read

Aya 49 – 52: Na Miongoni Mwao Kuna Anayesema: Niruhusu

Maana

Na miongoni mwao kuna anayesema: Niruhusu wala usinitie katika fitina.

Wamekubaliana wafasiri kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipotoa mwito wa kwenda kwenye vita vya Tabuk, Jad bin Qays, aliyekuwa ni katika wakuu wa kinafiki, alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni ruhusu, kwa vile mimi ni mtu ninayependa wanawake, ninaogopa nikawaona wanawake wa Kirumi nitafitinika nao”, ndipo akashuka Aya hiyo. Mnaafiki huyu alidai kuwa anahofia dhambi kwa wanawake kama atapigana pamoja na Mtume (saw), lakini asiogope kuingia katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Hakika wamekwishatumbukia katika fitina.

Yaani walidai kukimbia dhambi na wakaingia katika dhambi waliyoikimbia au zaidi yake.

Na hakika Jahannam imewazunguka makafiri katika pande zote wala hawatapa kimbilio.

Mtume aliwapa mwito wa kujitakasha kwa kutubia dhambi zao ambazo zimewazunguka kila upande, lakini wakakataa mwito wake, ndipo ikawazunguka adhabu kila upande.

Ukikupata wema unawachukiza.

Kama ilivyo kawaida ya mtu mbaya, huchukia sana watu wema wanapopata yanayowapendeza; na hufurahi sana wanapopatwa na yanayowachukiza.

Na ukikusibu msiba husema: Tuliangalia vizuri mambo yetu tangu mwanzo, na hugeuka kwenda zao wakiwa wamefurahi

Mfumo unafahamisha kwamba makusudio ya msiba ni kuvunjika jeshi la waislamu. Kwa sababu kusema kwao: ‘Tuliangalia vizuri mambo yetu,’ maana yake ni kuwa waislamu walipokuwa wakipata machukivu, basi wanafiki walikuwa wakizungumziana kwa furaha na kuambiana kuwa sisi tulichukua tahadhari, umetangulia mfano wa hayo katika Juz. 4 (3: 120) na Juzuu hii (8:49)

Sema halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu.

Yaani sema ewe Mtume kuwaambia wanafiki. Sisi ndio ambao tumezinduka na kuchukua tahadhari, sio nyinyi kwa sababu nyinyi mmekaa tu, na sisi tumepigana jihad baada ya kujiandaa; na tumepitia desturi ya Mwenyezi Mungu katika vita, kuna siku yetu na siku yao, mapambano bado yanaendelea, mambo huangaliwa mwisho wake, ushindi ni wetu mwishoni na kila lijalo likaribu.

Yeye ni Mola wetu, basi waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.

Ambao wanajiandaa kisha wakaendelea kwa jina la Mwenyezi Mungu. Wakipatwa na vizuri husema: Hii ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu na rehema yake, na wakipatwa na msiba husema hiyo ni kudura ya Mwenyezi Mungu; wakiwa katika hali ya ikhlas na yakini ya dini yao; na kwamba Mwenyezi Mungu ataidhihirisha kuliko dini zote wajapochukia makafiri.

Sema: Nyinyi hamtutazami ila moja ya mema mawili, ambayo ni ushindi au kufa shahidi.

Katika ushindi kuna kuwadhalilisha makafiri na wanafiki; na katika shahada kuna thawabu kubwa. Yote mawili ni utukufu na heshima.

Na sisi tunawatizamia kuwa Mwenyezi Mungu awafikishie adhabu itokayo kwake au kwa mikono yetu. Basi ngojeni nasi tunangoja pamoja nanyi.

Kwa vyovyote mwisho wa wanaopigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni moja ya mambo mawili mazuri: ushindi au kufa shahidi.

Na, mwisho wa wanafiki na makafiri ni moja ya maovu mawili: Ama adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu au kupigwa na waumini wanapopata idhini ya Mwenyezi Mungu.

قُلْ أَنْفِقُوا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا لَنْ يُتَقَبَّلَ مِنْكُمْ ۖ إِنَّكُمْ كُنْتُمْ قَوْمًا فَاسِقِينَ {53}

Sema: toeni kwa kupenda au kuchukia haitakubaliwa kwenu. Hakika nyinyi mmekua watu mafasiki.

وَمَا مَنَعَهُمْ أَنْ تُقْبَلَ مِنْهُمْ نَفَقَاتُهُمْ إِلَّا أَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّهِ وَبِرَسُولِهِ وَلَا يَأْتُونَ الصَّلَاةَ إِلَّا وَهُمْ كُسَالَىٰ وَلَا يُنْفِقُونَ إِلَّا وَهُمْ كَارِهُونَ {54}

Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao, ila ni kwamba wao wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wala hawaiendei swala ila katika hali ya uvivu, wala hawatoi ila kwa kuchukia.

فَلَا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُمْ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُعَذِّبَهُمْ بِهَا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنْفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ {55}

Basi zisikushangaze mali zao wala watoto wao. Hakika Mwenyezi Mungu anataka tu kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia. Na roho zao zitoke na hali wao ni makafiri.

وَيَحْلِفُونَ بِاللَّهِ إِنَّهُمْ لَمِنْكُمْ وَمَا هُمْ مِنْكُمْ وَلَٰكِنَّهُمْ قَوْمٌ يَفْرَقُونَ {56}

Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, na wala wao si katika nyinyi. Lakini wao ni watu wanaogopa .

لَوْ يَجِدُونَ مَلْجَأً أَوْ مَغَارَاتٍ أَوْ مُدَّخَلًا لَوَلَّوْا إِلَيْهِ وَهُمْ يَجْمَحُونَ {57}

Lau wangelipata pa kukimbilia au mapango au mahali pa kuingia wangeligeukia huko kwa kasi sana.