read

Aya 25-27: Mwenyezi Mungu Amewanusuru

Kisa Cha Hunain

Hunain ni bonde lilioko baina ya Makka na Taif. Vita vilvyopiganwa hapo vinaitwa vita vya Hunain, vita vya Autas au vita vya Hawazin. Vita hivyo vilikuwa mwezi wa Shawwal (mfunguo mosi) mwaka wa nane Hijra.

Mtume (saw) alipoiteka Makka walimlia njama Hawazin na Thaqif wakakusanya maelfu kumpiga vita Mtume. Ilipomfikia Mtume (saw) habari hiyo, alijiandaa na kukusanya jeshi la watu elfu 12, Elfu kumi kati yao ni Maswahaba wake aliotoka nao Makka na elfu mbili walikuwa ni Tulaqau1 akiwemo Abu Safyan na mwanawe Muawiya.

Mtume (saw) akaelekea kwa Hawazin njia yake ilipitia bonde la Hunain na ilikuwa nyembamba yenye maporomoko. Jeshi la adui lilikuwa limewatangulia kufika kwenye uchochoro wake wakajificha.

Mara tu jeshi la Waislamu lilipofika katikati ya bonde, maadui waliwamiminia mishale, watu wakaanza kusambaratika na Abu Sufyan ndiye wa mwanzo wao.

Sheikh Ghazali katika kitabu Fiqh Sera. Anasema: “Wengine walirudia ukafiri wao. Abu Sufyan akasema: ‘Kushindwa kwao hakutakoma mpaka baharini.’ Hilo si ajabu kwani mburuga alizokuwa akiagulia wakati wa Jahilia bado ziko mkobani mwake”.

Ali akabaki na Mtume wa Mwenyezi Mungu akiwa ameuchomoa upanga wake, huku Abbas ameshika lijamu ya farasi wake, Al-fadhl bin Abbas akiwa kuumeni kwa Mtume pamoja na Mughira Bin Harith Bin Abdul Muttalib, Zaid Bin Usama na Aiman Bin Ummu Aiman. Wakapigana mbele ya mtume wa Mwenyezi Mungu.

Washirikina walipoona waislam wanasamabaratika, walitoka kwenye ngome za bonde wakimfuatia Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume (saw) akamwambia Ami yake Abbas aliyekuwa na sauti kubwa. Waite watu na uwakumbushe ahadi.

Akanadi kwa sauti kubwa: “Enyi watu wa Baia ya mti! (Mliombai mtume chini ya mti) Enyi watu wa Sura ya Baqara! Mnakwenda wapi? Kumbukeni ahadi mliyomwahidi Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ansar waliposikia mwito wa Abbas walirudi na wakavunja ala za panga zao wakiwa wanasema: Labeka! Labeka! Wakamkabili adui na makundi mawili yakapambana vikali

Mshika bendera na shujaa wa washirikina alikuwa ni Abu Jarwal. Huyu alikuwa akiwashambulia waislamu na kuwaua. Ali Bin Abu Talib akapambana naye na kumuua. kwa kuliwa kwake jeshi la washirikina lilitawanyika na ushindi wa Mtume (saw) na wa waumin ukapatikana.

Tulaqau walipojua kuwa waislamu wameshinda na kuna ngawira nyingi, walirudi kwa Mtume (saw). Katika Tafsir Bahrul-Muhit imeelezwa kuwa Tulaqau walikimbia wakikusudia waumin washindwe”.

Sharqawi naye anasema katika kitabu Muhammad Rasulul-Huriyya (Muhammad Mtume wa uhuru): “Maquraish elfu mbili wakiongozwa na Abu Suffin walisilimu kwa hofu au tamaa. Walikuja hiyo siku si kwa ajili ya kuusaidia Uislamu bali ni kwa ajili ya kuudhalilisha na kueneza ulegevu kwa wapiganaji jihadi waliowatangulia”.

Hivi ndivyo walivyo wanafiki na watu walio huku na kule. Wanajifanya ni wenye ikhlas, wanajiingiza katika safu za wapigania ukombozi na kupanga mambo. Wakichunguza mbinu zao, kisha wanapanga njama, zikifaulu njama zao, inakuwa wamepata waliyoyataka, au wakifaulu wakombozi, basi husema sisi na nyinyi tuko pamoja. Yametangulia maelezo ya hawa katika kufasiri Juz. 5 (4:141)

Hakika Mwenyezi Mungu amewasaidia katika mwahala mwingi.

Kama vile vita vya Badr, Quraidha, Nadhr, Hudaibiya, Khaibar na kuiteka Makka.

Na siku ya Hunain ulipowafurisha wingi wenu.

Razi anasema. “Mtu moja katika waislam alisema. Hatutashindwa kwa uchache leo. Akaona vibaya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Inasemekana kuwa aliyesema hayo ni Mtume (saw) na ilisemakana ni Abu Bakr. Kutegemeza neno hili kwa Mtume ni mbali.”

Lakini haukuwafaa chochote, na ardhi ikawa finyu juu yenu ingawa ilikuwa pana, kisha mkageuka mkirudi nyuma.

Kuanzia kufura kichwa hadi kulemewa kabisa kiasi cha kutopata hata upenyo wa kujiokoa na adui yao. Huu ndio mwisho wa kila mwenye kujigamba na kumdharau adui yake.

Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya waumin.

Utulivu ni kuwa na mategemeo na umakini. Maana ya kuuteremsha kwa Mtume (saw) ni kubakia kwake mwenye kuthibiti katikati ya vita akiwa makini na mwenye ushupavu akipangilia mambo, ingawaje wanajeshi wake, waliokuwa kiasi cha watu elfu kumi na mbili, wamekimbia wote, isipokuwa watu wasiozidi kumi, na huku jeshi la maadui likiwa na idadi ya maelfu.

Wapokezi wanasema Mtume (saw) alikuwa akimchochea nyumbu wake kuwaelekea maadui huku akiwalingania wale waliokimbia. Njooni enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi ni Mtume sisemi uwongo mimi ni mwana wa Abdul-Muttalib.

Waumin ambao Mwenyezi Mungu aliwateremshia utulivu ndio wale waliothibiti bila ya kumkimbia, na wale waliorudi baada ya kushindwa na kuitikia mwito wa Mtume (saw) wakiwa wenye ikhlas. Maana ya kuteremshiwa utulivu ni kuwa na utulivu katika nyoyo zao na kuwaondokea hofu.

Na akawateremshia majeshi ambayo hamkuyaona.

Razi anasema : “Hakuna tofauti kwamba makusudio ni kuteremshwa Malaika”. Ama sisi tunaitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ana jeshi la Malaika na lisilokuwa Malaika kwa aina isiyokuwa na idadi. Miongoni mwa aina hizo ni nguvu ya nafsi na silika yake na nguvu za nje. Aya haikubainisha aina hii ya jeshi aliloteremsha Mwenyezi Mungu siku ya Hunain. Kwa hiyo ujuzi wake tunamwachia Mwenyezi Mungu aliyesema:

وَمَا يَعْلَمُ جُنُودَ رَبِّكَ إِلَّا هُوَ ۚ {31}

“Na hakuna ajuaye majeshi ya Mola wako ila yeye tu” (74:31)

Na akawaadhibu wale waliokufuru.

Aliwaadhibu duniani kwa kuuliwa kutekwa, kushindwa na kuchukuliwa mali na atawaadhibu Akhera kwa moto wa Jahannam na ni marejeo mabaya.

Kisha baada ya haya Mwenyezi Mungu atamkubalia toba amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Mwenyezi Mungu ni mkarimu, hashindwi kusamehe dhambi kubwa, na mlango wake uko wazi kwa kila mwenye kubisha. Aliyekimbia Mtume wa Mwenyezi Mungu katika waislamu, kisha akatubia basi Mwenyezi Mungu anawapenda wanaotubia. Na mwenye kukufuru na akampiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) kisha akatubia na akaamini na akafanya amali njema basi yeye ni katika waliofaulu.

Wanahistoria wanasema baada ya kwisha vita na ngawira kugawanywa ulikuja ujumbe kutoka Hawazin hali ya kuwa ni waislamu. Wakasema Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu wewe ni bora wa watu na mwema wao, wake zetu na watoto wetu wametawaliwa na mali zetu zimechukuliwa. Basi Mtume (saw) akawakubalia Uislamu wao na wakarudishiwa wake na watoto wao.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَٰذَا ۚ وَإِنْ خِفْتُمْ عَيْلَةً فَسَوْفَ يُغْنِيكُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ إِنْ شَاءَ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {28}

Enyi Mlioamini! Hakika washirikina ni najis, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu baada ya mwaka wao huu. Na kama mkihofia umasikini, basi hivi karibuni Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake akitaka. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.
  • 1. Mahuria: walioachwa huru siku ya kutekwa Makka