read

Aya 44 – 48: Hawakuombi Ruhusa Ambao Wanawamwamini Mwenyezi Mungu

Maana

Hawakuombi ruhusa ambao wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ya kuacha kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao.

Kutakuwa na sababu gani ya kuomba ruhusa ikiwa jihadi ni wajibu. Je, mumin wa kweli anaweza kuomba ruhusa ya kuacha kuswali na kufunga na kusema lailaha illa llah, Muhammad Rasullah?

Hakika wanaokuomba ruhusa ni wale tu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Kila moja katika Aya mbili hizi inafahamisha juu ya mwenzake. Kwa sababu maana ya kuwa Mumin hakuombi ruhusa nikuwa asiyekuwa mumin hukuomba. Na maana ya asiyekuwa mumin anakuomba ruhusa ni kuwa mumin hakuombi. Mwenyezi Mungu amechanganya Aya mbili hizi kwa kusisitiza maana.

Na nyoyo zao zikatia shaka, kwa hiyo wanasitasita katika shaka yao.

Yaani kwamba wao wanajionyesha kuwa ni waislamu, lakini kumbe walivyo ni kuwa wanashaka shaka, hawasemi kuwa ni kweli au ni uwongo. Huu ndio unafiki. Kwa sababu mkweli mwenye ikhlasi hufanya vile inavyoonelea akili yake na kudhihirisha kwa watu, iwe ni shaka au yakini.

Lau wangelitaka kutoka pamoja na mtume kwenye vita vya Tabuk, bila shaka wangeliandalia maandilio ya vipando na masurufu ya njiani; nao walikuwa wakiliweza hilo.

Lakini Mwenyezi Mungu alichukia kutoka kwao, kwa sababu hawana wanalolitokea isipokuwa ufisadi na fitina; kama walivyofanya katika vita vya Hunain, wakati Abu Sufyan na walio mfano wake walipotoka na Mtume vita vilipochacha waligeuka wakakimbia na likalegea jeshi la waislamu.

Kwa hiyo akawazuia.

Mwenyezi Mungu aliwaamrisha kutoka kwa ajili ya Jihadi, lakini wao waliazimia ufisadi kwa kuleta migongano katika jeshi la wislamu; kama alivyosema katika Aya inayofuatia:

Lau wangelitoka pamoja nanyi wasingeliwazidisha ila mchafuko.

Kwa hiyo aliwazuia Mwenyezi Mungu na hili la fitina sio na jihadi, ambayo amewaaamrisha.

Na ikasemwa: Kaeni pamoja na wakaao.

Yaani kaeni pamoja na wanawake, watoto na vikongwe.

Mwenyezi Mungu hakubainisha aliyewaambia hivyo. Je, ni nafsi zao, au hali yenyewe ilivyokuwa au waliambiana wenyewe? Mwenyezi Mungu ndiye ajuae.

Unaweza kuuliza: Katika Aya 43, Mwenyezi Mungu amesema: Kwa nini umewapa ruhusa na katika Aya hii anasema: Mwenyezi Mungu hakupenda kutoka kwao. Sasa tutazichanganya vipi Aya hizi?

Jibu litaeleleweka kulingana na tuliyoyasema katika kufasiri kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Kwa nini umewaruhusu’ kwamba hiyo sio lawama na swali la kiuhakika; isipokuwa lengo ni kubainisha uwongo wa wanafiki katika nyudhuru zao.

Lau wangelitoka pamoja nanyi wasingeliwazidisha ila mchafuko na wangelikwenda huku na huko kati yenu kuwatakia fitina.

Huu ni ubainifu wa hekima ya Mwenyezi Mungu wa kutopenda kwake Mwenyezi Mungu na Mtume kutoka wanafiki pamoja na jeshi la waislam. kwamba wao wangefanya mbinu za kuwatenganisha na kuleta vurugu ndani ya jeshi. Watu wa aina hii wapo kila mahali na kila wakati. Siku hizi wanajulikana kwa jina la kikosi cha tano (Fifth Column)

Na miongoni mwenu wako wanawaosikiliza.

Nao ni wale wenye akili za juu juu ambao wanachukua maneno ya waongo ni bendera wanaofuata upepeo.

Walikwishataka fitina tangu zamani na wakakupindulia mambo.

Mwenyezi Mungu anadokeza vitimbi vyao na hadaa zao kwa Mtume kabla ya vita vya Tabuk, ikiwa ni pamoja na kukimbia Abu Sufyan katika vita vya Hunain, na kujitoa bin Ubayya pamoja na theluthi ya jeshi katika vita vya Uhud.

Mpaka ikaja haki na ikadhihiri amri ya Mwenyezi Mungu na wao wamechukia.

Kila aliyopenda Mwenyezi Mungu ni haki na kila aliyoyachukia ni batili. Mwenyezi Mungu alipenda Uislam pamoja na Mtume wake ushinde. Kwa hiyo yakatimia aliyoyataka Mwenyezi Mungu na akamwandalia sababu kwa ushindi wa kuiteka Makka, ushindi katika vita vya Hunain na Tabuk na kusafika bara Arabu kutokana na uchafu wa Mayahudi waovu.

Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Na ikadhihiri amri ya Mwenyezi Mungu’ ni kwamba ushindi huu waliushuhudia watu wote, na mpaka leo hivi hadi siku ya mwisho jina la Muhammad bin Abdullah linatajwa pamoja na la Mwenyezi Mungu kote - Mashariki mwa Ardhi na Magharibi.

وَمِنْهُمْ مَنْ يَقُولُ ائْذَنْ لِي وَلَا تَفْتِنِّي ۚ أَلَا فِي الْفِتْنَةِ سَقَطُوا ۗ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ {49}

Na miongoni mwao kuna anayesema: Niruhusu wala usinitie katika fitina. Hakika wamekwishatumbukia katika fitina. Na hakika Jahannam imewazunguka makafiri.

إِنْ تُصِبْكَ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ ۖ وَإِنْ تُصِبْكَ مُصِيبَةٌ يَقُولُوا قَدْ أَخَذْنَا أَمْرَنَا مِنْ قَبْلُ وَيَتَوَلَّوْا وَهُمْ فَرِحُونَ {50}

Ukikupata wema unawachukiza. Na ukikusibu msiba husema: Tuliangalia vizuri mambo yetu tangu mwanzo na hugeuka kwenda zo wakiwa wamefurahi.

قُلْ لَنْ يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا ۚ وَعَلَى اللَّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ {51}

Sema halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mola wetu, basi waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.

قُلْ هَلْ تَرَبَّصُونَ بِنَا إِلَّا إِحْدَى الْحُسْنَيَيْنِ ۖ وَنَحْنُ نَتَرَبَّصُ بِكُمْ أَنْ يُصِيبَكُمُ اللَّهُ بِعَذَابٍ مِنْ عِنْدِهِ أَوْ بِأَيْدِينَا ۖ فَتَرَبَّصُوا إِنَّا مَعَكُمْ مُتَرَبِّصُونَ {52}

Sema: Nyinyi hamtutazami ila moja ya mema mawili Na sisi tunawatizamia kuwa Mwenyezi Mungu awafikishie adhabu itokayo kwake au kwa mikono yetu. Basi ngojeni nasi tunangoja pamoja nanyi.