Table of Contents

Aya 55 – 62: Kafiri Ni Msadizi Wa Mpinzani Wa Mola Wake

Maana

Na wanaabudu wasiowadhuru wala kuwanufaisha badala ya Mwenyezi Mungu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 11 (10 18).

Na kafiri daima ni msaidizi wa mpinzani wa Mola wake.

Yaani anawasaidia watu wa batili dhidi ya haki. Kila mwenye kusaidia batili atakuwa amesaidia dhidi ya Mwenyezi Mungu na kuwa adui yake; hata kama atamsabihi na kumtukuza kwa ulimi wake. Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): “Mwenye kumsaidia dhalimu na huku anajua kuwa ni dhalimu basi amejitenga na Uislamu.”

Kadiri nitakavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka kuwa mwenye kumtegemea dhalimu ni kafiri; bali kafiri aliye mwadilifu ni bora kuliko yeye. Aya za Qur’an kuhusu hilo ni nyingi na ziko wazi. Ama Hadith za Mtume zimepituka kiwango cha mutawatir.

Ndio! Ni wajibu wetu kuamiliana naye muamala wa kiislamu kwa vile tu ametamka: Lailaha illallah Muhammadurrasulullah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.)

Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na muonyaji.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 15 (17:105).

Sema: Siwaombi ujira juu yake, isipokuwa mwenye kutaka ashike njia iendayo kwa Mola wake.

Mimi sina tamaa ya mali yenu wala siwauzii pepo. Ninalotaka ni kutengeneza tu. Anayetaka kufanya njia ya kumwendea Mola miongoni mwenu, basi malipo yake yako kwa Mungu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:90) na Juz.12 (11:88).

Na mtegemee aliye hai ambaye hafi na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kuwa yeye ni mwenye habari za dhambi za waja wake.
Ewe Muhammad! Toa bishara na onyo ukimtegemea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na ikhlasi naye katika kauli yako na vitendo vyako na ujitakashe na kumfanyia mfano na kila lile ambalo halifanani na utukufu na ukuu wake. Yeye anamjua zaidi aliyepotea njia, na atamhisabu na kumlipa.

Ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akastawi juu ya Arshi.

Makusudio ya kustawi ni kutawala. Lililo na nguvu ni kuwa makusudio ya siku ni mikupuo, kwa sababu hakuna siku kabla ya kupatikana ulimwengu na jua. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:54), Juz. 11 (103), na Juz. 12 (11:7).

Mwingi wa rehema! Uliza habari zake kwa ajuaye.

Habari yake, ni habari ya huko kuumbwa mbingu na ardhi, ambako kunafahamika kutokana na mfumo wa Aya. Hapa kuna maneno yaliyotan- gulizwa na ya kukadiriwa. Maana ni: Yeye ni Mwingi wa rehema, ulizia habari za kuumbwa mbingu na ardhi kwa yule ajuaye ambaye ni Mwenyezi Mungu.

Na wanapoambiwa msujudieni Mwingi wa rehema, wanasema: ‘Ni nani huyo mwingi wa rehema? Je, tumsujudie unayetuamrisha wewe?’ Na huwazidishia chuki.

Nabii (s.a.w.) akiwaambia washirikina: ‘Mwabuduni Mwingi wa rehema, wala msiabudu masanamu,’ wao husema kwa kujitia hamnazo, kwa madharau, ni nani huyo unayetuambia tumwabudu unayemuita Mwingi wa rehema? Unataka tukutii wewe na tuwaasi baba zetu katika yale waliyokuwa wakiyaabudu?’

Ujinga na upumbavu huu unatukumbusha ujinga wa vijana wetu wanapoambiwa swalini na mfunge, husema: “Bado kuna Swala katika karne hii ya ishirini? Jambo la kushangaza ni kuwa vijana hawa wanaimba uhuru wa bianadamu; kama kwamba uhuru ni uzandiki na utu ni kujitoa kwenye misimamo.

Hawajui kuwa aliye huru ni yule anayemwabudu Mwenyezi Mungu wala hamnyenyekei asiyekuwa yeye na kwamba utu ni dini ya Mwenyezi Mungu ambayo inakataza maovu na munkar.

Amekuwa na baraka yule aliyejaalia katika mbingu buruji na akajaalia humo taa na mwezi wenye nuru.

Makusudio ya buruji ni mashukio ya jua na mwezi. Tazama Juz.14 (15: 16). Makusudio ya taa hapa ni jua, kutokana na kuunganisha na mwezi. Mahali pengine Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا {5}

Yeye ndiye aliyefanya jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru.” Juz.11 (10:5).

Wengine wametofautisha baina ya nuru na mwanga. Kwamba mwanga unategemea sayari moja kwa moja; kama vile mwanga wa jua, unatoka kwenye jua moja kwa moja.

Nuru inategemea sayari kupitia sayari nyingine; kama vile nuru ya mwezi inavyotegmea jua. Wametoa dalili wanaotofautisha, kwa Aya hiyo ya Juz. 11 (10:5) tuliyoitaja punde.

Naye ndiye ambaye ameujaalia usiku na mchana kufuatana, kwa yule anayetaka kukumbuka au anayetaka kushukuru.

Usiku unaondoka kisha unakuja mchana, nao unaondoka kisha unarudi usiku na kuendelea; wala hakuna unaobakia muda mrefu kuzidi kiasi cha haja ya viumbe.

Kufuatana kwa namna hii kunafahamisha kuweko mpangiliaji mwenye hekima. Kufuatana huku kunategemea harakati za ardhi, nazo zinategemea msababishaji wake wa kwanza.

Ama hekima ya mfuatano huu, ni kwamba lau lingelibakia giza tu, au mwangaza tu, maisha yangelikuwa magumu hapa ardhini.

Kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ‘Kwa anayetaka kukumbuka,’ maana yake ni kuwa mwenye kutaka dalili ya kuweko Mwenyezi Mungu ataipata katika vitu vyote, vikiwemo kufuatana usiku na mchana.

Na kauli yake ‘Au anayetaka kushukuru,’ ni kuwa anayetaka kumshukuru Mweneyzi Mungu kwa neema yake naashukuru vile vile kwa kufuatana usiku na mchana, kwa sababu hilo ni katika neema kubwa.

وَعِبَادُ الرَّحْمَٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا {63}

Na waja wa Mwingi wa rehema ni wale wanaotembea ardhini kwa unyenyekevu. Na wajinga wakiwasemesha, husema: ‘Salama.’

وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا {64}

Na wale wanaokesha kwa ajili ya Mola wao kusujudu na kusimama.

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ ۖ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا {65}

Na wale wanaosema: ‘Mola wetu! Tuondolee adhabu ya Jahannam,hakika adhabu yake ni yenye kuendelea.

إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا {66}

Hakika hiyo ni mbaya kuwa kituo na mahali pa kukaa.

وَالَّذِينَ إِذَا أَنْفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامًا {67}

Na wale ambao wanapotumia hawafanyi israfu wala hawafanyi uchoyo wanakuwa katikati baina ya hayo.

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا {68}

Na wale ambao hawamwombi mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaiui nafsi aliyoiharamisha ila kwa haki, wala hawazini. Na mwenye kuyafanya hayo atapata madhambi.

يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا {69}

Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama na atadumu humo kwa kufedheheka.

إِلَّا مَنْ تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا {70}

Isipokuwa atakayetubia na akatenda matendo mema, basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

وَمَنْ تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّهِ مَتَابًا {71}

Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli.

وَالَّذِينَ لَا يَشْهَدُونَ الزُّورَ وَإِذَا مَرُّوا بِاللَّغْوِ مَرُّوا كِرَامًا {72}

Na wale ambao hawawi kwenye uzushi, na wanapopita kwenye upuzi hupita kwa heshima zao.

وَالَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ لَمْ يَخِرُّوا عَلَيْهَا صُمًّا وَعُمْيَانًا {73}

Na wale ambao wanapokumbushwa ishara za Mola wao hawajifanyi ni viziwi nazo na vipofu.

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا {74}

Na wale ambao wanasema: Mola wetu! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wenye takua.

أُولَٰئِكَ يُجْزَوْنَ الْغُرْفَةَ بِمَا صَبَرُوا وَيُلَقَّوْنَ فِيهَا تَحِيَّةً وَسَلَامًا {75}

Hao ndio watakolipwa ghorofa kwa walivyosubiri na watakuta humo maamkuzi na salaam.

خَالِدِينَ فِيهَا ۚ حَسُنَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا {76}

Watadumu humo kituo na makao mazuri.

قُلْ مَا يَعْبَأُ بِكُمْ رَبِّي لَوْلَا دُعَاؤُكُمْ ۖ فَقَدْ كَذَّبْتُمْ فَسَوْفَ يَكُونُ لِزَامًا {77}

Sema, Mola wangu asingewajali lau si kupewa kwenu mwito, lakini nyinyi mmewakadhibisha, basi (adhabu) ni lazima.