read

Aya 1-4: Kujitoa

Maana

Mwaka wa nane wa Hijra Mtume (saw) aliiteka Makka, mwaka wa tisa ilishuka Sura hii, katika mwaka wa kumi Mtume alihiji hija ya mwisho, na katika mwaka wa kumi na moja akafariki. Kwa hiyo Sura hii siyo ya mwisho kushuka, lakini ni katika Sura za mwisho mwisho. Hivoyo imekusanya hukumu za mwisho za uhusiano wa waislamu na washirikina. Twaha Hussein anasema katika kitab Mir-atul-Islam.

“Waarabu walizidi kuukubali Uislamu baada ya Hijja aliyohiji Abu Bakr mwaka wa tisa. Katika Hijja hii alimtuma Ali amuwahi Abu Bakr na awasomee watu Qur’an. Ikawa ni upambanuzi wa zama mbili: Zama ambazo Uislamu ulikuwa unapata nguvu kidogo kidogo, huku ushirikina ukiwa umebaki katika baadhi ya makabila ya Kiarabu. Na zama ambazo bara ya Arabu yote ilikuwa na Uislamu.

Qur’an yenyewe - ambayo Ali aliwasomea watu na kutenganisha baina ya zama hizo mbili - ni Aya hizi tukufu za Sura ya baraa, akatangaza kujitoa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na washirikina, akawaharamisha, katika tangazo hilo, washirikina wasikurubie Ka’aba au kuipitia au kutufu uchi’.

(Tangazo la) Kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina.

Tumetangulia kueleza kuwa Sura hii ilishuka mwaka uliofuatia kutekwa Makka ambapo Uislamu ulikuwa na kuenea bara Arabu yote, lakini pamoja na hayo ushirikina ulikuwa umebakia vifuani mwa baadhi ya makabila ya Kiarabu ili vifua hivyo visiwe kikosi cha tano1 katika jamii ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake katika Sura hii kutangaza kujitoa katika dhima na washirikina.

Kwa ufasaha zaidi kumpa onyo la vita kila mshirikina anayekaa bara Arabu mpaka aseme: Lailaha Illa Llah na aingie waliyoingia wenzake.

Onyo hilo liliwahusu washirikina wote, hata wale waliowekeana mkataba wa amani na Mtume; isipokuwa katika hali moja tu ambayo Mwenyezi Mungu ameiashiria kwa kusema:

Ispokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha wasiwapunguzie chochote.

Tafsir yake inafuatia.

Basi tembeeni katika nchi miezi minne; na jueni kwamba nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwadhalilisha makafiri.

Yaani semeni. Enyi waislamu kuwaambia washirikina: Tembeeni katika nchi kwa usalama katika muda huu. Baada ya Mwenyezi Mungu (swt) kuwatangazia vita washirikina, aliwapa muda wa miezi minne wahame kwa amani waende watakako bila ya kuguswa na yeyote.

Wakisilimu baada ya hapo basi wamesalimika na kufuzu duniani na akhera. Wakiendelea na ushirikina basi malipo yao ni kuuawa katika dunia na adhabu kali katika Akhera na hawataweza kuheba hayo.

Utauliza: kupigana na washirikina mpaka watamke shahada, hakuafikiani na kauli ya Mwenyezi Mungu:

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ {256}

“Hakuna kulazimishwa katika dini” Juz.3. (2:256)

Pia hakuafikiana na kauli ya Mwenyezi Mungu:

أَفَأَنْتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ {99}

“Je, wewe utawalazimisha watu wawe waumini?” (10:99)

Na Uislamu ni dini ya usalama si dini ya vita?

Jibu ni kweli kuwa Uislamu hamlazimishi yeyote kutamka: Lailaha Illa Llah; isipokuwa unalingania kwa hekima, na dalili. Mwenyezi Mungu anasema:

وَقُلِ الْحَقُّ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ فَمَنْ شَاءَ فَلْيُؤْمِنْ وَمَنْ شَاءَ فَلْيَكْفُرْ ۚ {29}

“Na sema haki inatoka kwa Mola wenu basi atakaye aamini na atakaye akufuru” (18:29).

Lakini hutokea, katika hali maalum, haja ya kutokuwepo washirikina kwa sababu wao wanaeneza ufisadi katika ardhi. Katika hali hii inajuzu kwa kuwalazimisha washirikina watamke kalima ya shahada. Na, washirikina wa bara Arabu wakati huo walikuwa ni kikosi cha tano katika jamii ya kiislamu mpya.

Kwa ajili hiyo ndipo ikawa hukumu kwao ni kuuawa au kudhihirisha Uislamu na wawe na walionayo Waislamu. Kwa maneno mengine ni kwamba hukumu hiyo ilikuwa ni maalum kwa washirikina wa bara Arabu wakati huo tu. yametangulia maelezo kuhusu hayo katika Juz.3 (2:256)

Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa watu siku ya Hijja kubwa ya kwamba Mwenyezi Mungu amejitoa na washirikina na pia Mtume wake. Basi kama mkitubu ndiyo heri kwenu, na kama mkikengeuka, basi jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu na wabashirie waliokufuru adhabu iumizayo.

Siku ya Hijja kubwa ni ile siku ya kuchinja (siku ya kumi ya Dhul-Hijja). Miezi minne ilianzia hapo, mnamo mwaka wa tisa wa Hijra na kumalizikia siku ya kumi, Rabiul-Akhar, mwaka wa kumi Hijra. Baada ya muda huo ndipo ikawa sasa washirikina wa bara Arabu wachague mawili. Kusilimu au kupigwa, kwa sababu ilikuwako haja ya kufanya hivyo kama tulivyoashiria.

Wafasiri, akiwemo Tabari, Razi na Abu Hayan Al-Andalusi, wamesema kwamba: iliposhuka Sura Tawba Mtume (saw) alimwamrisha Ali awaendee watu kwenye msimu wa Hijja awasomee. Akaambiwa: kwa nini usimpe Abu Bakr, akasema: Hanitekelezei ila mtu anayetokana na mimi. Ali akasimama kwenye Jamratul-Aqaba siku ya kuchinja na kusema: “Enyi watu! Mimi ni mjumbe wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu.” Akawasomea Aya hizo.

Ispokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha hawakuwapunguzia chochote wala hawakumsaidia yeyote juu yenu, basi watimizieni ahadi yao mpaka muda wao.

Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamrisha Mtume wake (saw) kuwapa muda wa miezi minne washirikina; hata wale ambao walivunja ahadi na waislamu, aliwatoa katika washirikina wale waliokuwa na mkataba wa amani na waislamu na hawakuvunja mkataba huo.

Aliwatoa hawa na kuwapa muda wa miezi minne tu, bali aliwapa muda wao kadiri watakavyokuwa wanatekeleza mkataba wao. Wafasiri wengi wanasema kuwa washirikina hao waliotekeleza mkataba ni watu wa Kinana, na muda wao ulikuwa umebakia miezi tisa. Ndipo mtume akawatimizia muda wao.
Aya hii inafahamisha kwamba si wajibu kutekeleza mkataba ila ikiwa upande wa pili nao unatekeleza. Ukiharibu kipengele chochote, basi huhis- abiwa uhaini na uvunjaji ahadi. Wala hapana ahadi kwa anayevunja ahadi.

Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua ambao wanaogopa kuvunja ahadi na ufisadi mwengineo.

فَإِذَا انْسَلَخَ الْأَشْهُرُ الْحُرُمُ فَاقْتُلُوا الْمُشْرِكِينَ حَيْثُ وَجَدْتُمُوهُمْ وَخُذُوهُمْ وَاحْصُرُوهُمْ وَاقْعُدُوا لَهُمْ كُلَّ مَرْصَدٍ ۚ فَإِنْ تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَخَلُّوا سَبِيلَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {5}

Ikisha miezi mitukufu, basi waueni washirikina popote mtakapowakuta, na wakamateni na muwazingire na wakalieni katika kila njia. Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu

وَإِنْ أَحَدٌ مِنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَا يَعْلَمُونَ {6}

Na kama yeyote katika washirikina akikutaka hifadhi, basi mhifadhi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha mfikishe mahali pake pa amani. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua.

كَيْفَ يَكُونُ لِلْمُشْرِكِينَ عَهْدٌ عِنْدَ اللَّهِ وَعِنْدَ رَسُولِهِ إِلَّا الَّذِينَ عَاهَدْتُمْ عِنْدَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ ۖ فَمَا اسْتَقَامُوا لَكُمْ فَاسْتَقِيمُوا لَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ {7}

Itakuwaje ahadi kwa washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake. Isipokuwa wale mlioahidiana kwenye msikiti mtakatifu. Basi maadamu wanakwenda na nyinyi sawa nanyi nendeni nao sawa. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua.

كَيْفَ وَإِنْ يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ لَا يَرْقُبُوا فِيكُمْ إِلًّا وَلَا ذِمَّةً ۚ يُرْضُونَكُمْ بِأَفْوَاهِهِمْ وَتَأْبَىٰ قُلُوبُهُمْ وَأَكْثَرُهُمْ فَاسِقُونَ {8}

Itakuwaje! nao wakiwashinda hawaangalii kwenu ujirani wala ahadi. Wanawafurahisha kwa midomo yao tu, hali nyoyo zao zinakataa. Na wengi wao ni mafasiki.
  • 1. Kikosi cha tano (fifth column) ni jina linalotumiwa kwa wale wanaofanya ujasusi wakijifanya ni miongoni mwao. Jina hili lilianza kutumiwa katika vita ya Uhispania mnamo mwaka 1936. Emilio Mola, kiongozi aliyekuwa chini ya Franco, alisema: "Nina vikosi vine dhidi ya Madrid kuongeza cha tano kitakachotokea kwao wenyewe." Mwandishi amelitu- mia neno hili hapa, kama lugha ya kufananisha -Mtarjumu