read

Aya 6 – 14: Musa

Maana

Na kwa hakika wewe unapewa Qur’an kutoka kwake Mwenye hekima, Mwenye ujuzi.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyekupa Qur’an na wala haitoki kwako, kama wanavyodai wapinzani.

Musa alipowaambia ahli zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda kuwaletea habari au kuwaletea kijinga kinachowaka ili mpate kuota.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:10).

Basi alipoufikia, pakanadiwa kwamba umebarikiwa uliomokatika moto huu na aliyeko pembezoni mwake na ametakasika Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.

Makusudio ya moto hapa ni nuru, uliomo ndani yake ni uweza wa Mwenyezi Mungu na aliyeko pembeni ni Musa.

Maana ni kuwa, ewe Musa! Kile ulichokiona ukadhania ni moto ni nuru iliyobarikiwa iliyoletwa na Mwenyezi Mungu kwa uweza wake na wewe uliyesimama pembeni mwa nuru hii pia umebarikiwa vilevile. Kwa sababu mimi nimekuchagua kwa risala yangu, upeleke bishara, kuonya na kueneza baraka ardhini. Hivi ndivyo tulivyoifahamu Aya baada ya kufuatilia na kutaamali. Ikiwa ndio makusudio ni sawa; ikiwa sivyo, lakini maelezo yenyewe ni sahihi.

Ewe Musa! Hakika mimi ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Alimfichulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwa anayemuita na kumwambia maneno ni Mola Mwenyezi, ili asikie na kutii.

Na itupe fimbo yako! Alipoiona inatingishika, kama kwamba ni nyoka, aligeuka kurudi nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usihofu! Hakika mimi hawagopi mbele yangu mitume.

Neno nyoka hapa limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu Jann lenye maana ya Jinn. Limefasiriwa kutokana na Aya nyingine zinazotaja nyoka moja kwa moja:

فَأَلْقَاهَا فَإِذَا هِيَ حَيَّةٌ تَسْعَىٰ {20}

“Akaitupa mara ikawa nyoka anayekwenda mbio.” Juz. 16 (20:20),

فَأَلْقَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ ثُعْبَانٌ مُبِينٌ {107}

“Akaitupa fimbo yake mara ikawa nyoka dhahiri.” Juz. 9 (7:107).

Musa ni mtu, na kawaida ya mtu ni lazima ahofie. Ni nani asiyeogopa atakapoiona kanzu yake iliyo mwilini imegeuka kuwa mnyama anayeshambulia, pete iliyomo kidoleni mwake imekuwa nge au fimbo iliyo mkononi mwake imegeuka nyoka?

Musa alihofia, kwa vile yeye ni mtu, anakula chakula, anatembea sokoni n.k. Lakini Mwenyezi Mungu alimpa amani na akamwambia kuwa wewe ni mjumbe wangu na wajumbe wangu wote wako katika amani na salama.

Ila aliyedhulumu kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi haki- ka mimi ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Mitume hawahofii, kwa sababu wao hawazidhulumu nafsi zao wala kuwadhulumu wengine; isipokuwa anayetakiwa kuwa na hofu ni yule aliyemdhulumu Mwenyezi Mungu kwa ushirikina na kufuru, kujidhulumu yeye mwenyewe kwa maasi au kuwadhulumu wengine kwa kuingilia haki zao.

Lakini aliyetubia baada ya dhulma yake basi Mwenyezi Mungu atam- takabalia toba na kumpa msamaha na rehema yake.

Na ingiza mkono wako katika mfuko wako utatoka mweupe pasipo ubaya.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7: 108), Juz. 16 (20:22) na Juzuu hii tuliyo nayo (26:33).

Ni katika ishara tisa kwa Firauni na watu wake. Hakika wao ni watu mafasiki.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:101).

Zilipowafikia ishara zetu zionyeshazo, walisema: Huu ni uchawi dhahiri.

Yaani zionyeshazo watu haki watakapoona hiyo miujiza tisa aliyokuja nayo Musa. Firauni na watu wake waliiona haki walipoona miujiza hii tisa, lakini walifanya kiburi na inadi, wakamkadhibisha Mwenyezi Mungu na wao wenyewe kwa kusema kuwa ni uchawi dhahiri. Ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema:
Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali yakuwa nafsi zao zina yakini nazo.

Nyoyo zao na akili zao zilikuwa na yakini na ukweli wa Musa na miujiza yake, lakini walimpinga kwa ndimi zao kuhofia manufaa yao na vyeo. Haya ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Kwa dhulma na kujivuna.’

Basi angalia ulikuwaje mwisho wa wafisadi katika ardhi kwa kufuru, dhulma na ufisadi?

وَلَقَدْ آتَيْنَا دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ عِلْمًا ۖ وَقَالَا الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي فَضَّلَنَا عَلَىٰ كَثِيرٍ مِنْ عِبَادِهِ الْمُؤْمِنِينَ {15}

Na hakika tulimpa Daud na Suleiman elimu na wakasema: Sifa njema zote (alham-du-lillah) ni za Mwenyezi Mungu ambaye ametufadhilisha kuliko wengi katika waja wake waumini.

وَوَرِثَ سُلَيْمَانُ دَاوُودَ ۖ وَقَالَ يَا أَيُّهَا النَّاسُ عُلِّمْنَا مَنْطِقَ الطَّيْرِ وَأُوتِينَا مِنْ كُلِّ شَيْءٍ ۖ إِنَّ هَٰذَا لَهُوَ الْفَضْلُ الْمُبِينُ {16}

Na Suleiman alimrithi Daud. Na akasema: “Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege. Na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhahiri.

وَحُشِرَ لِسُلَيْمَانَ جُنُودُهُ مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ وَالطَّيْرِ فَهُمْ يُوزَعُونَ {17}

Na alikusanyiwa Suleiman majeshi yake kutokana na majini na watu na ndege nayo yakapangwa kwa nidhamu.

حَتَّىٰ إِذَا أَتَوْا عَلَىٰ وَادِ النَّمْلِ قَالَتْ نَمْلَةٌ يَا أَيُّهَا النَّمْلُ ادْخُلُوا مَسَاكِنَكُمْ لَا يَحْطِمَنَّكُمْ سُلَيْمَانُ وَجُنُودُهُ وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ {18}

Hata walipofikia kwenye bonde la chungu, alisema chungu mmoja: Enyi chungu, ingieni maskani zenu, asije akawaponda Suleiman na jeshi lake na hali wao hawatambui.

فَتَبَسَّمَ ضَاحِكًا مِنْ قَوْلِهَا وَقَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَىٰ وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَدْخِلْنِي بِرَحْمَتِكَ فِي عِبَادِكَ الصَّالِحِينَ {19}

Basi akatabasamu akicheka kwa kauli yake, akasema: Ewe Mola wangu! Nizindue niishukuru neema yako uliyonineemesha na wazazi wangu na nipate kutenda mema unayoyaridhia na uni- ingize kwa rehema yako katika waja wako wema.