Table of Contents

Aya 69 – 89: Ibrahim

Maana

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekitaja kisa cha Ibrahim kwa kukigawa kulingana na mnasaba ulivyo.

Katika Aya hizi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amerudia majibizano baina ya Ibrahim na watu wake, kwa mfumo mwingine unaotofautiana na ule ulio katika Juz. 17 (21:51).

Na wasomee habari za Ibrahim.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) kuwa awasomee makuraishi ambao wanadai kuwa ni kizazi cha Ibrahim na wako kwenye dini yake.

Alipomwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?

Katika Juz.7 (6:74) tumetaja tofauti za wafasiri kuhusu baba aliyeambiwa maneno haya na Ibrahim, kuwa je, ni baba yake hasa au ni baba wa kimajazi au ni ami yake?

Wakasema: Tunaabudu masanamu nasi tutaendelea kuanyenyekea.

Tutadumu kuyaabudu na kuyatukuza. Kukubali kwao kuabudu masanamu kunajulisha kuwa neno sanamu halikuwa linamaanisha shutuma katika ufahamu wao, kama tunavyofahamu sisi; bali neno hilo lilikuwa likimaanisha utukufu na ukuu.

Akasema: Je yanawasikia mnapoyaita? Au yanawafaa au yanawadhuru?

Ni kawaida anayeabudiwa asikie, aone, adhuru na kunufaisha. Je, haya mnayoyaabudu yana sifa hizi? Swali hapa ni la kupinga.

Wakasema: Bali tumewakuta mababa zetu wakifanya hivyo hivyo.

Hii ni kukubali kuwa wao ni waigaji. Wala hilo si ajabu. Katika karne ya ishirini, zama za kutembea angani, tumeona wafuasi wakiwaiga viongozi wao na wakitoa dalili kwa kauli zao na kuzichukulia kuwa ni msingi, bila ya kuhakisha na kuchunguza.

Akasema: Je, mmewaona mnaowaabudu nyinyi na baba zenu wa zamani? Hakika hao ni maadui zangu isipokuwa Mola wa walimwengu wote.

Ikiwa nyinyi mnawaiga baba zenu, basi mimi simwigi yeyote na ninatangaza kujitenga kwangu na uadui wangu kwa hao waungu wenu; wala siabudu isipokuwa Mola wa walimwengu wote. Yeye ndiye walii wangu duniani na akhera. Yakiwa masanamu ni miungu, kama mnavyodai, basi na waniteremshie hasira zao, mimi napingana nao.

Ambaye ameniumba naye ananiongoza.

Mwenyezi Mungu amenipa akili nami naitumia kuniongoza kwenye haki. Ninaifuata na ninaitumia vizuri; wala simuigi yoyote; kama mnavyodai.

Na ambaye ananilisha na kuninywesha.

Kwa kuzifanya nyepesi sababu kwangu mimi na kwa viumbe vyake vyote.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameiumba ardhi hii na akaweka kila wanayoyahitajia na akasema: Yeye ndiye aliyeidhalisha ardhi kwa ajili yenu, basi tembeeni katika pande zake na kuleni katika riziki zake. Na kwake yeye ndio kufufuliwa.

Na ninapougua basi yeye ananiponya kutokana na madawa aliyoyaumba.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema, “Hakika kila ugonjwa una dawa, dawa ikifika kwenye ugonjwa hupona kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.” Kuna Hadithi nyingine isemayo: Hakika Mwenyezi Mungu ameteremsha ugonjwa na dawa, basi fanyeni dawa wala msifanye dawa kwa haramu.

Na ambaye atanifisha kisha atanihuisha na ambaye ndiye ninayemtumai kunighufuria makosa yangu siku ya malipo.

Uhai, mauti na maghufira yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu, hilo halina shaka. Na Ibrahim (a.s.) ni mwenye kuhifadhiwa na makosa na hatia (maasumu). Katika isma ya kila maasumu ni kuikuza hofu yake kwa Mwenyezi Mungu.

Mola wangu! Nitunukie hukumu.

Makusudio ya hukumu hapa, sio utawala bali ni hekima na kukata hukumu:

وَآتَيْنَاهُ الْحِكْمَةَ وَفَصْلَ الْخِطَابِ {20}

“Na tukampa hekima na kukata hukumu.” (38:20).

Na uniunganishe na wema.

Unipe tawfiki ya kufuata nyao zao na kutenda matendo yao.

Na unijaalie kutajwa kwa wema na wengine.

Makusudio ya wengine ni umma utakaokuja baadaye. Maana ni nijaalie kutajwa kwa wema baina ya watu baada yangu. Mwenyezi Mungu aliitikia dua yake; ambapo dini zote za mbinguni zimeafikiana kumtukuza na kumwadhimisha Nabii Ibrahim (a.s.).

Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.

Ni nani anayestahiki hizo zaidi kuliko Ibrahim.

Na umghufirie baba yangu, kwani alikuwa miongoni mwa wapotevu.

Angalia tafsiri ya “Na haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila ni kwa sababu ya ahadi aliyofanya naye, lakini ilipopambanukia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye.” Juz. 11 (9:114).

Wala usinihizi siku watakapofufuliwa.

Dua hii ni katika aina ya dua za mitume na viongozi wema. Siku ambayo haitafaa mali wala wana. Isipokuwa mwenye kuja kwa Mwenyezi Mungu na moyo uliosalimika.

Kutokana na maafa ya ukafiri, unafiki, mifundo, ria na maafa mengineyo na maradhi.

Moyo ukiwa salama na uchafu, basi viungo vyote huwa salama: ulimi utasalimika na uwongo, kusengenya, kusikiliza upuzi na ubatilifu. Vile vile mkono unasalimika na kufanya haramu na tupu kutokana na zina na uovu.

وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ {90}

Na Bustani (Pepo) itasogezwa kwa wenye takua.

وَبُرِّزَتِ الْجَحِيمُ لِلْغَاوِينَ {91}

Na Jahannam itadhihirishwa kwa wapotofu.

وَقِيلَ لَهُمْ أَيْنَ مَا كُنْتُمْ تَعْبُدُونَ {92}

Na wataambiwa, wako wapi mliokuwa mkiwaabudu.

مِنْ دُونِ اللَّهِ هَلْ يَنْصُرُونَكُمْ أَوْ يَنْتَصِرُونَ {93}

Badala ya Mwenyezi Mungu? Je, watawasaidia au kujisaidia wenyewe?

فَكُبْكِبُوا فِيهَا هُمْ وَالْغَاوُونَ {94}

Basi watavurumizwa humo wao na wapotofu.

وَجُنُودُ إِبْلِيسَ أَجْمَعُونَ {95}

Na majeshi ya Ibilisi yote.

قَالُوا وَهُمْ فِيهَا يَخْتَصِمُونَ {96}

Watasema na hali ya kuwa wanazozana humo:

تَاللَّهِ إِنْ كُنَّا لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {97}

Wallah! Hakika tulikuwa katika upotevu ulio wazi.

إِذْ نُسَوِّيكُمْ بِرَبِّ الْعَالَمِينَ {98}

Tulipowafanya sawa na Mola wa walimwengu wote.

وَمَا أَضَلَّنَا إِلَّا الْمُجْرِمُونَ {99}

Na hawakutupoteza ila wakosefu.

فَمَا لَنَا مِنْ شَافِعِينَ {100}

Basi hatuna waombezi.

وَلَا صَدِيقٍ حَمِيمٍ {101}

Wala rafiki wa dhati.

فَلَوْ أَنَّ لَنَا كَرَّةً فَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ {102}

Laiti tungepata kurejea tena tungelikuwa katika waumi- ni.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً ۖ وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُمْ مُؤْمِنِينَ {103}

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ {104}

Na hakika Mola wako ndiye mwenye nguvu mwenye kurehemu.