read

Aya 42 – 44: Mlipokuwa Kando Ya Bonde Lililokaribu

Maana

Aya hizi zinaonyesha baadhi ya sababu ambazo aliziandaa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ushindi wa waislamu kwa washirikina katika vita vya Badr. Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) aliwapa ilhamu waislam kujiweka mwenye bonde lililo karibu na Madina. Ama washirikina wao walikuwa upande ulio mbali zaidi na hapa; na kati ya pande mbili kulikuwa na kilima kinachotenganisha.

Kulingana na mfumo wa maneno, inaonyesha kuwa upande wa waislamu ulikuwa ndio mahali pa vita walipomkusudia adui yao. Ni katika mipango yake Mwenyezi Mungu kuliweka kila jeshi mahali pake bila ya kujuana. Kwani lau waislamu wangeliwaona maadui zao kwa macho, wangeliogopa na kukata tamaa ya kuwashinda.

Vile vile ni katika mipango yake Mwenyezi Mungu, kwamba yeye – imetukuka hekima yake – aliwafanya wachache washirikina kwenye macho ya waislam walipokutana. Yote hayo ni kwa ajili kuidhirisha dini yake juu ya dini zote, hata kama watachukia washirikina.

Pia ni katika hekima yake kuwa Abu Sufyan aupeleka msafara wa ngamia kwenye mwambao wa bahari, ili majeshi mawili, ya batili na haki, yakutane na wala waislamu wasifuate msafara tu wakaacha jeshi.

Baada ya utangulizi huu, sasa tunaingilia kufasiri Aya:

Mlipokuwa kando ya bonde lililo karibu, nao wako kando ya bonde lililo mbali.

Msemo unatoka kwa Mwenyezi Mungu kuelekezwa kwa waislamu, akiwakumbusha mahali walipokuwa - kando ya bonde lililo karibu ya Madina, na mahali walipokuwa washirikina nao ni upande wa mbali: Vile vile anawakumbusha kugeuza njia kwa msafara wa ngamia kuelekea mwambao wa bahari, ambako Mwenyezi Mungu (swt) amekuashiria kwa kauli yake:
Na msafara upo chini yenu.

Lengo la ukumbusho huu ni kwamba mambo yote yalikuwa kwa masilahi yao; kama ilivyobainika.

Na lau mngeliagana mngelihitalifiana katika miadi.

Waislamu walitoka pamoja na Mtume (saw) kufuatia msafara wa ngamia na mizigo yake, bila ya kukusudia kupigana, lakini Mwenyezi Mungu akaigeuza safari hii ya kufuatia mali kuwa ya kupigania jihadi katika njia yake.

Hilo likawa ni heri kubwa kwao. Lau kama tangu mwanzo wangelijua kuwa wanakwenda kupigana na washirikina; kisha wakajua wingi wao, basi baadhi ya waislamu wangeligeuka kwa hofu, na kutofautiana na wale watakaotaka kupigana. Matokeo yake ushindi usingelipatikana.

Lakini ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.

Yaani lakini Mwenyezi Mungu alipanga kukutana huku bila ya ahadi, ili litimie alilokukusudia la kutukuka dini na kudhalilika washirikina.

Ili aangamie wa kuangamia kwa dalili dhahiri na awe hai wa kuwa hai kwa dalili dhahiri.

Makusudio ya mwenye kuangamia ni kafiri, na mwenye kuwa hai ni yule mwenye kuamini. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwanusuru vipenzi vyake na kuwashinda nguvu maadui zake, siku ya Badr ili hilo liwe ni hoja mkataa kwa yule mwenye kupinga na hoja dhahiri kwa mwenye kuamini.

Utauliza: Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa mwenye kushindana na haki atashindwa, lakini tujuavyo, wabatilifu mara nying si wanaishinda haki?

Jibu: Mwenyezi Mungu (swt) aliwaahidi ushindi waislamu kupitia kwa Mtume wake, kabla ya vita, ingawaje walikuwa wachache na wanyonge; kama alivyosema katika Aya ya 7 ya sura hii: “Na alipowaahidi moja ya makundi mawaili kuwa ni lenu.” Mwenyezi Mungu akatekeleza ahadi hiyo, ukathibiti muujiiza wa Muhammad (saw) aliyewapa habari ya ushin- di wakati ambapo dalili zote zilionyesha ni kinyume na hivyo.

Zaidi ya hayo walisaidiwa na malaika, kama inavyofahamisha Aya ya 9 na fumba la mchanga au changarawe alilowatupia mtume (swa); kama ilivyo katika Aya ya 17. Yote haya na mengineyo yalikuwa ni muujiza wa wazi uliodhihiri mikononi mwa Muhammad, siku ya Badr. Na ndiyo makusudio ya dalili dhahiri kwa anayekufuru na dalili dhahiri kwa anayeamini; na wala sio ushindi tu.

Kwa maneno mengine ni kutoa habari ya ushindi kabla ya kutokea kwake pamoja na miujiza; na wala sio makusudio ya ushindi wenyewe.

Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.

Hakifichuki chochote katika kauli na vitendo na yanayopita nyoyoni.

Alipokuonyesha katika usingizi wako kuwa ni wachache. Na lau angelikuonyesha kuwa ni wengi mngelivunjika moyo na mngelizozana katika jambo (hilo), lakini Mwenyezi Mungu alilinda.

Huu nao ni muujiza mwingine wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Nao ni kuwa Mwenyezi Mungu (swt) alimwonyesha usingizini kwamba washirikina ni wachache tena madhaifu; na kushujaika. Lau Mwenyezi Mungu angelimuonyesha kuwa maadui wana nguvu, basi azma ya waislamu ingelidhoofika, wakawa wanyonge wa kupigana na kutofautiana. Hilo lingelifuatiwa na kushindwa. Lakini Mwenyezi Mungu alilinda tatizo hili na akawahurumia waja wake waumini.

Hakika yeye ni mjuzi wa yalimo vifuani.

Yaani anajua kuwa nyoyo za waislamu zitahisi hofu ya kupigana zikijua wingi wa adui; ndipo akiziweka mbali, Mwenyezi Mungu, hisia hizi kwa alivyoona Mtume uchache wa maadui usingizini.

Na alipowaonyesha machoni mwenu mlipokutana kuwa ni wachache ili muwe imara enyi waislamu, na muwe na ukakamavu na uthabiti katika kupigana na adui yenu.

Na akawafanya nyinyi kuwa wachache machoni mwao ili wasijiandae sana kupigana nanyi na kuchukua hadhari.

Hivyo ndiyo ilivyokuwa; hata Abu Jahl akasema: “Watu wa Muhammad ni mboga tu.” Mwisho wa dharau hii ulikuwa ni balaa na udhalili.

Matukio yamethibitisha kuwa silaha kubwa iliyo mkononi mwa adui ni kudharau na kutojiandaa vizuri.

Ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.

Wafasiri wamesema: Jumla hii imekaririka kwa vile sababu yake katika Aya ya kwanza ni kukusanyika waislamu na washirikina katika vita bila ya miadi. Ama sababu katika Aya hii imekuja kwa kufanyisha uchache kila kundi machoni mwa mwenzake.

Nasi tumetangulia kusema kuwa kukaririka katika Qur’an ni aina ya utangazaji uliofaulu.

Na kwa Mwenyezi Mungu hurejeshwa mambo yote.

Hutokea kwake na huishia kwake. Yeye ndiye mwenye kuyapanga kwa uadilifu wake na hekima yake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُوا وَاذْكُرُوا اللَّهَ كَثِيرًا لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {45}

Enyi mlioamini! Mnapokutana na jeshi, basi kazaneni, na mumkumbuke Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufaulu.

وَأَطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ ۖ وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ {46}

Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane, msije mkavunjika moyo na zikapotea nguvu zenu, na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ خَرَجُوا مِنْ دِيَارِهِمْ بَطَرًا وَرِئَاءَ النَّاسِ وَيَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۚ وَاللَّهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ {47}

Wala msiwe kama wale waliotoka majumbani mwao kwa fahari na kujionyesha kwa watu, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu: Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka wanayoyafanya.

وَإِذْ زَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ وَقَالَ لَا غَالِبَ لَكُمُ الْيَوْمَ مِنَ النَّاسِ وَإِنِّي جَارٌ لَكُمْ ۖ فَلَمَّا تَرَاءَتِ الْفِئَتَانِ نَكَصَ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ وَقَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِنْكُمْ إِنِّي أَرَىٰ مَا لَا تَرَوْنَ إِنِّي أَخَافُ اللَّهَ ۚ وَاللَّهُ شَدِيدُ الْعِقَابِ {48}

Na shetani alipowapambia vitendo vyao, na kusema: Leo hakuna wa kuwashinda na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipoonana majeshi mawili, alirudi nyuma na kusema: Mimi si pamoja nanyi, mimi naona msiyoyaona, mimi namwogopa, Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

إِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ مَرَضٌ غَرَّ هَٰؤُلَاءِ دِينُهُمْ ۗ وَمَنْ يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَإِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {49}

Waliposema wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao: Hawa imewadanganya dini yao. Na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.