read

Aya 19-22: Kuwanywesha Mahujaji

Maana

Je, mnafanya kuwanywesha mahujaji na kuamirisha msikiti mtukufu ni sawa na yule aliyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na akapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu?

Makusudio ya kunywesha mahujaji ni kuwapa watu maji ya kunywa katika Hijja na kuamirisha msikiti hapa ni kuuhudumia.

Tafsir nyingi, ikiwemo tafsir ya Tabari, Razi, Naisaburi na Suyuti, imeelezwa kuwa Abbas bin Abdul Muttalib alikuwa akiwanywesha maji watu katika Hijja, na Twalha bin Shayba kutoka ukoo wa Abduddar alikuwa na funguo za Al-Kaaba. Twalha akasema mimi ndio mwenye Al-Kaaba, nina funguo zake. Abbas naye akasema mimi ndio mwenye kunywesha, Ali Bin Abutalib akasema.
Sijui mnasema nini. Mimi nimeswali kibla miezi sita kabla ya watu wengine na mimi ni mwenye jihadi ndipo, Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hiyo.

Kwa hiyo Ali ndio makusudio ya ‘ yule aliyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na akafanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu’

Hiki ndicho kipimo cha ubora mbele ya Mwenyezi Mungu - imani na kupigana jihadi katika njia yake. Ama wadhifa na vyeo mara nyingi humwongoza mtu kwenye ufisadi na maangamizi.

Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu katika malipo na thawabu.

Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

Baada ya kuwalingania kwenye uongofu na kukataa kwa chaguo lao ovu.

Wale walioamini na wakahama na wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa mali zao na nafsi zao, wana cheo kikukbwa mbele ya Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye kufuzu.

Wapi na wapi kunywesheleza mahujaji na kutumikia miskiti kulinganisha na imani, Hijra na Jihadi?
Umekwishapita mfano wa Aya hii katika Juzuu hii Sura (8:72). Neno cheo kikubwa hapa halina maana ya kuzidiana, isipokuwa ni kuthibitisha ubora wa waumini tu, kwani makafiri hawana cheo hata kile kidogo mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mola wao anawabashiria rehema kutoka kwake na radhi na pepo ambazo watapata humo neema zitakazodumu. Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu kuna malipo makubwa.

Anasema mwenye Bahrul-Muhit: “Waumin wamesifika na sifa tatu: Imani, Hijra na Jihad. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawakabili na matatu Rehema, Radhi na Pepo”

Razi amerefusha maneno katika kubainisha tofauti ya sifa hizi. Ama sisi tunaona kuwa sifa hizo pamoja na kufuzu na malipo ni kwa maana moja kwamba waumin wenye kufanya amali wako katika hifadhi ya Mwenyezi Mungu. Na neno ‘Radhi ya Mwenyezi Mungu’ lingetoshelezea yote, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema:

وَرِضْوَانٌ مِنَ اللَّهِ أَكْبَرُ ۚ {72}

“Na radhi za Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi.” (9:72).

Lakini Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) alitaka kuwatukuza na kuwahimiza waja wake kwenye Imani na Matendo mema.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا آبَاءَكُمْ وَإِخْوَانَكُمْ أَوْلِيَاءَ إِنِ اسْتَحَبُّوا الْكُفْرَ عَلَى الْإِيمَانِ ۚ وَمَنْ يَتَوَلَّهُمْ مِنْكُمْ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ {23}

Enyi mlioamini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa mawalii ikiwa wamestahabu kufuru kuliko imani. Na atakayewafanya mawalii katika nyinyi basi hao ndio madhalimu.

قُلْ إِنْ كَانَ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ وَإِخْوَانُكُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ وَعَشِيرَتُكُمْ وَأَمْوَالٌ اقْتَرَفْتُمُوهَا وَتِجَارَةٌ تَخْشَوْنَ كَسَادَهَا وَمَسَاكِنُ تَرْضَوْنَهَا أَحَبَّ إِلَيْكُمْ مِنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ وَجِهَادٍ فِي سَبِيلِهِ فَتَرَبَّصُوا حَتَّىٰ يَأْتِيَ اللَّهُ بِأَمْرِهِ ۗ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ {24}

Sema ikiwa baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa zenu na mali mlizozichuma na biashara mnazohofia kuharibikiwa, na majumba mnayopenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na jihadi katika njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki