Table of Contents

Aya 52 – 68: Kughariki Fairauni Na Watu Wake

Maana

Na tulimpelekea wahyi Musa kwamba nenda na waja wangu wakati wa usiku, kwa hakika mtafuatwa.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Musa atoke na wana wa Israil kutoka ardhi ya Misri usiku na akampa habari kwamba Firauni atawafuata ili awarudishe.

Basi Firauni akawatuma mjini wakusanyao.

Firauni alipojua kuwa Musa na watu wake wametoka aliwakusanyia watu ili awarudishe kwenye utawala wake na awape adhabu ya utoro.

Akasema: Hakika hawa ni kikundi kidogo nao wanatuudhi na sisi ni wengi wenye kuchukua hadhari.

Ni nani huyo Musa na watu wake. Wao si chochote kwetu; wanajaribu kutukasirisha na kutufanyia jeuri, na sisi tunawachunga. Basi watapata adhabu ya matendo yao. Lakini juu ya mipango ya Firauni kuna mipango ya Mwenyezi Mungu. Imam (a.s.) anasema: Mambo yanakuwa kwa makadirio ili maangamizi yawe kwa mpangilio.

Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem na mahazina na vyeo vya heshima.

Firauni na jeshi lake alitoka ili amwadhibu Musa na watu wake, lakini Mungu akawaadhibu wao na akawatoa katika yale waliyokuwa wakiyamilikii na kustarehe nayo; yakiwemo makasri ya ghorofa, mito inayotiririka, miti iliyojaa matunda kochokocho, mahazina yaliyojificha, mabembea, mabwawa ya kuogelea na sehemu za kupunga upepo. Yote haya na mengineyo waliyaacha bila ya kurudi.

Hivyo ndivyo! Na tukawarithisha wana wa Israil.

Tabari anasema: “Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwarithisha wana wa Israil majumba ya Firauni na watu wake.” Abu Hayyani Al-Andalusi naye amesema katika kitabu Al-bahrul-Muhit: “Haya ndio maana ya dhahiri, kwa sababu Aya ya kurithishwa wana wa Israil, imekuja moja kwa moja baada ya Aya ya kuwatoa.”

Wengine wamesema kuwa Mwenyezi Mungu aliwarithisha wana wa Israil mfano wa alivyokuwa Firauni na watu wake. Kwa sababu Waisrail hawakurudi Misri baada ya kuitoka.

Vyovyote iwavyo Aya inaeleza kuwa Mwenyezi Mungu hawaachi madhal- imu na dhulma yao na kwamba yeye anawaadhibu mikononi mwa wenye ikhlasi au kwa sababu yoyote. Haya ndiyo tunayoyaamini na kuyakubali. Ama uchunguzi wa historia na mfano wake tunawaachia wataalamu wake, ila ikiwa tuna yakini nayo.
Kisha wakawafuata walipotokewa na jua.

Firauni alitoka na jeshi lake la wapanda farasi na wendao kwa miguu kumtafuta Musa na watu wake wakawapata lilipochomoza jua.

Yalipoonana makundi mawili, kundi la Musa na la Firauni, watu wa Musa wakasema : Hakika tumepatikana.

Walisema hivyo kwa hofu na fazaa, kuwa adui amekwishatufikia hatuna la kufanya.

Akasema: Hapana! Hakika Mola wangu yuko pamoja nami, ataniongoza. Tulimpelekea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana na kila sehemu ikawa kama milima mkubwa.

Musa aliwaambia watu wake kuwa msimuogope Firauni na nguvu zake. Hakika Mwenyezi Mungu ana nguvu zaidi na yuko pamoja nami, nanyi mtaona.

Hakumaliza maneno yake, mara Mwenyezi Mungu akamwamrisha kupiga bahari kwa fimbo yake. Alipoipiga ikapasuka njia kumi na mbili kulingana na koo za waisrail. Maji yakainuka baina ya njia moja na nyingine kama mlima. Musa na watu wake wakavuka hadi ng’ambo ya pili.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:77).

Na tukawajongeza hapo wale wengine. Na tukamwokoa Musa na waliokuwa pamoja naye wote. Kisha tukawazamisha hao wengine.

Makusudio ya wengine ni kundi la Firauni. Maana ni kuwa baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwavusha wana wa Israil upande wa pili na wakawa wameokoka, kundi la Firauni nalo liliwasili. Wakaona muuujiza mkubwa – maji ya bahari yamesimama kama jabali na kutengeneza njia. Firauni akawaambia watu wake: Tazameni bahari ilivyoitikia matakwa yangu na kunifungulia njia ya kuwafuata walionitoroka.

Kisha wakajitoma na wakaenda kwa amani na utulivu. Hawakufika katikati, bahari ikawafunika wote, baada ya kuhadharishwa na kupewa muda mrefu, lakini walizama kwenye upotevu wao.

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara ya muujiza, mazingatio na mawaidha, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Wengi wao hapa wanakusudiwa wana wa Israil waliookolewa na Mwenyezi Mungu mikononi mwa Firauni, kwa kuchukilia dhahiri ya mfumo wa maneno ulivyo.

Na wala sio walioangamia, kama wasemavyo baadhi ya wafasiri. Dalili ya kuwa makusudio ni wana wa Israil ni kuwa wafuasi wa Firauni wote wlikuwa makafiri, bila ya kubaki; hasa wale aliokuwa nao. Na wana wa Israili, walipookolewa na Mungu kutoka kwa Firauni, walimwambia Musa: Tunataka sanamu tuliabudu badala ya Mwenyezi Mungu:

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتَوْا عَلَىٰ قَوْمٍ يَعْكُفُونَ عَلَىٰ أَصْنَامٍ لَهُمْ ۚ قَالُوا يَا مُوسَى اجْعَلْ لَنَا إِلَٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ ۚ {138}

“Na tukawavusha bahari wana wa Israil na wakawafikia waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakasema: Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu.” Juz. 9 (7:138).

Kwa hiyo maana yanakuwa kwamba Waisraili walishuhudia muujiza wa kupasuka bahari na miujiza mingineyo, lakini bado waliendelea kung’ang’ania ukafiri wao na jeuri yao.

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ إِبْرَاهِيمَ {69}

Na wasomee habari za Ibrahim.

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا تَعْبُدُونَ {70}

Alipomwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?

قَالُوا نَعْبُدُ أَصْنَامًا فَنَظَلُّ لَهَا عَاكِفِينَ {71}

Wakasema: Tunaabudu masanamu nasi tutaendelea kuyanyenyekea.

قَالَ هَلْ يَسْمَعُونَكُمْ إِذْ تَدْعُونَ {72}

Akasema: Je yanawasikia mnapoyaita?

أَوْ يَنْفَعُونَكُمْ أَوْ يَضُرُّونَ {73}

Au yanawafaa au yanawadhuru?

قَالُوا بَلْ وَجَدْنَا آبَاءَنَا كَذَٰلِكَ يَفْعَلُونَ {74}

Wakasema: Bali tumewakuta mababa zetu wakifanya hivyo hivyo.

قَالَ أَفَرَأَيْتُمْ مَا كُنْتُمْ تَعْبُدُونَ {75}

Akasema: Je, mmewaona mnaowaabudu?

أَنْتُمْ وَآبَاؤُكُمُ الْأَقْدَمُونَ {76}

Nyinyi na baba zenu wa zamani?

فَإِنَّهُمْ عَدُوٌّ لِي إِلَّا رَبَّ الْعَالَمِينَ {77}

Hakika hao ni maadui zangu isipokuwa Mola wa walimwengu wote.

الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ {78}

Ambaye ameniumba naye ananiongoza.

وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ {79}

Na ambaye ananilisha na kuninywesha.

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ {80}

Na ninapougua basi yeye ananiponya.

وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ {81}

Na ambaye atanifisha kisha atanihuisha.

وَالَّذِي أَطْمَعُ أَنْ يَغْفِرَ لِي خَطِيئَتِي يَوْمَ الدِّينِ {82}

Na ambaye ndiye ninayemtumai kunighufuria makosa yangu siku ya malipo.

رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ {83}

Mola wangu! Nitunukie hukumu na uniunganishe na wema.

وَاجْعَلْ لِي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الْآخِرِينَ {84}

Na unijaalie kutajwa kwa wema na wengine.

وَاجْعَلْنِي مِنْ وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ {85}

Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.

وَاغْفِرْ لِأَبِي إِنَّهُ كَانَ مِنَ الضَّالِّينَ {86}

Na umghufirie baba yangu, kwani alikuwa miongoni mwa wapotevu.

وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ {87}

Wala usinihizi siku watakapofufuliwa.

يَوْمَ لَا يَنْفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ {88}

Siku ambayo haitafaa mali wala wana.

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ {89}

Isipokuwa mwenye kuja kwa Mwenyezi Mungu na moyo uliosalimika.