read

Aya 36 – 37: Idadi Ya Miezi

Miezi Miandamo Ndiyo Miezi Ya Kimaumbile

Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu (tangu) siku alipoumba mbingu na ardhi.

Makusudio ya kwa Mwenyezi Mungu na katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kwamba miezi kumi na mbili iko kihakika katika ulimwengu wa kimaumbile, sawa na mbingu na ardhi si katika ulimwengu wa mazingatio na sharia, kama vile halali na haramu.

Makusudio ya siku alipoumba mbingu na ardhi ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu aliumba ulimwengu kwenye hali ambayo idadi ya miezi ni kumi na mbili, tangu siku ya kwanza ya kupatikana mbingu na ardhi; yaani idadi ya miezi hii, sio kwamba imewekwa na binadamu na ugunduzi wake; isipokuwa ni desturi na nidhamu ya maumbile.

Haya ndiyo maana ya Aya. Kimsingi ni kwamba binadamu hupima wakati na kuupanga kwa anavyoona na kuhisi. Tukiangalia maumbile ambayo yatatuongoza katika kujua wakati, hatupati zaidi ya jua na mwezi. Jua kila siku linakwenda kwa mfumo mmoja kutoka mashariki na kutua magharibi, bila ya kuweko tofauti.

Kupitia hilo jua twajua wakati wa asubuhi mchana na jioni, na wala halihusiki na kujua mwezi si kwa karibu wala mbali. Lakini mwezi ni kinyume na hivyo. nHuwa unajitokeza kwa picha maalum kuanzia siku ya kwanza, ya kila mwezi, ambao ndiyo siku ya kwanza ya mwezi. Tunapojua mwezi ndio tunajua mwaka.

Na kwa ajili hii ndipo ikawa miezi miandamano, ndiyo miezi inayo kwenda na maumbile, kinyume cha miezi mingine, na kwa ajili hii ndio Mwenyezi Mungu ameiwekea wakati wa Hijja, Swaumu eda ya watalikiwa na kunyonyesha, kama ambavyo wakati wa swala amuweka kwa jua, kwa vile ndio njia ya kujua mafungu ya siku. Kwa maneno mengine, jua ni la kujua saa na mwezi mwandomo ni wa kujua miezi. Binadamu alikuwa akihisabu muda wake kwa misingi hii.

Anasema Razi: Desturi ya Waarabu tangu zamani ni kuwa na mwaka wa mwezi na sio wa jua Hukumu hii walirithi kutoka kwa Ibrahim na Ismail”

Katika baadhi ya tafsir imeelezwa kuwa hekima ya kujaaliwa Hijja na Swaumu katika miezi miandamo ni kuwa izunguke katika vipindi vyote vya mwaka; mara inakuwa nzito na mara nyingine inakuwa sahali1. Lakini jitihadi hii haitegemei asili yoyote, hata hivyo haina kizuizi kwani haikukusudiwa kuthibitisha hukumu ya sharia, isipokuwa kubainisha masilahi ya hukumu yenye kuthibiti kisharia.

Katika hiyo iko mine mitakatifu.

Mitatu katika miezi mine hii, inafuatana: Dhul-qaada, Dhul-hajj na Muharram2. Na mwezi mmoja, Rajab, uko peke. Imeitwa mitakatifu kwa kukatazwa kupigana katika miezi hiyo wakati wa jahiliya na wa Uislamu. Hayo tumeyaeleza zaidi ya mara moja.

Hiyo ndiyo dini iliyo sawa.

Yaani kugawa miezi kwa idadi ya kumi na mbili kwa hisabu ya mwezi mwandamo ndio magawanyo sahihi wala haijuzu kufanya upotofu kwa hawa na matakwa mengine katika miezi hiyo wala katika miezi mitakatifu.

Basi msidhulumu nafsi zenu humo.

Kwa kuhalalisha kupigana katika miezi mitakatifu, au kufanyiana uadui katika wakati wowote. Kila anayemwasi Mwenyezi Mungu katika dhambi kubwa na ndogo, basi ameidhulumu nafsi yake kwa kujiingiza kwenye adhabu ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu yake.

Na piganeni na washirikina nyote, kama wanavyopigana nanyi wote.

Hii ndiyo dawa; watu wote jihadi, ni desturi ya Mwenyezi Mungu na huwezi kupata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. Ama vikao vya kutatua ugomvi ni kumyenyekea adui na kusalimu amri kwake. Wazayuni wote na wakoloni wamejitokeza kuwapiga waarabu na waislamu wote; wakaweka kambi ya kiadui katika ardhi ya waarabu, na kuipa jina ‘Taifa la Israil’, ili wapitishie mashambulizi yao kutokea hapo!

Hivi tuko katika mwezi Novemba 1968, katika umoja wa mataifa, inaendelea mipango ya kutafuta suluhisho la kudumu kutatua tatizo la mashariki ya kati kwa njia ya mazungumzo ambapo adui anatoa masharti, kila anapopata fursa, ambayo yanamzidisha mori wa uadui na kupata yote ayatakayo, kisha arudie tena mazungumzo. Mambo yatakuwa hivyo hivyo mpaka atawale sehemu zote.

Dawa pekee ya kuondoa mzizi wa fitina ni ile aliyoipanga Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:

Na piganeni na washirikina nyote, kama wanavyopigana nanyi wote, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye takua.

Ambao wamejikomboa na chuki na tamaa na kuungana pamoja wote kwa ajili ya kupigana na adui wao na adui wa Mwenyezi Mungu na wa utu.

Hakika kuahirisha ni kuzidi katika kufru, kwa hayo hupotezwa wale walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuuharamisha mwaka mwingine.

Washirikina walikuwa wakiahirisha utukufu wa mwezi, kama vile Muharram, mpaka mwezi mwingine, kama vile Safar.

Ikiwa ni masilahi yao kupigana katika mwezi mtukufu basi hupigana bila ya kujali, lakini wanautukuza mwezi mwingine badala yake, katika miezi ya halali, ili ipatikane miezi mitukufu minne ya mwaka.

Ili wafanye sawa idadi ya ile aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu, hivyo huhalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu.

Tafsiri wazi zaidi kuhusu hii ni yale yaliyonukuliwa kutoka kwa Ibn Abbas aliposema: “Hakika wao hawakuhalalisha mwezi katika miezi mitakatifu ila huharamisha mahali pake mwezi wa halali. Na hawakuharamisha mwezi katika miezi ya halalali ila huhalalisha mahali pake mwezi mtakatifu. Wanafanya hivyo ili idadi ya miezi mitukufu iwe minne kwa kufuata aliyoyataja Mwenyezi Mungu.” Haya ndiyo makusudio ya kufanya sawa.

Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao.

Matamanio na malengo mengine ndiyo yanayompofusha mtu na ubaya wa amali yake. Anaiona shari kuwa ni heri na uzuri kuwa mbaya.

Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.

Yaani anawaacha kama walivyo baada ya kukata tamaa na kuongoka kwako. Angalia Juz. 5 (4:88)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَا لَكُمْ إِذَا قِيلَ لَكُمُ انْفِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ اثَّاقَلْتُمْ إِلَى الْأَرْضِ ۚ أَرَضِيتُمْ بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا مِنَ الْآخِرَةِ ۚ فَمَا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا قَلِيلٌ {38}

Enyi mlioamnini! Mna nini mnapoambiwa nendeni katika njia ya Mwenyezi Mungu mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na Akhera ni kidogo tu.

إِلَّا تَنْفِرُوا يُعَذِّبْكُمْ عَذَابًا أَلِيمًا وَيَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ وَلَا تَضُرُّوهُ شَيْئًا ۗ وَاللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ {39}

Kama hamwendi atawaadhibu kwa adhabu iumizayo na atawaleta watu wengine badala yenu, wala hamtamdhuru chochote Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu.

إِلَّا تَنْصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّهَ مَعَنَا ۖ فَأَنْزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ اللَّهِ هِيَ الْعُلْيَا ۗ وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {40}

Kama hamtamsaidia, basi Mwenyezi Mungu alimsaidia walipomtoa wale waliokufuru Alipokuwa wa pili katika wawili alipomwambia sahibu yake: Usihuzunike hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona. Na akalifanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.
  • 1. Usahali huu na uzito wake, pengine sisi tulio karibu au kwenye msitari wa ikweta (equator) hatuwezi kuhisi sana, lakini katika nchi nyingine tofauti ya usiku na mchana ni kubwa sana, lau isingefuatwa kalenda ya mwezi mwandamo, basi nchi nyingine zingekuwa na usahali daima wa ibada, kama swaumu nk, na nyingine ugumu daima -Mtarjumu
  • 2. Mafunguo pili, mfunguo tatu na mfunguo nne.