read

Aya 23-24: Msiwafanye Baba Zenu Na Ndugu Zenu Mawalii

Maana

Enyi mlioamini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa mawalii ikiwa wamestahabu kufuru kuliko imani.

Makusudio ya uwalii hapa ni kusaidia. Uislamu unaamrisha kutokata udugu, ukazingatia kuwa kuwaudhi wazazi ni katika madhambi makubwa, ukausia ujirani, kutekeleza haki ya urafiki na mikataba na ahadi zote.

Vilevile waislamu wamehalalishiwa kuwafanyia wema na uadilifu washirikina na yote hayo yanajuzu, lakini kwa sharti la kutoharamisha halali au kuhalalisha haramu.

Kwa mfano baba akiwa upande wa batili, haijuzu kwa mtoto kumsaidia, bali ni juu ya mtoto kumzuia na kumkataza akiweza.

Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu ‘ikiwa wamestahabu kufuru kuliko imani,’ inakusanya maasia yote. Ikiwa baba yako au ndugu yako ni Mwislamu na akamdhulumu mwingine, basi ni juu yako kumsaidia aliyedhulumiwa dhidi ya huyo baba yako au ndugu yako.

Na atakayewafanya mawili katika nyinyi basi hao ndio madhalimu.

Kuna Hadith isemayo “Mwenye kufanya dhuluma na mwenye kuisaidia na mwenye kuiridhia ni mshiriki” Kwa maneno mengine ni kuwa haki iko juu ya ndugu na urafiki.

Sema ikiwa baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa zenu na mali mlizozichuma na biashara mnazohofia kuharibikiwa, na majumba mnayopenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na jihadi katika njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki.

Inasemekana kuwa Aya hii ilishuka kwa ajili ya tukio maalum. Inawezekana kuwa ni kweli, lakini tamko lake ni la ujumla, pia hukumu yake.

Aya hii inawaelezea mumin kwa maelezo wazi na ya uhakika. Mwenye kuathirika na haki kuliko maslahi yake binafsi wakati yana-pogongana na haki basi huyo ni mumin mwema, vinginevyo basi ni mnafiki mwovu.

Hiyo ndiyo njia inayomtofautisha mumin na asiyekuwa mumin, kama ilivyoelezewa na Aya. Kutajwa ndugu mali na majumba ni mfano tu wa kuweka mbele manufaa kuliko haki ambayo Mwenyezi Mungu ameitolea ibara ya kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Zaidi ya hayo yako manufaa mengine; kama vile kupupia maisha, kupenda jaha, utawala n.k.

Mtu kwa maumbile yake hujipenda na kupenda watu wake na mali yake, na dini haikatai hilo, wala haimzuii yeyote kustarehe atakavyo na kumpenda amtakaye, mradi tu amwogope Mwenyezi Mungu katika starehe hiyo, na yote hayo yamekutana na juhudi yake sio juhudi za wengine.

Imepokewa kutoka kwa Bukhari kwamba Umar Bin Al-Khattab alimwambia Mtume (saw). Kwa hakika wewe unapendeza kwangu kuliko chochote isipokuwa nafsi yangu iliyo mbavuni mwangu.”

Mtume (saw) akamwambia: Hapana! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, ni mpaka niwe napendeza kwako kuliko nafsi yako iliyo mbavuni mwako.”

Wala hakuna maana ya kumpenda Mtume (saw) isipokuwa kumtii na kufanya mambo kulingana na sharia yake. Tumeyazungumzia haya katika Juz.5 (4:135)

لَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّهُ فِي مَوَاطِنَ كَثِيرَةٍ ۙ وَيَوْمَ حُنَيْنٍ ۙ إِذْ أَعْجَبَتْكُمْ كَثْرَتُكُمْ فَلَمْ تُغْنِ عَنْكُمْ شَيْئًا وَضَاقَتْ عَلَيْكُمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ ثُمَّ وَلَّيْتُمْ مُدْبِرِينَ {25}

Hakika Mwenyezi Mungu amewasaidia katika mwahala mwingi, kama vile na siku ya Hunain ulipowafuraisha wingi wenu. Lakini haukuwafaa chochote, na ardhi ikawa finyu juu yenu ingawa ilikuwa pana, kisha mkageuka mkirudi nyuma.

ثُمَّ أَنْزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَعَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَأَنْزَلَ جُنُودًا لَمْ تَرَوْهَا وَعَذَّبَ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الْكَافِرِينَ {26}

Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya waumin. Na akawateremshia majeshi ambayo hamkuyaona. Na akawaadhibu wale waliokufuru. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri

ثُمَّ يَتُوبُ اللَّهُ مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ عَلَىٰ مَنْ يَشَاءُ ۗ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {27}

Kisha baada ya haya Mwenyezi Mungu atamkubalia toba amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.