read

Aya 41-43: Nendeni Mkiwa Wazito Na Mkiwa Wepesi.

Kwenda Wote

Nendeni mkiwa wepesi na wazito, na mpiganie jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu.

Makusudio ya wepesi nikwenda kupigana jihadi kwa wepesi, na uzito ni kupigana kwa mashaka. Aya inafahamisha wajibu wa kutoka wote. Ufuatao ni ubainifu:

Adui akijaribu kuichokoza dini ya Kiislam kwa kukipotoa kitabu cha Mwenyezi Mungu na yaliyothibiti katika sunna ya Mtume wake, au kuwazuiya waislamu kutekeleza wajibu wao na nembo za kidini; akijaribu kutawala mji katika miji yao, basi hapo itakuwa ni wajibu kwa waislam kumpiga jihadi adui huyu na kuzuia upotevu wake.

Ikiwa baadhi wanaweza kumzuia, basi wajibu utakuwa ni kutosheana (kifaya) kwa maana kuwa wakitekeleza baadhi, basi jukumu litawaondokea wote, na wakipuza wote, basi jukumu ni lao wote na watastahiki adhabu wote.

Na kama haiwezekani ila kwa watu wote, basi itakuwa ni lazima kwa vijana, wazee, wanawake, vilema, vipofu na hata wagonjwa, kadiri mtu atakavyoweza.

Mwenye Jawahir anasema!” Adui akishambulia waislamu na kuhofiwa kuutia doa Uislamu au kafiri akitaka kutawala miji ya waislamu na kuwateka na kuchukua mali zao, basi ni wajibu kupigana kwa mungwana, mtumwa, mwana mume, mwanamke, mzima, mgonjwa, kipofu, mlemavu na wengineo; iwapo kuna haja ya kufanya hivyo.

Wala lilo halitahitajia kuweko Imam wala idhini yake; na wala halitahusika na wale waliochokozwa tu, bali ni wajibu kwa kila atakayelijua hilo, hata kama hakuchokozwa. Kama hakujua kuwa waliochokozwa wanaweza kumkabili adui.”

Hii ni ahadi aliyoichukua Mwenyezi Mungu kwa kila mwislamu kwa maafikiano ya madhehebu yote; sawa na walivyoafikiana juu ya wajibu wa Swaum, Swala, Hijja na Zaka.

Waislamu na waarabu hivi sasa wamejaribiwa kwa uchokozi wa Uzayuni wa kikoloni juu ya dini yao na miji yao. Wameuliwa wamefukuzwa na wakafungwa kwa maelefu. Kwa hiyo ni juu ya kila Mwarabu na Mwislamu popote alipo, Mashariki au Magharibi apigane kwa nguvu zake zote dhidi ya genge hili linalojiita dola ya Israil.

Hilo ni kheri kwenu

Yaani hilo la kutoka ni kheri kwa waislamu katika dini yao na dunia yao.

Mkiwa mnamjua

Ndio sisi tunajua kwamba kutoka kuwapiga jihadi waisrail ni wajibu kwa kila Mwislamu, lakini linalotuzuia kuwapiga jihadi waisrail ni viongozi wahaini. Kwa hiyo basi ni wajibu kuwapiga jihadi hawa kabla ya chochote. Kwa sababu wao ndio sababu ya sababu; lau si hiyana yao kwa dini yao, uma wao na kuwatii kwao wazayuni na ukoloni, basi Israil isigekuwako kabisa.

Lau ingekuwa ni faida iliyo karibu na safari nyepesi wangelikufuata.
Dhamiri ya wangekufuata inawarudia walio rudi nyuma katika vita vya Tabuk. Faida ya karibu ni ngawira baridi. Maana ni kuwa Ewe Muhammad! lau ungeliwaita kwenye manufaa ya haraka wangelikuitikia haraka haraka.

Lakini imekuwa ndefu kwao yenye mashaka.

Safari ya Sham kupitia jangwani kwenye vumbi la upepo na joto kali na adui Mrumi ndiye mwenye nguvu wakati huo, vipi watakuitikia?

Sifa hizi hazihusiki na wale waliorudi nyuma katika vita vya Tabuk tu, bali nafsi hupendelea raha na manufaa. Lakini watu wa imani wanaojiridhia kwa takua, wanaona chepesi kila kitu anachokiridhia Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Imam Ali (as) anasema: “Amali bora ni ile inayokirihisha nafsi yako.”

Yametangulia maelezo yanayoambatana na hayo katika Juz.5 (4:37)

Na wataapa kwa Mwenyezi Mungu lau tungeliweza bila shaka tungelitoka pamoja nanyi.

Hii ni habari kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kwamba wanafiki waliorudi nyuma ya vita vya Tabuk, wamemwandalia viapo na nyudhuru za uwongo atakaporudi. Kimsingi ni kwamba sifa ya uongo haiepukani na mnafiki; kama si hivyo basi asingelikuwa mnafiki.

Wanaziangamiza nafsi zao

Kwa vile wao wameiangamiza dini yao kwa uwongo na unafiki.

Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika hao ni waongo katika nyudhuru zao na viapo vyao.

Inasemekana kuwa hasemi uwongo isipokuwa mwoga, nasi tunaogozea kuwa anayeangamizwa na tamaa pia ni mwoga.

Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini umewapa ruhusa kabla ya kubainika kwako wanaosema kweli na ukawajua waongo.

Mtume (saw) alipotoa mwito wa kwenda kwenye Jihadi, baadhi walimwomba ruhusa ya kutokwenda, wakatoa sababu kadhaa. Mtume akawakubalia kabla ya kujua ukweli wao na uwongo wao katika nyudhuru. Ndipo Mwenyezi Mungu (swt) akamlaumu kwa hilo, akamwambia, ingekuwa vizuri kungoja kuwapa ruhusa mpaka ikufunukie hakika yao.

Hayo ndiyo yanayofahamika kutokana na dhahiri ya Aya Utaweza kuuliza kuwa Mtume (saw) ni Maasumu, na kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Amekusamehe’ inaonyesha kuweko kosa (dhambi), pia kauli yake Mwenyezi Mungu ‘kwa nini umewapa ruhusa.’

Jibu: Msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu haulazimishi kuweko dhambi. Mara nyingi inakuwa ni ibara ya thawabu yake na rehema yake. Mitume wote walikuwa wakiomba msamaha kwake Mwenyezi Mungu. Ama kusema “Kwa nini”, hilo ni jambo jepesi ambapo inasihi katika mambo ya halali na mengineyo. Unaweza kumwambia sahibu yako; kwa nini umefanya hivi? Bila ya kuona kuwa amefanya jambo baya, isipokuwa unakusudia angefanya jingine.

Lengo la lawama hapa inayotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake, ni kubainisha uwongo wa wanafiki katika nyudhuru zao, na kwamba hilo lilikuwa ni kukimbia jihadi tu. Mfumo huu ni fasaha zaidi katika kukanusha udhuru kuliko mifumo yote. Zaidi ya hayo Mwenyezi Mungu amesema katika Aya 117 ya Sura hii: “Mwenyezi Mungu amekubalia toba wahajir na answar waliomfuata katika saa ya dhiki Ikiwa toba haifahamishi kuweko dhambi, basi msamaha na kuuliza kwa nini, ndiko kusikofahamisha zaidi dhambi.

لَا يَسْتَأْذِنُكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ أَنْ يُجَاهِدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِالْمُتَّقِينَ {44}

Hawakuombi ruhusa ambao wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ya kuacha kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua wenye takua.

إِنَّمَا يَسْتَأْذِنُكَ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَارْتَابَتْ قُلُوبُهُمْ فَهُمْ فِي رَيْبِهِمْ يَتَرَدَّدُونَ {45}

Hakika wanaokuomba ruhusa ni wale tu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Na nyoyo zao zikatia shaka, kwa hiyo wanasitasita katika shaka yao.

وَلَوْ أَرَادُوا الْخُرُوجَ لَأَعَدُّوا لَهُ عُدَّةً وَلَٰكِنْ كَرِهَ اللَّهُ انْبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ وَقِيلَ اقْعُدُوا مَعَ الْقَاعِدِينَ {46}

Lau wangelitaka kutoka bila shaka wangeliandalia maandilio. Lakini Mwenyezi Mungu alichukia kutoka kwao, kwa hiyo akawazuia Na ikasemwa: Kaeni pamoja na wakaao.

لَوْ خَرَجُوا فِيكُمْ مَا زَادُوكُمْ إِلَّا خَبَالًا وَلَأَوْضَعُوا خِلَالَكُمْ يَبْغُونَكُمُ الْفِتْنَةَ وَفِيكُمْ سَمَّاعُونَ لَهُمْ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ {47}

Lau wangelitoka pamoja nanyi wasingeliwazidisha ila mchafuko na wangelikwenda huku na huko kati yenu kuwatakia fitina. Na miongoni mwenu wako wanawaosikiliza. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu.

لَقَدِ ابْتَغَوُا الْفِتْنَةَ مِنْ قَبْلُ وَقَلَّبُوا لَكَ الْأُمُورَ حَتَّىٰ جَاءَ الْحَقُّ وَظَهَرَ أَمْرُ اللَّهِ وَهُمْ كَارِهُونَ {48}

Walikwishataka fitina tangu zamani na wakakupindulia mambo. Mpaka ikaja haki na ikadhihiri amri ya Mwenyezi Mungu na wao wamechukia.