Table of Contents

Aya 63 – 77: Waja Wa Mwingi Wa Rehema

Maana

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja sifa za makafiri na kiaga chao, kama kawaida yake, anataja sifa za waumini na malipo aliyowaandalia. Zifuatazo ndizo sifa zao:

1. Na waja wa Mwingi wa rehema ni wale wanaotembea ardhini kwa unyenyekevu.

Imam Jafar Sadiq (a.s.) anasema katika tafsiri ya hilo: “Ni yule mtu anayetembea kwenye asili yake aliyoumbiwa, hajikalifishi wala hajifanyi.” Ndio, anayetembea kwenye umbile lake aliloumbiwa, tena akiwa peke yake bila ya kuwa na wapambe na wafuasi wanaomfuta nyuma na wengine mbele wakiwa wamepanda farasi au pikipiki na kupiga ving’ora vinavyohanikiza watu kwa sauti zake vikitangaza kuja kwake ili aachiwe njia, kwa ajili ya kumheshimu na kumtukuza.

2. Na wajinga wakiwasemesha, husema: ‘Salama.’

Makusudio ya kusemeshwa na wajinga ni kama vile kejeli zao, shutuma zao au mijadala ya hawa na masilahi. Amani ni kinaya cha kuachana nao, kwa kuwadharau na kuchunga mtu heshima yake. Maana ni kuwa, muumini akisikia neno ovu, aachane nalo; kama kwamba hakulisikia au kama anayekusudiwa ni mwingine sio yeye. Huu ndio mwepuko mwema aliousema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَاهْجُرْهُمْ هَجْرًا جَمِيلًا {10}

“Na uwaepuke mwepuko mwema.” (73:10).

Hakuna mwenye shaka kwamba kuachana na jambo ni pale ikiwa hakuna uwezo au nguvu za kulikabili. Vinginevyo itakuwa ni wajibu kulikabili. Hapana budi kuihusisha Aya na hilo.

3. Na wale wanaokesha kwa ajili ya Mola wao kusujudu na kusimama.

Waumini wanasimama usiku kwenye giza wakifanya ibada ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu hilo liko mbali na ria, wala hawaupitishi usiku mikahawani na kwenye mambo ya mchezo mchezo tu, huku wakifuja mali na kupanga njama dhidi ya waumini na wenye ikhlasi. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

كَانُوا قَلِيلًا مِنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ {17}

Walikuwa wakilala kidogo usiku.” (51:17).

4. Na wale wanaosema: ‘Mola wetu! Tuondolee adhabu ya Jahannam, hakika adhabu yake ni yenye kuendelea. haikwepeki na ni yakudumu. Hakika hiyo ni mbaya kuwa kituo na mahali pa kukaa,

Waliamini Pepo na Moto, kutokana na waliyoyashuhudia na kuyaona; ndio wakauhofia moto wakaitumai pepo. Imam Ali (a.s.) anasema: “Wao na Pepo ni kama walioiona wakiwa ndani yake wananeemeshwa. Na wao na moto ni kama waliouona wakiwa ndani yake wanaadhibiwa.”
5. Na wale ambao wanapotumia hawafanyi israfu wala hawafanyi uchoyo wanakuwa katikati baina ya hayo, hakuna kupitisha kiasi. Si ubakhili wala ubadhirifu.

Huu ndio mwenendo wa Uislamu, wastani katika kila kitu; hakuna ulahidi wala waungu wengi, udikteta wala ukiritimba na hakuna kutaifisha mali ya mtu wala ubepari. Tazama Juz. 15 (17:29) kifungu cha ‘Uislamu na nadharia ya maadili.’

6.Na wale ambao hawamwombi mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu.

Mwenye kufanya riya au akamtii kiumbe katika kumuasi Muumba, basi huyo ni kama aliyemwomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu.

Wala hawaiui nafsi aliyoiharamisha ila kwa haki.

Nafsi inayouliwa kwa haki na kwa uadilifu ni ile iliyoua nafsi nyingine bila ya haki, aliyezini akiwa kwenye ndoa, kurtadi dini au kuleta ufisadi katika ardhi.

Ufafanuzi wa hayo uko katika vitabu vya Fiqh.

Wala hawazini

Kwa sababu zinaa ni katika madhambi makubwa. Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Akaiweka sawa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuua nafsi na akajaalia hukumu ya haya matatu ni kuuliwa kwa masharti yaliyotajwa kwenye vitabu vya fiqh.

Na mwenye kuyafanya hayo atapata madhambi.

Hayo ni hayo ya shirk, kuua na kuzini. Na madhambi ni adhabu.

Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama na atadumu humo kwa kufedheheka.

Kuna adhabu gani kubwa na kufedheheka zaidi kuliko adhabu ya Jahannam? Si kwambii tena ikiwa itazidishwa pamoja na kudumu kusiko na mwisho.

Isipokuwa atakayetubia na akatenda matendo mema, basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe mwenye kurehemu.

Mwenye kutubia dhambi ni kama asiyekuwa na dhambi, zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu atampa thawabu kwa kule kutubia kwake na atampa mema kulingana na maovu ya dhambi zake; kiasi ambacho toba itafuta maovu ya dhambi.

إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ {114}

“Hakika mema huondoa maovu.” Juz. 12 (11:114).

Haya ndiyo maana ya ‘Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema’ kwa sababu uovu, kwa ulivyo, haustahiki kuwa wema, wala wema, kwa ulivyo, haustahiki kuwa uovu’

Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli.

Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Aya iliyotangulia kwamba mwenye kutubia atampa thawabu za mwenye kufanya mema, hapa anamsifu kuwa amerejea kwa Muumba wake kurejea kuzuri.

7. Na wale ambao hawawi kwenye uzushi, na wanapopita kwenye upuzi hupita kwa heshima zao.

Neno ‘hawawi’ limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu ‘laa yash-hadu- una’ kama ilivyotumika tafsiri hiyo katika Juz. 2 (2:185). Makusudio ya uzushi ni mambo ya batili na upuzi ni kila lisilo na kheri. Maana ni kuwa waumini hawahudhurii vikao vya ubatilifu wala hawavisaidii, sikwambii kuvifanya. Pia hawashiriki mazungumzo yasiyokuwa na kheri na wanapoyapitia hayo masiko yao huyaepuka; kama wanavyoziepusha ndimi zao kuayatamka; sawa na nyuki anavyopita haraka kwenye mzoga na harufu mbaya.

8. Na wale ambao wanapokumbushwa ishara za Mola wao hawaji- fanyi ni viziwi nazo na vipofu.

Mshairi huwa anasikiliza mashairi kwa umakini kabisa. Vile vile kila mwenye kuhusika na jambo akizungumziwa huwa anakuwa makini nalo sana anapolisikilza. Mtu unapomzungumzia jambo lililo mbali naye atakuepuka na hayo mazungumzo yako, hata kama ni ya uongofu na mwangaza.

Hapa ndipo inabainika siri ya muumini kuikubali Qur’an, na kafiri kuachana nayo. Mumin anakikubali Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa vile anakiamini na kutambua maana yake na makusudio yake. Anakikuta kwenye nafsi yake, itikadi yake, matendo yake mema na malipo aliyomuandalia Mola wake.

Kafiri anakipa mgongo Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa sababu anakipinga na hajui malengo yake na siri yake; wala hapati humo isipokuwa kushutumiwa na kukosolewa itikadi yake na sifa zake na pia makaripio ya ukafiri wake.

9. Na wale ambao wanasema: Mola wetu! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wenye takua.

Muovu huwa anatamaani watu wamfuate katika uovu wake, sio kwa kuwa amekinai kuwa yuko kwenye uongofu kutoka kwa Mola wake, hapana! Isipokuwa anataka kupunguza lawama na shutuma na kufunika kosa lake kwa kuwa wengi wakosefu. Lakini hataki mkewe na watoto wake wawe hivyo; kama vile mgonjwa asivyopenda watu wake wapatwe na ugonjwa alio nao.

Ama yule aliye mwema na mwenye takua ana yakini na dini yake na ana busara katika mambo yake. Kwa hivyo huwa anatamaani kwa dhati ya moyo kimsingi na kiitikadi kuwa watu wote wafuate njia yake na kwamba watoto wake wakimuiga yeye huwa anafurahi.

Kwa hiyo wenye ikhlasi humuomba Muumba wao wapate wa kuwaiga, sio kwa kuziba vitendo vyao kwa watu wala kutaka jaha duniani na kuchukua mali kwa kutumia haki za Mwenyezi Mungu; bali ni kwa kujipendekeza mbele ya Mwenyezi Mungu aliye peke yake.

Hao ndio watakaolipwa ghorofa kwa walivyosubiri na watakuta humo maamkuzi na salaam. Watadumu humo kituo na makao mazuri.

Ghorofa ni kinaya cha makao ya juu. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kubainisha wasifu wa wenye takua na watiifu, sasa anataja malipo yao watakayoyapata kwake, ambayo ni kudumu katika raha, amani na neema pamoja na heshima.

Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja subira hapa kuashiria kuwa kila mwenye haki hana budi kupata taabu na udhia kutoka kwa wasio na haki na kwamba thawabu za Mwenyezi Mungu hatazipata ispokuwa mwenye kuwa na uvumilivu na subira na akaendelea kuwa na msimamo kadiri hali itakavyokuwa ngumu.

Sema, Mola wangu asingewajali lau si kupewa kwenu mwito, lakini nyinyi mmewakadhibisha, basi (adhabu) ni lazima.

Makusudio ya neno ‘duakum’ hapa ni kupewa mwito kutokana na maneno yanayovutia, lakini mlikadhibisha. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَدَعَوْهُمْ فَلَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُمْ {52}

“Basi watawaita nao hawatawaitikia.” Juz. 15 (18:52)

Kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwapa mwito kwenye imani na utiifu kupitia kwa Mtume wake.

Maana ni kuwa nyinyi washirikina hamstahiki hata kutajwa pia lau si kuwa mliitwa kwenye imani na utiifu, ili kuweko na hoja siku ya hisabu na malipo, ikiwa hamtasikia na kuitikia mwito. Nanyi mmeupinga mwito na mkadhibishaji aliyetoa mwito huo, basi adhabu inawastahiki na ni lazima.