read

Aya 28: Washirikina Ni Najisi

Enyi Mlioamini! Hakika washirikina ni najis, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu baada ya mwaka wao huu.

Yaani mwaka wa tisa wa Hijra, mwaka ambao Ali (as) aliwasomea watu Aya za kujitoa katika dhima.

Aghlabu Qur’an hulitumia neno washirikina kwa wanaoabudu masanamu; hasa washirikina wakiarabu. Na hutumia neno ‘Watu wa Kitab’ kwa mayahudi na wanaswara (wakristo). Kuunganisha washirikina na watu wa Kitab katika Aya isemayo:

مَا يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَلَا الْمُشْرِكِينَ{105}

“Hawapendi waliokufuru miongoni mwetu wa Kitab wala washirikina” (2:105)

na ile isemayo:

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ {6}

“Hakika waliokufuru katika watu wa Kitab na washrikina…”(98:6)

Kunafahamisha kuwa kinachounganishwa si sawa na kinachouganishiwa, ingawaje inawezekana kuunganisha maalum kwenye ujumla, lakini ni kulingana na jumla yenye ilivyo.

Mafakihi wametofautiana kuhusu kuwazuia makafiri kuingia msikitini. Shafii anasema wanazuiwa mskikiti mtukufu (Masjidul-haram) tu. Malik anasema watazuiwa misikiti yote. Abu Hanifa anasema hazuiwi msikiti wowote. Hayo yamo katika Tafsir ya Razi katika kufasri Aya hii.

Tuonavyo sisi ni kuwa ni wajibu kuzuia najisi kwenye msikiti wowote na ikiwemo ndani ni wajibu kuitoa, ni sawa iwe ni ya mtu, mnyama au kitu kingine chochote. Iwe ni najisi ya itakayochafua msikiti na kuivunjia heshima yake au la. Dalili ya hayo ni kwamba hukumu ya kuharamisha imeachwa bila ya kufungwa na kitu chochote.

Tukisema mtu aliye najisi tuna maanisha mkanushaji na mwabudu masana- mu na mizimu. Ama watu wa Kitab tumethibtisha utohara wao katika Juz. 6 (5:5)

Unaweza kuuliza kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu” inafahamisha kusihi kauli ya Shafii, kuwa kuzuia kunahusika na Msikiti Mtakatifu (Masjidul-haram) tu, sio mwengineo. Kwa sababu hakusema wasikaribie kila msikiti.

Jibu mkusanyiko wa Aya unafahamisha kuenea, sio mahsusi. Kwa sababu linalokuja haraka kwenye fahamu ni kuwa sababu ya kuzuiwa kuingia ni najisi na kuheshimu msikiti mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hakuna mwenye shaka kwamba kila msikiti unaheshimiwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sababu unanasibishiwa kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hukumu inakwenda pamoja na sababu yake kwa kuthibitisha na kukanusha.

Ndio maana mafakihi wakakongamana kuwa wiski ni haramu, ingawaje hakuna kauli wazi juu yake, kwa kutosheka na sababu ya kuharimishwa ulevi.

Na kama mkihofia umasikini, basi hivi karibuni Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake akitaka. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

Washirikina katika pembe zote za bara Arabu walikuwa wakielekea Makka kuhiji na kufanya biashara. Watu wa Makka walikuwa wakinufaika na hilo, wakiuza na kununua kutoka kwao, pia walikuwa wakiwakodisha majumba. Na Makka iko katika jangwa lisilokuwa na mmea.

Basi Mwenyezi Mungu alipowazuia washirikina baadhi ya watu wa Makka walihofia ufukara, ndipo Mwenyezi Mungu (swt) akawaambia hivyo; yaani mkihofia ufukara kwa sababu ya kukatika mawasiliano ya washirikina na Makka, basi Mwenyezi Mungu atawapa badali kwa njia nyingine.

Kwani sababu za riziki mbele yake ni idadi ya matone ya mvua; kama ilivyoelezwa katika Hadith.

Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, aliwafungulia waislamu miji na ngawira, wakaingia watu kwa makundi katika dini yake, wakaelekea Makka kwa mamilioni pamoja na nyoyo zao na mali zao.

Watu wa Makka wakaona faida ambayo hata hawakuiota.

Utauliza nini lengo la kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Akitaka’ pamoja na kuwa alikwishataka?

Jibu: Yanaweza kuwa makusudio ni kudokeza kuwa visababishi vinapita kwa sababu zake na inaweza kuwa makusudio ni kuwafundisha waja wake wamtegemee Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote na malengo yao wayaambatanishe na matakwa yake Mwenyezi Mungu pamoja na juhudi; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا {23}

إِلَّا أَنْ يَشَاءَ اللَّهُ ۚ{24}

Wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya kesho ispokuwa Mwenyezi Mungu akitaka (inshaallah)” (18:23-24)

قَاتِلُوا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ الْحَقِّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حَتَّىٰ يُعْطُوا الْجِزْيَةَ عَنْ يَدٍ وَهُمْ صَاغِرُونَ {29}

Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho wala hawaharamishi aliyoharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawashiki dini ya haki, miongoni mwa waliopewa Kitab, mpaka watoe kodi kwa mkono hali wametii.

وَقَالَتِ الْيَهُودُ عُزَيْرٌ ابْنُ اللَّهِ وَقَالَتِ النَّصَارَى الْمَسِيحُ ابْنُ اللَّهِ ۖ ذَٰلِكَ قَوْلُهُمْ بِأَفْوَاهِهِمْ ۖ يُضَاهِئُونَ قَوْلَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ قَبْلُ ۚ قَاتَلَهُمُ اللَّهُ ۚ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ {30}

Na mayahudi wanasema, Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao, wanayaiga maneno ya wale waliokufuru zamani. Mwenyezi Mungu awangamize! Wanageuzwa wapi?

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِنْ دُونِ اللَّهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَٰهًا وَاحِدًا ۖ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ {31}

Wamefanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu na Masih mwana wa Maryam. Wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwambudu Mungu mmoja hakuna Mungu ila yeye Ametakata na wanayomshirikisha nayo.

يُرِيدُونَ أَنْ يُطْفِئُوا نُورَ اللَّهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّهُ إِلَّا أَنْ يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ {32}

Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu amekataa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wamechukia.

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ {33}

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia.