read

Aya 54 – 58: Lut

Maana

Umetangulia mfano wa Aya 54 - 58 katika Juz. 8 (7:80 – 84). Wala hakuna tofauti isipokuwa katika baadhi ya ibara zifuatazo:

Kule Mwenyezi Mungu amesema: Je, mnafanya uchafu ambao hajawatangulia yeyote kwa hilo katika walimwengu? Na hapa anasema:

Je, mnafanya uchafu nanyi mnaona?

Maneno yote hayo ni ya kutahayariza. Kule amesema: “Bali nyinyi ni watu warukao mipaka” na hapa akasema:
Bali nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.

Ujinga pi ni katika aina ya kuruka mipaka. Kule amesema: “Na tukawamiminia mvua,basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa waovu.” Na hapa amesema:

Na tukawamiminia mvua, ni mbaya mno mvua hiyo ya wale walioonywa.

Mifano hii ni mingi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Anasimulia maneno ya mitume kwa matamshi mengine katika Aya ya pili na pia katika Aya ya tatu anasimulia kwa matamshi mengine. Hii inafahamisha kuwa mtu anaweza kunukuu maneno ya watu wengine neno kwa neno au kwa maneno mengine yenye maana sawa, lakini kwa sharti la kutopunguza au kuongeza chumvi.

قُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ وَسَلَامٌ عَلَىٰ عِبَادِهِ الَّذِينَ اصْطَفَىٰ ۗ آللَّهُ خَيْرٌ أَمَّا يُشْرِكُونَ {59}

Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (alhamdu-lillah) na amani ishuke juu ya waja wake aliowateua. Je Mwenyezi Mungu ni bora au wale wanaowashirikisha naye?