read

Aya 34 – 35: Wale Wanaokusanya Dhahabu Na Fedha

Maana

Enyi mlioamini! Hakika wengi katika watawa na makuhani wanakula mali za watu kwa batili na kuwazuilia njia ya Mwenyezi Mungu.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (swt) amewataja mayahudi na wakristo kwamba wao wanawafanya viongozi wao wa kidini ni waungu badala ya Mwenyezi Mungu. Katika Aya hii amewataja hao viongozi kwa kula mali ya batili na kuzuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya kula mali kwa batili ni kuchukua bila ya njia ya sharia; kama vile rushwa na riba ambayo ilienea sana kwa mayahudi. Pia uuzaji wa cheki ya msamaha kwa wakatoliki nk. Wanahistoria wanasema watu wa kanisa waliwahi kuwa ndio matajiri zaidi.

Makusudio ya kuzuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu ni kuwazuilia akili zao na kuzuia watu kukubali Uislam, bali na kuwafanya wautuhumu na Mtume wake.

Voltaire alilichagiza kanisa na kuwalaumu wakubwa wake kwa ulafi wao wa mali; akaituhumu Tawrat kutokana na mgongano. Akazuiliwa na kanisa na baadhi ya kubwa wake wakataka afungwe maisha. Akaogopa sana mwanafalsafa huyu wa kifaransa.1 Hakupata njia yoyote ya kuokoka isipokuwa kutetewa na baba mtakatifu Bendedict xiv kwa kutunga Kitab cha kumtukana Muhammad. Akafanya hivyo na akasamehewa na kanisa; kikabarikiwa kitabu na mwandishi wake.

Abu Dhar Na Ujamaa

Na wale walimbikizao dhahabu na fedha na hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi wabashirie adhabu iumizayo.

Kuna maneno mengi kuhusu Aya hii. Baadhi wakaitolea dalili juu ya kuweko ujamaa (usoshalist) katika Uislamu. Wengine wamediriki hata kusema kuwa Abu dharr alikuwa mjamaa kwa vile yeye alikuwa akiwatisha, kwa Aya hii, wale walioathirika na mali ya Mwenyezi Mungu kuliko watu wa Mwenyezi Mungu.

Tutaonyesha maana ya Aya na kila linalofugamana nayo kwa karibu au mbali, na kwayo tutaihukumu kauli ya anayeutolea dalili ujamaa wa Abu dhar kwa Aya hii:

1. Muawiya bin Abu Sufyan alisema kuwa Aya hii ilishuka kwa watu wa Kitab tu na wala haiwahusu Waislamu. Yaani, kwa mtazamo wake, Waislamu wanaweza kurundika mali wanavyotaka na wala wasitoe chochote katika njia ya Mwenyezi Mungu. Alinukuu kauli hii kutoka kwa Uthman bin Affan.

Kwenye Durrul Manthur ya Suyuti imeelezwa kuwa Uthman alipoandika msahafu walitaka kuondoa herufi wau (na) katika kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na wale walimbikizao dhahabu na fedha… ili iwe ‘Walimbikizao ni sifa ya makasisi na watawa. Sahaba mmoja akapinga na kusema: Mtaiweka wau au ni uweke upanga wangu begani kwangu, ndipo wakaiweka.

Ilivyo hasa ni kuwa Aya inamhusu kila mwenye kukusanya mali na asitoe katika njia ya Mwenyezi Mungu, awe Mwislamu au si Mwislamu, kwa kuchukulia kuwa tamko ni la kuenea.

Imepokewa kutoka kwa Zaid bin Wahab kwamba alipita Rabdha, akamuona Abu dharr huko, akamuuliza: Kitu gani kilichokufikisha hapa? Akasema: Nilikuwa Sham nikasoma: ‘Na wale walimbikizao dhababu ….’ Muawiya akasema Aya hiyo haituhusu sisi ni ya watu wa Kitab. Nikasema: Hakika hiyo inatuhusu sisi na wao. Basi akanishtaki kwa Uthman ndipo wakanifukuza hadi hapa unaponiona.

2. Neno dhahabu na fedha ni Mahsus, lakini hukumu ni ya ujumla kwa aina zote za mali, hata ardhi madini miti majengo mifugo, magari na viwanda. Kwa sababu waliotishiwa adhabu iumizyao na Mwenyezi Mungu ni matajiri bahili na wala sio wanaomiliki dhahabu na fedha tu. Vingenevyo ingekuwa matajiri wa mafuta na wengineo ndio watu wema na watukufu zaidi kwa Mwenyezi Mungu duniani na akhera.

Linalotufahamisha kuwa, makusudio ni ya ujumla ni kuwa Aya hii iliposhuka iliwashughulisha waislamu kwa sababu wao walifahamu mali zote. Walipomuuliza Mtume (saw) aliwathibitshia walivyo fahamu na kuwambia: “Hakika Mola hakufaradhisha zaka ila kwa kuifanya njema iliyobakia katika mali zenu; na hakika amefaradhishia warithi mali zinazobakia baada yenu.”

3. Kutumia katika njia ya Mwenyezi Mungu ni pamoja na jihadi ya kupigania dini na nchi, kujenga madrasa, mahospitali na nyumba za mayaitma. Vile vile kuwapa sadaka mafukara kumtunza mke na watoto. Sehemu nzuri ya kutumia ni ile inayoienzi na haki na watu wake.

4. Madhehebu mane yamekongamana kuwa katika mali hakuna haki yoyote isiyokuwa zaka; kama ilivyoelezwa katika Ahkamul Qur’an cha Abu Bakr Al-Muafirir Al-andalusi.

Mafakihi wengi wa Kishia wamesema katika mali hakuna haki zaidi ya khumsi na zaka. Sheikh Tusi anasema “Iko haki nyingine nayo ni ile aliyoiaishiria Imam Saffer As-Sadiq kwa kauli yake: “Hakika Mwenyezi Mungu amefaradhisha katika mali za matajiri haki nyingine zisizokuwa zaka.

Kwa sababu yeye amesema:

وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ {19}

“Na ambao katika mali zao iko haki maalum kwa ajili ya aombaye au ajizuiaye” (51:19)

Haki maalum ni kitu chochote anachojilazimisha mtu kwa kadiri ya uwezo wake, atatoa kila siku akipenda, kila Ijuma au kila mwezi; kiwe kichache au kingi, mradi tu kiwe ni cha kudumu. Lakini kauli ya Imam, atajifaradhishia yeye mwenyewe, inatambulisha suna sio wajibu, kwa sababu wajibu unatokana na Mwenyezi Mungu si mwenginewe.

Tuonavyo sisi, baada ya kufuatilia Aya za Qur’an Tukufu, ni kwamba matajiri wanao wajibu, sio suna, kujitolea mali zao zaidi ya zaka na khums; kwa ajili ya kuipigania dini na nchi ihitajika; na ni juu ya mkuu wa waislamu kuwalazimisha hilo. Bali pia ni wajibu wajitolee kwa nafsi ikihitajika. Aya za namna hii ziko chungu nzima.

5. Siku zitakapotiwa moto katika moto wa Jahannam, na kwazo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao; Haya ndiyo mliyojilimbikizia, basi onjeni yale mliyokuwa mkiyalimbikiza.

Hili ni fumbo la adhabu kali na vituko vyake. Aya hiyo ni mfano wa Aya isemayo: “Watatiwa mandakozi ya hivyo walivyofanyia ubakhili siku ya kiyama” Juz.4 (3: 180)

6. Kutokana na yaliyotangulia imetubainikia kuwa Aya inafahamisha kwa kinukuu na kimaana kwamba ni wajibu juu yao matajiri kutoa sehemu ya mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kama wataifanyia uchoyo, basi Mwenyezi Mungu atawadhibu kwa adhabu kali. Ama kiwango cha fungu hili, na kwamba je, ni khumsi au ushuri, zaidi au chini na kwamba je, ni zaka au zaidi, Aya haifahamishi kwa Ibara wala kwa ishara.

Sasa basi ni wapi panapofahamisha ujamaa. Ujamaa ni siasa ya kiuchumi ambayo, kabla ya chochote, huangalia nyenzo za uzalishaji, kama ardhi nk, na kuweko viwango vya kumiliki; kisha huangalia uzalishaji wenyewe na njia za kukua kwake na mgawanyo wake. Hili ni jambo jingine na kuhimiza matajiri kutoa ni jambo jingine.

Kwa hiyo inatubainikia kuwa kauli ya mwenye kusema kuwa Abu Dhar alikuwa mjamaa kwa vile aliwakaripia matajiri kwa Aya hii, kuwa ni makosa na kuchanganyikiwa. Abu Dhar hana habari na ujamaa wala kitu chochote isipokuwa Uislamu. Mfano wake katika hilo ni mfano wa Mwislamu yeyote. Lakini yeye alikuwa mwenye Ikhlasi na dini yake, aliufanyia ikhlasi Uislamu na kutupilia mbali tamaa na malengo mengine.

Ikhlasi yake hii ndiyo iliyomfanya awapinge Maquraish na kuwatusi waungu wao siku aliposilimu, pale aliposimama kwenye Al-Kaaba akinadi kwa sauti kubwa: Hapana Mola mwingine ispokuwa Mwenyezi Mungu. Akikinadi tamko la Uislamu juu ya vichwa vya Maquraish siku waislamu walipokuwa hawana nguvu wala uwezo na hakuna aliye kuwa akithubutu kutamka jina la Mwenyezi Mungu na Mohammad isipokuwa kwa kujificha.

Aliendelea kuwa na msimamo huu hata mbele ya Uthman na Muawiya. Kama ambavyo alipata mapigo ya kuumiza kutoka kwa washirikina, pia kwa Uthman alipata pigo la kufukuzwa na kuwekwa mbali na watu, lakini halikumkasirisha kwa sababu yeye hakukasirikia katika maisha yake yote isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Kwa ufupi alilofanya Abu Dhar ni kuwataka viongozi watawale kwa uadilifu na kuchunga haki pia aliwahofisha na adhabu kali na kuwahimiza wanaodhulumiwa kuwapinga madhalimu na kurudisha haki zao kutoka kwa madhalimu hao.
Sasa wapi na wapi hayo na Ujamaa? Tumezungumzia kuhusu kunasibish- wa ujamaa kwa Abudhar katika Kitab Maashiah Al-Imamia kwenye kifungu ‘Je Abudhar ni mjamaa?’ Na katika Kitabu Ma’ulamainnajaf Al-Ashraf kwenye kifungu ‘Abudharr’.

إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِنْدَ اللَّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنْفُسَكُمْ ۚ وَقَاتِلُوا الْمُشْرِكِينَ كَافَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَافَّةً ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ {36}

Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu (tangu) siku alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na washirikina nyote, kama wanavyopigana nanyi wote, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.

إِنَّمَا النَّسِيءُ زِيَادَةٌ فِي الْكُفْرِ ۖ يُضَلُّ بِهِ الَّذِينَ كَفَرُوا يُحِلُّونَهُ عَامًا وَيُحَرِّمُونَهُ عَامًا لِيُوَاطِئُوا عِدَّةَ مَا حَرَّمَ اللَّهُ فَيُحِلُّوا مَا حَرَّمَ اللَّهُ ۚ زُيِّنَ لَهُمْ سُوءُ أَعْمَالِهِمْ ۗ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ {37}

Hakika kuahirisha ni kuzidi katika kufru, kwa hayo hupotezwa wale walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuuharamisha mwaka Ili wafanye sawa idadi ya ile aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu, hivyo huhalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao. Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.
  • 1. Angalia Kitabu Voltaire cha Gustave Lanson