read

Aya 41: Khums

Lugha

Neno Ghanima kwa lugha ya kiarabu lina maana ya kupata kitu. Wametofautiana kuhusu maana ya Fay-u kwa kauli mbili : Kwanza kuwa ni ghanima, pili kuwa ni mali inayochukuliwa bila ya vita.

Ama kuhusu Nafal yametangulia maelezo yake mwanzo wa Sura hii. Makusudio ya jamaa ni jamaa za Mtume. Yatima ni yule aliyefiwa na baba yake kabla ya kubaleghe. Na Khums ni humusi (sehemu moja ya tano).

Maana

Na jueni kwamba chochote mlichopata ghanima, basi khumsi yake ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri.

Wafasiri wamefanya utafiti katika pande nyingi kuhusu Aya hii. Ama sisi tutatosheka na pande mbili tu: Kwanza, dhahiri ya Aya inafahamisha pande hizo mbili. Pili, kwamba upande mwingine hautumiki. Katika pande hizo mbili tutakazozitaja ni kueleza maana ya neno ghanima na kubainisha wale wanaostahiki Khumsi.

Wametofautiana Sunni na Shia kuhusu makusudio ya neno ghanima katika Aya. Sunni wamesema ni ngawira wanayoiteka waislamu kutoka kwa makafiri kwa vita.

Kulingana na kauli yao hii, suala la Khums linakuwa kwao halipo siku hizi; sawa na suala utumwa. Kwa vile hakuna dola ya kiislamu inayopigana jihadi na makafiri na washirikina hivi sasa.

Shia wamesema kuwa ghanima ni zaidi ya ngawira ya vita inayochukuliwa na Waislamu kutoka kwa makafiri, na kwamba inakusanya madini; kama vile mafuta ya petroli, dhahabu nk. Vile vile dafina ikiwa haijulikani mwenyewe na wanavyovitoa watu kutoka baharini kwa kuzamia; kama vile lulu.

Nyingine ni mali inayozidi gharama za mtu yeye na watoto wake katika chumo la mwaka, mali ya halali iliyochanganyika na ya haramu na haijulikani kiwango cha haramu.

Pia ghanima ni ardhi aliyoinunua kafir dhimmi kutoka kwa Mwislamu. Ufafanuzi uko kwenye vitabu vya Fiqh, kikiwemo Fiqh Imam Jaffer As Sadiq Juz.2. Kulingana na kauli ya Shia suala ya khums linakuwa bado lipo.

Kama walivyotofautiana katika maana ya ghanima, vile vile wametofau- tiana katika idadi ya mafungu ya khums na wanaostahiki.

Shia wamesema: khums hugawanywa mafungu mawili: La kwanza litagawanywa mafungu matatu: Fungu la Mwenyezi Mungu, la Mtume wake na la jamaa. Lile la Mweneyzi Mungu ni la Mtume na la Mtume ni la jamaa zake.

Na msimamizi wa jamaa baada ya Mtume ni Imam anayesimamia kazi za Mtume. Akiweko atapewa yeye; kama hayuko basi ni wajibu kulitoa fungu hilo katika maslahi ya kidini, ambayo muhimu zake ni kuutangaza Uislamu na kazi ya kuusambaza na kuutukuza.

Ama fungu la pili, nalo lina sehemu ya mayatima wa ukoo wa Muhammad (saw), masikini wao na wasafiri wao. Wanaohusika katika fungu hilo ni ukoo wa Muhammad (saw) tu peke yao. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawaharamishia sadaka akawawekea Khums.

Tabari katika tafsir yake na Abu Hayan Al-Andalus katika Bahrul-Muhit wanasema: “Amesema Ali bin Abu Talib (as): Mayatima na maskini ni mayatima wetu. Anaongeza Tabari: “Ali bin Hussein (ra) alimwambia mtu mmoja kutoka Sham: Je, hukusoma katika Sura Anfal: “Na jueni kwamba chochote mlichopata ghanima, basi hakika khums yake ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri.

Akasema yule mtu, “Naam! Kwani ndiyo nyinyi? Akasema ndiyo.” Ama wasemavyo Sunni, tuwaachie maulamaa wawili wakubwa, mmoja wao ni wa zamani, Razi, na mwingine ni wa hivi karibuni, Maraghi, mmoja wa Masheikh wa Az-har na rais wake wakati wake.

Razi anasema: “Kauli zilizo mashuhuri ni kwamba hiyo humusi ni sehemu tano:

1. Mtume wa Mwenyezi Mungu.

2. Jamaa zake katika Bani Hashim, na Bani Muttwalib, sio Bani Abdu Shams (Umayya) na Bani Naufal.

3. Mayatima.

4. Masikini.

5. Wasafiri.

“Hiyo ni katika uhai wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ama baada ya kufa kwake (saw), kwa upande wa Shafii sehemu ni tano.

Ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, inatolewa kwenye maslahi ya Waislamu, ya jamaa matajiri na makufara, ilyobaki ni ya mayatima, maskini na wasafiri.

Abu Hanifa anasema kuwa sehemu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu inaondoka baada ya kufa kwake kwa saba Na hugawanywa Khums kwa mayatima, maskini na wasafiri. Malik naye anasema: “Mambo ya khums huachiwa rai ya Imam.”

Sheikh Maraghi anasema: “Amepokea Bukhari kutoka kwa Mut’im bin Jubair wa Bani Nawfal, kwamba yeye alikwenda na Uthman bin Affan wa Bani Abd Shams kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akawaambia : “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Umewapa Bani Muttalib na ukatuacha na hali sisi na wao ni daraja moja. Akasema Mtume (saw): Hakika Bani Muttalib na Bani Hashim ni kitu kimoja.”

Sheikh Maraghi anaongezea juu ya Hadith hii kwa kusema, na siri ya hilo ni kwamba Makuraish walipoandika maazimio yao ya kuwatoa Bani Hashim Makka na kuwazuia katika Shii’b waliingia humo pamoja na Bani Muttalib, na wala hawakuingia Bani Abu Shams wala Bani Nawfal kwa uadui waliokuwa nao na Bani Hashim wakati wa Jahaliyya na wakati wa Uislamu.

Akawa Abu Sufyan anapigana na Mtume (saw) na kuungana na washirikina na watu wa Kitab dhidi yake, mpaka Mwenyezi Mungu alipompa ushindi Mtume wake na Waarabu wakaingia kwenye dini kwa ushindi wa Makka. Vile vile baada ya Uislamu Muawiya alimtokea Ali na akapigana naye.

Nasi tunaungia maneno ya Sheikh Maraghi kuwa vile vile Yazid mjukuu wa Abu Sufyan alimuuwa Hussein Bin Ali, mjukuu wa Mtume (saw). Mshairi anasema kuhusu uadui huu wa kurithiana baba na babu.

Bin Harb na Mustwafa, Aliy na mwana wa Hind, Husein hawakumfaa, alipambana na Yazid

Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu na tuliyoteremsha kwa mja wetu siku ya upambanuzi, siku yalipokutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu.

Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya siku ya upambanuzi na siku yalipokutana majeshi mawili ni siku ya Badr. Kwa sababu Mwenyezi Mungu alifarikisha baina ya ukafiri na imani kwa kuuweka Uislamu juu ya shirk. Vile vile ni siku yalipokutana majeshi mawili, la waumini na la washirikina ambapo jeshi la washirikina waliipata.

Maana ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) hakubali kumwamini yeye, vitabu vyake na Mitume yake kama nadharia tu, bila ya vitendo, isipokuwa anakubali imani ya anayehukumu na kufanya amali kwa anavyohukumu Mwenyezi Mungu.

Razi anasema: “Kauli yake Mwenyezi Mungu: Mkiwa mmemwamini Mwenyezi Mungu, inafahamisha kuwa ikiwa haukupatikana ugavi huu, kama alivyohukumu Mwenyezi Mungu, basi imani nayo haipo.”

Nasi tunaongezea juu ya kauli ya Razi kuwa vile vile ikiwa hukumu haikupatikana katika usiokuwa ugavi huu, kama alivyohukumu Mwenyezi Mungu, basi imani nayo haitapatikana. Kwa vile, sababu inayowajibisha ukafiri ni moja nayo ni kuhalifu hukumu ya Mwenyezi Mungu makusudi. Kimisingi ni kwamba sababu hii haikubali kufungwa wala kuhusishwa na jambo moja tu.
Tumeeleza mara nyingi kwamba makusudio ya ukafiri katika mfano huu ni ukafiri wa kimatendo, yaani ufasiki sio ukafiri wa kiitikadi.

إِذْ أَنْتُمْ بِالْعُدْوَةِ الدُّنْيَا وَهُمْ بِالْعُدْوَةِ الْقُصْوَىٰ وَالرَّكْبُ أَسْفَلَ مِنْكُمْ ۚ وَلَوْ تَوَاعَدْتُمْ لَاخْتَلَفْتُمْ فِي الْمِيعَادِ ۙ وَلَٰكِنْ لِيَقْضِيَ اللَّهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا لِيَهْلِكَ مَنْ هَلَكَ عَنْ بَيِّنَةٍ وَيَحْيَىٰ مَنْ حَيَّ عَنْ بَيِّنَةٍ ۗ وَإِنَّ اللَّهَ لَسَمِيعٌ عَلِيمٌ {42}

Mlipokuwa kando ya bonde lililo karibu, nao wako kando ya bonde lililo mbali; na msafara upo chini yenu. Na lau mngeliagana mngelihitalifiana katika miadi. Lakini ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike Ili aangamie wa kuangamia kwa dalili dhahiri na awe hai wa kuwa hai kwa dalili dhahiri. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.

إِذْ يُرِيكَهُمُ اللَّهُ فِي مَنَامِكَ قَلِيلًا ۖ وَلَوْ أَرَاكَهُمْ كَثِيرًا لَفَشِلْتُمْ وَلَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ سَلَّمَ ۗ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ {43}

Alipokuonyesha katika usingizi wako kuwa ni wachache. Na lau angelikuonyesha kuwa ni wengi mngelivunjika moyo na mngelizozana katika jambo hilo, lakini Mwenyezi Mungu alilinda. Hakika yeye ni mjuzi wa yalimo vifuani.

وَإِذْ يُرِيكُمُوهُمْ إِذِ الْتَقَيْتُمْ فِي أَعْيُنِكُمْ قَلِيلًا وَيُقَلِّلُكُمْ فِي أَعْيُنِهِمْ لِيَقْضِيَ اللَّهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا ۗ وَإِلَى اللَّهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ {44}

Na alipowaonyesha machoni mwenu mlipokutana kuwa ni wachache Na akawafanya nyinyi kuwa wachache machoni mwao ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.