read

Aya 45 – 49: Mnapokutana Na Jeshi Kazaneni

Yanayoleta Ushindi

Enyi mlioamini! Mnapokutana na jeshi, basi kazaneni, na mumkum- buke Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufaulu.

Makusudio ya jeshi ni lile linalofanya ufisadi katika nchi. Kauli yake Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu yaani mlishinde.

Mwenyezi Mungu (swt) ametaja mambo mawili yanayoleta ushindi katika Aya hii:

La kwanza, ni uthabiti na ushupavu, aliposema; “Kazaneni.” La pili, ni ikhlas, aliposema “Mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana.” Makusudio ya kumkumbuka Mungu vitani sio dhikri ya takbira na tahalili tu; isipokuwa ni kuwe kupigana na ukakamavu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu; kwa maana ya kutoathirika vita na hali yoyote isipokuwa kwa ajili ya kuthibitika haki na kubatilika batili; kwa ajili ya kuhifadhi amani ya watu na usalama wao; na kuwapiga waovu wanaoeneza ufisadi katika nchi kwa kunyanganya na kupora huku wakileta vita na fitina ili watawale miji na riziki za waja.

Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane, msije mkavunjika moyo na kupoteza nguvu zenu, na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

Mwenyezi Mungu (swt) ametaja katika Aya iliyotangulia mambo mawili ya kuleta ushindi; na katika Aya hii anataja matatu: Kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, kujiepusha na mizozo na kusubiri (kuvumilia.) Lakini kuwa na subira ndiko kukazana. Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu: Subirini ni ibara nyingine ya kazaneni; kama ambavyo kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndiyo ikhlasi. Ama kutofautiana kwingine ni kuzuri na kwengine ni kubaya. Ufafanuzi utafuatia.

Kwa ufupi mambo yanayoleta ushindi wa hakika yaliyoelezwa katika Aya mbili ni matatu:

1. Subira na kukazana, nako ni kujitolea mhanga kwa moyo wote ili kuinusuru haki ishinde batili; kama ambavyo haki inashinda kwa kuondoka batili, vile vile haki inashinda kwa kufichuka batili na kuidhihirisha kwa watu.

Subira ni lazima katika kufika lengo lolote. Hakuna mwanafunzi, mwalimu, mgunduzi, au mfanyi biashara yeyote anayeweza kupata kitu bila ya subira (uvuumilivu) na kukazana. Kiwango cha kuvumilia kwake mashaka na uchungu ndicho kiwango cha kufaulu kwake. Na hii ndiyo siri ya kauli yake Mwenyezi Mungu.

Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ {155}

Wape habari njema wanaosubiri (2:155)

وَلَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الصَّابِرُونَ {80}

Wala hawatapewa hayo isipokuwa wanaosubiri.” (28:80);

وَلَئِنْ صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِلصَّابِرِينَ {126}

“Na kama mkivumilia hiyo ni kheri kwa wanaosubiri” (16:126) na Aya nyinginezo.

Mimi nimejaribu kuwa na subira nilipokuwa mwanafunzi na mtunzi. Sikuona kitu chenye mwisho mtamu na manufaa kama hicho. Tumezungumzia kuhusu kuwa na subira na uvimilivu katika Juz.2 (Sura 2:155)

2. Ikhlasi: Kukusudia kitendo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kumtegemea yeye sio mwingine na kuamini kwa imani mkato kwamba yaliyoko mbele ya Mwenyezi Mungu ni bora na yatasalia kuliko jaha, mali na watoto. kisimwaathiri chochote katika hivi na kumtii Mwenyezi Mungu na radhi yake.

Mtu huweza kufikia malengo yake ya kishetani, lakini haya hayahisabiwi kuwa ni ushindi, ila kama tukizingatia batili ni fadhila, wizi ni ghanima na ufisadi ni takua na utengenevu.

3. Kujiepusha na aina yoyote ya kutofautiana. Inaweza kutokea kutofautiana katika maoni na mtazamo kwa ikhlasi. Kutofautiana huku hakupingani na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wala hakuzuii kuafikiana lengo; kama vile kupigana jihadi na wafisadi. Mara nyingi huko kunakuwa ni njia ya kufunguka uhakika.

Vile vile inaweza kuwa sababu ya kutofautiana ni hawaa, na ubinafsi na kupupia dunia. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: “Wala msizozane msije mkaharibikiwa na kupoteza nguvu zetu.”

Mifano ya madhara ya kuzozana na kushindana haina idadi, na katika Historia ni mamia. Hatuna haja ya kutoa mfano wa historia ya mbali, Historia yetu tu ya sasa hivi inatutosha kwa mifano yote. Hivi karibuni nimesoma makala ya mwandishi wa Kimarekani, Salz Bridge aliyoiandika katika gazeti la Herald Tribune. Ninamnukuu:

“Washington inapima tofauti ya idadi ya waarabu na Israil; na inasisitiza kwamba, hata kama si kwa masilahi ya Israil, lakini daima kipimo kitakuwa ni kugawanyika kunakoendelea baina ya dola za kiarabu. Kwa sababu kugawanyika huku kunaifanya idadi ya waarabu iwe ni nambari tu, isiyokuwa na thamani yoyote.”

Kabla ya mwandishi huyu viongozi wa Israil wametangaza mara nyingi kuwa wao walifaulu katika vita vya tarehe 5 Juni kwa msaada wa Marekani na kutofautiana kwa waarabu. Na ni kitu gani kilichowapendeza waisrail kuliko kushikiana silaha waarabu wenyewe kwa wenyewe, badala ya kuwashikia Israil? Kwa ajili hiyo wakoloni wa kizayuni wamefanya kila wawezalo kuwagombanisha waarabu. Jambo la kusikitisha ni kuwa wamepatikana waliowaitikia, bali wanaozungumza kwa niaba yao. Hata hivyo, mapambano bado yanaendelea. Ni lazima wakoloni na vibaraka wao watashindwa, sasa au baadaye.

Wala msiwe kama wale waliotoka majumbani mwao kwa fahari na kujionyesha kwa watu, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka wanayoyafanya.

Baada ya Mwenyezi Mungu (swt) kuwaamrisha waislamu mambo matatu wakiwa wanawaelekea vitani, sasa anawakataza mambo matatu: fahari, kujionyesha, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu.

Amenasibisha sifa hizi tatu kwa makafiri wa kiquraish kwa sababu wao waliotoka kuelekea Badr kumpiga vita Mtume (saw) wakiwa wanajifaharisha, wanajionyesha na kuwazuilia waislamu na njia ya Mwenyezi Mungu.

Wafasiri wanasema: Abu Jahli alipokuwa akiwaongoza maquraish kumpiga vita Mtume huko Badr, njiani alijiwa na Ibn Al-Hiqaf Al-Kinaniy na zawadi kutoka kwa baba yake. Akamwambia Abu Jahli: “Baba yangu anakwambia, kama unataka atakuongozea watu, na kama unataka nitaungana nawe.” Abu Jahli akasema “Ikiwa tunapigana na Mwenyezi Mungu, kama anavyodai Muhammad, basi Wallahi hatumuwezi Mwenyezi Mungu na ikiwa tunapigana na watu, basi sisi ndio watu wenye nguvu zaidi, wala hatutarudi nyuma kupigana na Muhammad mpaka tufike Badr tunywe pombe na watuimbie watumwa na waarabu wasikie.”

Kujifaharisha kunadhihiri katika maana yake pana kwa kauli ya Abu Jahl: “Na sisi ni watu wenye nguvu zaidi.” Ama kujionyesha kuko katika kauli yake: “Na waarabu wasikie.” Kwa ajili hii basi nasi tunaelemea kwenye kauli ya mwenye kusema kuwa Aya hii imemshukia Abu Jahli.
Ama mwisho wa fahari hiyo na ria ni kuuawa waliouawa, akiwemo Abu Jahli na kutekwa waliotekwa na kushindwa waliobakia.

Na shetani alipowapambia vitendo vyao, na kusema: Leo hakuna wa kuwashinda na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipoonana majeshi mawili, alirudi nyuma na kusema: Mimi si pamoja nanyi, mimi naona msiyoyaona, mimi namwogopa, Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

Aya hii inasema waziwazi kuwa kuna kitu kinachoitwa Shetani kiliwachochea maquraish kumpiga vita Mtume huko Badr na kuwapa dhamana ya ushindi, na kwamba yeye alipoyakinisha mwisho wao alijitoa.

Tumekwishaelezea mara nyingi kwamba sisi tunaamini kila linaoelezwa na wahyi na lisilokataliwa na akili; na kwamba tunaiachia ghaibu ufafanuzi. Hakuna kitu katika hukumu ya akili kinachozuia kupatikana kitu kinachoonekana au kisichoonekana kinachowatia mshawasha watu kwenye batili na kuwahadaa. Mwenyezi Mungu (swt) alimwamrisha Mtume wake mtukufu ajilinde na shari ya mwenye kutia wasiwasi katika nyoyo za watu, awe jini au mtu.

Waliposema wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao: Hawa imewadanganya dini yao. Na mwenye kutegemea kwa

Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.

Wanafiki ni wale wanaodhihirisha Uislamu na kuficha ukafiri. Ama wale ambao nyoyoni mwao mna maradhi, ni wanafiki, makafiri na mafasiki.

Kwa hiyo kuunganisha wenye maradhi nyoyonni juu ya wanafiki ni kati- ka kuunganisha jumla juu ya mahsusi.

Mwenyezi Mungu amesimulia, katika Aya hii, kuhusu wenye maradhi ya moyo, kwamba wao walishangaa walipoona kujitokeza kwa waislamu wachache wa kupigana vita na makafiri; wala hawakufahamu tafsir ya kujitokeza huku isipokuwa kujiangamzia kwa waislamu na kuhadaliwa na matumaini ya kufuzu pepo. Kwao hayo ni maneno yasiyo na maana. Kwa sababu kila kitu kwao ni biashara tu; hata dini.

Je Wakombozi Ni Waharibifu?

Wakati huu ambapo nguvu za shari zimeungana kuwafanyia njama waarabu na waislamu na kuwafukuza wazalendo wa Palestina katika ardhi zao na kuwatupa ufuoni wanawake, wazee na watoto; wakati huu ambapo wakombozi wanawanyima usingizi waisrail na kuwakosesha raha; na kutamka neno, uhuru juu ya ukombozi wa ardhi iliyovamiwa, ndipo anaposema Sheikh mwenye kilemba kwenye mpaka wa Israil katika kijiji kimoja cha kaskazini, akinadi kwa kupaza sauti kadamnasi na kusema: “Wakombozi ni waharibifu” sawa na anavyosema Moshe Dayan.

Ewe mheshimiwa! Wakombozi ni waharibifu! Je, wewe na Israil ndio watengenezaji? Kwa nini wakombozi wawe waharibifu? Je, ni kwa kuwa wanapigania haki zao, katika njia ya kuuawa na kuua; au ni kwa vile wao wamebadilisha jina la wakimbizi na kuwa wakombozi? Na, je, wewe katika kauli yako hii unamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kupigana jihadi kutekeleza wajibu wa kidini na wa kiuzalendo?

Ni dini gani hiyo inayokataza kujitolea mhanga kwa ajili ya kulinda mtu nchi yake na kutaka kuishi huru na kuheshimiwa; hata kwa thamani ya namna gani?

Mimi nimeelewa mantiki yako ewe Sheikh. Wewe unasema kuwa Israil inajibu mashambulizi ya wakombozi kwa kuwatesa wanyonge, nasi twakuuliiza: Walikuwa wapi wakombozi mnamo tarehe 29 Juni 1897, wakati Uzayuni ulipofanya mkutano mkuu huko Uswisi, na kupitisha azimio la kuwafukuza waarabu Palestina na waikalie Mayahudi? Je, azimio hilo lilitokana na wakombozi wakati huo?

Kisha utasema nini kuhusu mauaji ya Diryasin na uchinjaji ulofanywa na Mayahudi kwa wakazi wasio na hatia, kabla ya jeshi kuingia Palestina?

Inakupasa ujue ewe mwenye kilemba cha usheikh na kila Mwarabu kwamba waisrail hawatosheki tu na Palestina, Jordan, Lebanon, Syria na Iraq; isipokuwa lengo lake ni kuwadhalilisha waarabu wote wanyenyekee Uzayuni na ukoloni kisiasa na kiuchumi. Israil inatamani mafuta ya Kuwait, Qatar, Abu Dhabi na Saudia.

Tamaa yao hii wameipanga na kuiwekea mkakati kwa kula njama pamoja na dola za kikoloni. Harakati za wakombozi ndizo zilizoharibu mikakati hii ya waisrail kiasi cha kufikiria kuwa Israil haitakuwako.
Ni bora mara elfu tuvumilie maumivu yanayosababishwa na vitendo vya wakombozi, kuliko kuwacha yatimie malengo ya Israil ambayo haiatoshe- ki na chochote; hata mto Nail na Furat.

Zaidi ya hayo, hivi sasa inatulazimu kumkabili adui kwa kupatikana wakombozi wa kujitolea mhanga; kama hatua ya kwanza na tuvumilie taabu zote zitakazosababishwa nao ili kukinga ambalo ni baya na kubwa zaidi.

Baada ya hayo, ewe Sheikh! Unasemaje kuhusu vikosi vilivyokuwa vikitumwa na Muhammad (saw) kukata njia ya maadui zake washirikina na kuchukua mali zao, kuua na kuchukua mateka na kuwakosesha amani majumbani akiwa yeyey mwenye binafsiakiongoza baadhi ya mashmbulizi hayo; kama alivyowapiga Mayahudi wa Bani Quraidha baada ya kuvunja ahadi na kujiiunga na Abu Sufyan, adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika vita vya Ahzab.

Mtume (saw) aliliamrisha jeshi lake alilokuwa akiliongoza yeye mwenyewe lichome mimea ya mayahudi, na kukata miti yao na kuvunja majumba yao. Je, kitendo chake hicho Mtume kilikuwa cha utengezaji au uharibifu?

Imepokewa Hadith Mutawatir aliposema Mtume (saw): “Mwenye kufa akilinda mali yake amekufa Shahid” Je vipi kwa yule atakayokufa katika hali ya kumzuia Mwisrail adui wa Mwenyezi Mungu, wa nchi na wa binadamu wote?

Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّ اللَّهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنْفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ ۚ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ ۖ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنْجِيلِ وَالْقُرْآنِ ۚ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ مِنَ اللَّهِ ۚ فَاسْتَبْشِرُوا بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُمْ بِهِ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ {111}

‘Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa waumini nafsi zao na mali zao kuwa wao watapata pepo. Wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanaua na wanuawa. Hii ni ahadi aliyojilazimisha kwa haki katika Tawrat na Injili na Qur’an. Na ninani atimiziaye ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.” (9:111)

Wala hakuna anayeitumia Aya hii katika umma wa Kiarabu isipokuwa wapiganaji ukombozi; na kujitolea kwao ndio jiwe la msingi la mapinduzi ya mataifa yote ya kiarabu.

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ يَتَوَفَّى الَّذِينَ كَفَرُوا ۙ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ {50}

Na lau ungeliwaona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakipiga nyuso zao na migongo yao na (kuwaambia) ionjeni adhabu iunguzayo.

ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِلْعَبِيدِ {51}

Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyokwishatangulizwa na mikono yenu. Na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.

كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ ۙ وَالَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۚ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّهِ فَأَخَذَهُمُ اللَّهُ بِذُنُوبِهِمْ ۗ إِنَّ اللَّهَ قَوِيٌّ شَدِيدُ الْعِقَابِ {52}

Ni kama ada ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; walizikufuru ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa sababu ya makosa yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mkali wa kuadhibu.

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّهَ لَمْ يَكُ مُغَيِّرًا نِعْمَةً أَنْعَمَهَا عَلَىٰ قَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنْفُسِهِمْ ۙ وَأَنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {53}

Hiyo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizowaneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo nafsini mwao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.

كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ ۙ وَالَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۚ كَذَّبُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُمْ بِذُنُوبِهِمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ ۚ وَكُلٌّ كَانُوا ظَالِمِينَ {54}

Ni kama hali ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; walizikadhibisha ishara za Mola wao, kwa hiyo tukawaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, na tukawazamisha watu wa firaun. Na wote walikuwa madhalimu.