read

Aya 29 – 33: Piganeni Na Wasiomwamni Mwenyezi Mungu

Maana

Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho wala hawaharamishi aliyoharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawashiki dini ya haki, miongoni mwa waliopewa Kitab, mpaka watoe kodi kwa mkono hali wametii.

Baada ya Mwenyezi Mungu (swt) kuamrisha kupigana na washirikina ikiwa hawakusilimu wala hawakutoka, katika Aya hii ameamrisha kupigana na watu wa Kitab ikiwa hawakutoa kodi na kunyenyekea hukumu ya Kiislam.

Mwenyezi Mungu amewasifu kuwa hawamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho wala hawaharamishi haramu ya Mwenyezi Mungu au kufuata dini ya haki.

Ilivyo ni kwamba neno ‘miongoni’ katika kauli yake Mwenyezi Mungu ‘miongoni mwa wale walopewa Kitab’ ni la kubainisha jinsi. Na imesemekana ni la kufanya baadhi.

Hapa kuna maswali mawili: Kwanza Aya imeawakanushia watu wa Kitab kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho pamoja na kwamba wao wanaamini kuweko Mwenyezi Mungu. Kwa sababu neno watu wa Kitab hilo lenyewe linafahamisha kumwamini kwao Mwenyezi Mungu ambaye ameteremsha Tawrat na Injil.
Vile vile wanaamini siku ya mwisho kwa nukuu ya Aya isemayo: “Na wanasema: hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu” Juz. 1 (2:80) Ingawaje ni kweli kuwa wao hawafuati dini ya haki. Mayahudi wanaabudu mali na kanisa linauza cheki za msamaha?

Jawabu la swali hilo tunalipata katika Aya iliyo baada yake, bila ya kuweko kati kitu kingine:

Na mayahudi wanasema, Uzeir ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu.

Njia ya jawabu ni kuwa Mayahudi na Wakristo wamemfanya Mwenyezi Mungu kuwa na mtoto. Maana yake ni kuwa wanamwamini Mwenyezi Mungu asiyekuwepo ila katika mawazo yao tu. Ama Mungu aliyeko kweli, wao hawamwamini. Wameleta picha ya kua ni Mungu mwenye watoto. Ama Mola wa uhakika ambaye hakuzaa wala hakuzaliwa wao hawamwamini wala hafungamani nao kwa mbali au karibu.

Kwa ufupi ni kuwa Mungu aliyeko hawamwamini na wanamwamini mungu asiyeko. Natija ya yote hayo ni kuwa wao hawamwamini Mwenyezi Mungu.

Kimsingi ni kwamba asiyemwamini Mwenyezi Mungu haamini akhera kwa imani sawa, wala hafuati dini ya haki, hata kama itafikiriwa kuwa yeye ni katika wanaoamini akhera na wenye kufuata dini ya haki. Kwa sababu kumwamini Mwenyezi Mungu ndio asili (shina) mengineyo ni matawi, yaani yeye anaamini akhera na dini ambayo haina athari yoyote isipokuwa katika mawazo yao tu; kama kusema kwao: Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu. Dini hiyo ndiyo ile iliyotajwa na yule aliye- sema: “Dini inatengenezwa na mawazo na njozi.”

Swali la pili, Uislamu haumlazimishi yeyote kuukubali kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ {256}

“Hakuna kulazimishwa katika dini….”Juz. 3(2:256)

Na pia kauli yake Mwenyezi Mungu:

أَفَأَنْتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ {99}

Basi je, wewe unawalazimisha watu hata wawe waumini? (10: 99).

Sasa imekuwaje kuamrishwa kupigana na watu wa Kitab mpaka waamini au watoe kodi?

Swali hili tumelitaja katika kufasiri Aya ya pili katika Sura hii, ambayo imeamrisha kupigana na washirikina. Tukajibu kwamba amri ya kupigana nao ilikuwa ni hukumu maalum ya wakati huo, kwa sababu mahsusi, kwamba jamii ya Kiislam ndio ilikuwa inaanza na washirikina walikuwa ni kikosi cha tano1 walifanyia vitimbi Uislamu na watu wake.

Masilahi yakawa ni kuwatoa bara arabu au kuwaua. Na amri ya kupigana hapa ni mahsusi kwa watu wa Kitab ambao walikuwa wakiungana na washirikina kuwapiga vita waislamu kama walivyofanya Mayahudi wa Madina na walio pembeni baada ya kuwekeana mkataba wa amani na mtume na kufanya muungano nao.

Zaidi ya hayo, kiini cha Sura hii ni vita vya Tabuk, kama itakavyoelezwa katika Aya 38 na zinazofuatia. Na, Mtume (saw) alipata habari kwamba Warumi wakiwa Sham wanaanda majeshi kwa ajili ya kuumaliza Uislamu na watu wake. Na dalili zilionyesha wazi kuwa watu wa Kitab walikuwa ni wasaidizi na mawakala wa wakristo wa Roma; na kwamba wao walikuwa wakila njama nao dhidi ya Mtume na wafuasi wake waumini.
Kwa ajili hiyo ndipo ikawa hukumu ni kupigana nao au waweke silaha chini na wawe chini ya hukumu ya Kiislamu, pamoja na kutoa kodi ambayo itaonyesha usalama wao na kutekeleza kwao ahadi yao. Wakitoa kodi basi ni wajibu kuwapa amani kuwahami na kuwapa uhuru katika dini yao. Wakisilimu watapata waliyonayo waislamu. Vinginevyo basi ni kuwaua kujikinga na shari yao.

Wafasiri na mafakihi wamerefusha maneno kuhusu kodi, kiasi chake na sharti zake. Maneno yao wakati huo yalikuwa na faida ambapo uislamu ulikuwa na dola yake na nguvu zake. Ama leo mazungumzo kuhusu kodi ni kuongeza maneno tu.

Na mayahudi wanasema, Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema, Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu.

Kauli ya Wakristo kuwa Masih ni mwana wa Mwenyezi Mungu ni maarufu na tumeizungumzia katika Juz.6 (5:18)

Ama kauli ya Mayahudi kuhusu Uzair, mwenye Tafsir Al-Manar amenukuu kuwa jina la Uzair liko katika vitabu vitakatifu vya mayahudi. Vile vile amenukuu kutoka Daira tul-Maarifil-Yahudiyya kwamba zama za Uzair ndizo zama nzuri za Historia ya mayahudi. Katika Tafsir ya Tabari, Razi na Tabrasi imeelezwa kwamba kikundi cha Mayahudi walimwambia Mtume (saw): Tutakufuata vipi nawe umeacha Qibla chetu na wala hudai kuwa Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu, ndipo ikashuka Aya.

Kwa vyovyote ilivyo ni kwamba Mtume aliwakabili Mayahudi wa zama zake kwa Aya hii, na haikunukuliwa kutoka kwa yeyote katika wao kumkosoa au kumpinga pamoja na kumkadhibisha kwao sana Mtume. Kwa hiyo inafahamisha kuwa wao waliamini hivyo wakati huo.

Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao, wanayaiga maneno ya wale waliokufuru zamani. Mwenyezi Mungu awangamize! Wanageuzwa wapi?

Yaani kauli ya mayahudi inafanana na kauli ya washirikina waarabu ambao walisema: Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu, vile vile kauli ya waabudu mizimu wa zamani, waroma, wayunani, wabudha na wengineo.

Wamefanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu na Masih mwana wa Maryam.

Hii ni dalili nyingine kwamba wao hawamwamini Mwenyezi Mungu bali wanaamini wanayoyasema watu wa dini yao na itikadi yao. Imam Jaffer As-sadiq (as) anasema: “Wao hawakuwafungia swaum au kuwaswalia, lakini waliwhalalishia haramu na wakawaharamishia halali, wakawafuata na kuwaabudu bila ya kutambua.”

Haya ni sawa na yaliyo katika Hadith kwamba Udey bin Hatim alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): Sisi hatuwaabudu wao.

Mtume akamwambia: Je, hawaharimishi aliyohalalisha Mwenyezi Mungu mkayaharamisha; na kuhalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu mkayahalalisha? Udey akasema: Ndio. Mtume akasema huko ndiko kuwaabudu.

Voltare anasema: Makasisi wetu hawajui chochote isipokuwa sisi ni wepe-si wa kusadiki wayasemayo.

Wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwambudu Mungu mmoja hakuna Mungu ila yeye Ametakata na wanayomshirikisha nayo.

Razi katika Tafsir yake anasema: Maana yako dhahiri. Lakini mfasiri mwingine ambaye alitaka asema tu: “Yaani wamwabudu Mola Mkuu”.

Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao.

Makusuido ya nuru ya Mwenyezi Mungu hapa ni Uislamu. Maana ni kuwa watu wa Kitab walijaribu kuumaliza Uislamu kwa kila njama na uwongo; ikawa ni kama mtu anayejaribu kuzima nuru, ambayo imeenea ulimwenguni, kwa pumzi yake.

Na Mwenyezi Mungu amekataaa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wanachukia.

Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, kupitia mdomoni mwa Mtume wake, kuunusuru Uislamu na kuudhihirisha mashariki ya ardhi na magharibi. Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na ahadi ambayo inafahamisha utume wa Mohammad (saw) ikathibiti na ukweli wake katika kila alilolitolea habari.

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wanachukia.

Aya hii ni ubainifu na ufafanuzi wa Aya iliyo kabla yake. Mwenyezi Mungu aliwajalia waislamu kuwashinda washirikina katika miji ya Kiarabu, Mayahudi walipowatoa huko, wakristo katika Sham na Majusi katika Fursi. Imam Ali anasema: “Hakika huu Uislamu umedhalilisha dini (nyingine) kwa utukufu wake, ukaziondoa mila kwa utukufu wake na ukawatweza maadui zake kwa utukufu wake.”

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۗ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ {34}

Enyi mlioamini! Hakika wengi katika watawa na makuhani wanakula mali za watu kwa batili na kuwazuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Na wale walimbikizao dhahabu na fedha na hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi wabashirie adhabu iumizayo.

يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنْفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَكْنِزُونَ {35}

Siku zitakapotiwa moto kati- ka moto wa Jahannam, na kwazo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao; Haya ndiyo mliyojilimbikizia, basi onjeni yale mliyokuwa mkiyalimbikiza.
  • 1. Askari wa siri (Fifth Colomn)