَبِيرًا {59}

Ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akastawi juu ya Arshi. Mwingi wa rehema! Uliza habari zake kwa ajuaye.

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اسْجُدُوا لِلرَّحْمَٰنِ قَالُوا وَمَا الرَّحْمَٰنُ أَنَسْجُدُ لِمَا تَأْمُرُنَا وَزَادَهُمْ نُفُورًا ۩ {60}

Na wanapoambiwa msujudieni Mwingi wa rehema, wanasema: Ni nani huyo mwingi wa rehema? Je, tumsujudie unayetuamrisha wewe? Na huwazidishia chuki.

تَبَارَكَ الَّذِي جَعَلَ فِي السَّمَاءِ بُرُوجًا وَجَعَلَ فِيهَا سِرَاجًا وَقَمَرًا مُنِيرًا {61}

Amekuwa na baraka yule aliyejaalia katika mbingu buruji na akajaalia humo taa na mwezi wenye nuru.

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ خِلْفَةً لِمَنْ أَرَادَ أَنْ يَذَّكَّرَ أَوْ أَرَادَ شُكُورًا {62}

Naye ndiye ambaye ameujaalia usiku na mchana kufuatana, kwa yule anayetaka kukumbuka au anayetaka kushukuru.