read

Aya 38 – 40: Mnanini Mnapoambiwa

Vita Vya Tabuk

Aya hizi ziko karibu na mwisho wa sura iliyoshuka katika vita vya Tabuk. Kwa ufupi ni kuwa Roma ilikuwa ikimiliki Sham iliyopakana na Bara Arabu. Walisikia nguvu ya Uislamu na kukua kwake. Hercules, mfalme wa Roma, aliwahofia waislamu akasema: “Nikiwaacha mpaka wanikabili basi dola yangu haitakuweko mashariki.” Akaazimia kuanza vita.

Mtume (saw) naye kwa upande wake akaona asingoje mpaka ajiwe na Hercules na jeshi lake Madina. Akawataka watu watoke wakapigane na Waroma. Wakati huo joto lilikuwa kali sana.
Wanafiki wakapata fursa na kuwahofisha waislamu kwa umbali wa safari, joto kali na wingi wa adui. Wakaitikia mwito wao wale wadhaifu wa imani; wakatoa udhuru na kutafuta sababu, lakini Mtume akatangaza jihadi na kwamba watu wote. Hakutoa ruhusa kwa yoyote isipokuwa mgonjwa na asiye na cha kutoa Pamoja na njama za wanafiki, lakini walijotokeza wapiganaji kiasi elfu thelathini.

Kabla ya Mtume (saw) kutoka na jeshi lake alimweka Ali bin Abu Talib kuwa kaimu wake kwa watu wake na familia yake. Muslim katika sahih yake, Sahih Muslim J2 uk 108 chapa ya mwaka 1348 A.H, anasema: “Ali akamwambia mtume: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu unaniacha nyuma na wanawake na watoto? Mtume (saw) akasema: Je, huridhiii kuwa wewe kwangu mimi ni daraja ya Harun na Musa; isipokuwa hakuna Mtume baada yangu?

Jeshi la Waislamu likaosonga; wote wakawa wako jangwani kwenye mvuke unachoma nyuso na mili. Njiani walimkuta sahaba mtukufu Abu Dhar akitembea kwa miguu kwa vile hakuwa na cha kupanda; wakati ambapo kiongozi wa wanafiki Abdallah bin Ubayya alijitoa na sehemu ya jeshi wakarudi Madina. Wanawake wakawapokea kwa kuwazoma na kuwarushia michanga nyusoni.

Baada ya mwendo wa siku saba, jeshi la waislamu likafika mpakani mwa dola ya Roma. Mkuu wa mji akataka suluhu na Mtume (saw) kuwa atoe jiziya. Mtume akakubali. Akaendelea mbele na jeshi lake mpaka akafika katika mji wa Tabuk ulioko kati kati ya njia baina ya Damascus na Madina. Wakati huo ilikuwa ni mwezi wa Rajab mwaka wa 9 A.H.

Ikatokea kuwa kiongozi wa Tabuk ametoka nje kwenda kuwinda. Waislamu wakamteka na kuuchukua mji. Mtume akawa anatoka mahali fulani hadi mahali pengine mpaka akawashinda nguvu walinzi wa mpakani, akakomboa makabila ya kiarabu kutoka katika serikali ya Roma. Haya yote yalifanyika ndani ya siku ishirini.

Waislamu wakarudi Madina wakiwa na ngawira; na Mtume (saw) akatoa agizo la kuwasusia waliorudi nyuma, akazuia wasizungumze na kuamiliana na watu hata wake na watoto. Ufafanuzi zaidi utakuja katika Aya zitakazofuatia; hasa Aya 117 na 118 katika sura hii.

Maana

Enyi mlioamnini! Mna nini mnapoambiwa nendeni katika njia ya Mwenyezi Mungu mnajitia uzito katika ardhi?

Mtume (saw) alipowataka waislamu watoke kwa ajili ya vita vya Tabuk, liliwatia uzito hilo baadhi yao wakaathirika kubaki ardhini mwao na majumbani mwao.

Ilikuwa ni desturi ya Mtume (saw), anapotoka kwa ajil ya vita, kuwapa dhana watu kuwa anatokea jambo jingine kwa masilahi ya siri katika vita, lakini katika vita hivi alisema wazi wazi, ili watu wajue taabu zinazowangojea.

Baadhi ya wafasiri wamewatolea udhuru wale waliojitia uzito kutoka, kwamba wakati ulikuwa wa joto kali, watu wanadhiki ya chakula na mazao yamekwisha komaa tayari kwa kuvunwa.

Vyovyote iwavyo maneno kwa hali ilivyo – yanaelekezwa kwa waliojitia uzito na jihadi. Na Mwenyezi Mungu akawalaumu kwa kuwaambia:

Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na Akhera ni kidogo tu.

Je, ni sawa imani yenu na akili zenu kuathirika na neema ya dunia inayokiwisha kuliko neema ya Akhera iliyo adhimu na yenye kudumu?

Kama hamwendi atawaadhibu kwa adhabu iumizayo na atawaleta watu wengine badala yenu, wala hamtamdhuru chochote.
Yaani kama hamtaitikia mwito wa Mtume wa kutoka naye kupigana na Waroma, basi Mwenyezi Mungu atawateremshia adhabu iumizayo, enyi wanafiki mnaojitia uzito; na atamsaidia Mtume wake kwa mikono ya wengine, wala kurudi nyuma kwenu hakuwezi kumdhuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake .

Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu.

Hashindwi kuwaadhibu wala kuinusuru dini yake na Mtume wake kwa watu bora zaidi yenu.

Kama hamtamsaidia, basi Mwenyezi Mungu alimsaidia walipomtoa wale waliokufuru;

Inadokeza tukio la vitimbi na njama walizopanga makafiri wa Kiquraish, kumua Mtume (saw) akiwa amelala kitandani kwake, jinsi alivyomwokoa nao kwa kulala Ali mahali pake na alivyo hama kutoka Makka kwenda Madina baada ya Mwenyezi Mungu kumfichulia njama zao. Hayo tumeyaeleza katika kufasiri (8:30)

Alipokuwa wa pili katika wawili alipomwambia sahibu yake: Usihuzunike hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi.

Makusudio ya wa pili katika wawili na sahibu ni Abu Bakr, kwa vile yeye alikuwa pamoja na Mtume katika kuhama kwake na walijificha pamoja katika pango Thawr. Razi anasema: “Washirikina walipofuata nyayo na kukurubia pango, Abu Bakr alilia akimhofia Mtume (saw). Mtume (saw) akamwambia usihuzunike, hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi. Abu Bakr akasema: Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi. Mtume (saw) akasema ndio.

Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona.

Amesema Abu Hayan Al-Andalusi katika tafsir yake: “Amesema Ibnu Abbas: Utulivu ni rehma, na dhamir katika akateremshia inamrudia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kwa vile yeye ndiye anayezungumziwa.”

Hayo yanafikiana na kauli ya Sheikh wa Al az-har, Al Maraghi, aliposema katika tafsir yake, ninamnakuu: “Yaani akateremsha utulivu wake, unao tuliza moyo, kwa Mtume wake (saw), akampa nguvu kwa majeshi kutoka kwake ambao ni Malaika.” Vile vile yanaafikiana na mfumo wa Aya Kwa sababu dhamir katika kumsaidia na kumtoa inamrudia Mtume (saw).

Na akalifanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Neno la Mwenyezi Mungu ni Tawhid na neno la waliokufuru ni shirk na ukafiri.

Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

Hekima yake ilipitisha kumnusuru Mtume wake (saw) kwa nguvu yake na kuidhihirisha dini yake juu ya dini zote.

انْفِرُوا خِفَافًا وَثِقَالًا وَجَاهِدُوا بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنْفُسِكُمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ {41}

Nendeni mkiwa wepesi na wazito, na mpiganie jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu. Hilo ni kheri kwenu mkiwa mnamjua.

لَوْ كَانَ عَرَضًا قَرِيبًا وَسَفَرًا قَاصِدًا لَاتَّبَعُوكَ وَلَٰكِنْ بَعُدَتْ عَلَيْهِمُ الشُّقَّةُ ۚ وَسَيَحْلِفُونَ بِاللَّهِ لَوِ اسْتَطَعْنَا لَخَرَجْنَا مَعَكُمْ يُهْلِكُونَ أَنْفُسَهُمْ وَاللَّهُ يَعْلَمُ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ {42}

Lau ingekuwa ni faida iliyo karibu na safari nyepesi wangelikufuata. Lakini imekuwa ndefu kwao yenye mashaka . Na wataapa kwa Mwenyezi Mungu lau tungeliweza bila shaka tungelitoka pamoja nanyi. Wanaziangamiza nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika hao ni waongo.

عَفَا اللَّهُ عَنْكَ لِمَ أَذِنْتَ لَهُمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكَ الَّذِينَ صَدَقُوا وَتَعْلَمَ الْكَاذِبِينَ {43}

Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini umewapa ruhusa kabla ya kubainika kwako wanaosema kweli na ukawajua waongo.