read

Aya 5-8: Miezi Mitukufu Ikiisha

Maana

Ikisha miezi mitukufu, basi waueni washirikina popote mtakapowakuta, na wakamateni na muwazingire na wakalieni katika kila njia.

Kuwakamata ni kuwachukua mateka. Kuwazingira, kuwafunga na kuwakalia kila njia ni kuwachunga katika kila njia wanayopita na kutowaacha wasichomeke.

Ama miezi mitukufu tumetaja katika Juz.2 (2:194) kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha kupigana katika miezi minne: Dhul-Qaada, Dhul- Hijja, Muharram na Rajab.1

Miezi hii siyo iliyo kusudiwa hapa; isipokuwa makusudio ya miezi mitukufu hapa ni miezi minne ambayo Mwenyezi Mungu aliharamisha ndani yake kupigana na washirikina wa Bara Arabu. Akawahalalishia ndani ya muda huu watembee kwa amani katika nchi, kuanzia tarehe 10, Dhul-Hijja 9 A.H mpaka tarehe 9 Rabiul- Akhar 10A.H.

Baada ya hapo aliamrisha kuwapiga washirikina na kuwateka na kuwafunga na kuwaandama popote watakapoelekea, ikiwa hawakusilimu au wahame kabla ya kwisha muda. Hiyo ni kwa ajili ya kuchelea shari yao na ufisadi wao.

Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Yaani wakisilimu kabla ya kwisha muda na wakaendeleza nembo za dini ambazo miongoni mwa zilizo muhimu ni kuswali na kutoa zaka, basi wao wako katika amani. Watakuwa kama waislamu wengine bila ya tofauti yeyote.

Na kama yeyote katika washirikina akikutaka hifadhi, basi mhifadhi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha mfikishe mahali pake pa amani.

Yaani mshirikina yeyote ambaye inajuzu kumwua, akijitolea au kutaka hifadhi ya amani kwa waislamu basi wamhifadhi na kumpa amani ya nafsi yake na mali yake, na kumlingania kwenye Uislam kwa hikima na mawaidha mazuri.

Akikubali basi atachukuliwa kama waislamu wengine, na kama akikataa basi si halali kumuua na ni wajibu kwa waislamu kumfikisha mahali atakapo kuwa salama.

Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua.

Hayo ni ishara ya kutoa hifadhi kwa mshirikina, kumwambia maneno ya Mwenyezi Mungu na kumfikisha mahali pa salama yake. Kusema kwake Mwenyezi Mungu: ‘Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua’ ni kubainisha sababu ambayo ni kutojua wale washirikina wanaotaka hifadhi Uislamu na hakika yake.

Wametoa fat-wa mafaqih kwamba waislamu wawape amani washirikina kwa sharti ya kutokuweko uchafuzi wa amani, kwa yule mtaka hifadhi asiwe ni jasusi na wala jihadi isiyumbe kwa kumpa amani.

Itakuwaje ahadi kwa washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake.

Aya hii inakamilisha Aya ya kwanza na ya nne ya Sura hii. Mwenyezi Mungu (swt) amewajibisha, katika Aya ya kwanza, kuvunja mkataba na washirikina waliofanya hiyana. Hawa ndio wanaokusudiwa hapa. Na amewajibisha, katika Aya ya nne, kutekeleza mkataba na washirikina wanaoheshimu mkataba bila ya kupunguza kitu, hao ndio wanaokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Isipokuwa wale mlioahidiana kwenye msikiti mtakatifu.

Basi maadamu wanakwenda na nyinyi sawa nanyi nendeni nao sawa.

Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua.

Yaani bakieni nao na mkataba wa amani maadamu wao wamebaki hivyo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawachukia watu wa hiyana na anawapenda wanaotekeleza wenye kumcha Mwenyezi Mungun(takua).

Kusema kwake kwenye msikiti mtakatifu, ni kuashiria mahali palipofanyi- ka mkataba wa amani na Bani Kinana. Kwani Mtume (saw) aliwekeana nao mkataba aliopatana nao Hudaibiya karibu na Makka.

Itakuwaje! nao wakiwashinda hawaangalii kwenu ujirani wala ahadi. Wanawafurahisha kwa midomo yao tu, hali nyoyo zao zinakataa. Na wengi wao ni mafasiki.

Dhamir inawarudia wavunjaji mkataba. Amewataja, Mwenyezi Mungu, kwa mambo matatu mabaya:

1. Uovu, kwa sababu wao lau wangeliwashinda waislam wangewalifanya vya kuwafanya bila ya kuchunga ahadi wala ubinadamu.

2. Unafiki kwamba wao wanasema mdomoni yale yasiyokuwa nyoyoni mwao.

3. Ufasiki.

Sifa moja tu miongoni mwa sifa hizi tatu inawahukumu kuadhibiwa na kuwatoa katika haki zote za ubinadamu, sikwambii kuwatekelezea ahadi tena. Sasa itakuwaje wakisifika na zote tatu kwa pamoja!

Utauliza, makafiri wote ni mafasiki kwa sababu, ukafiri ni ufasiki na zaidi. Sasa vipi Mwenyezi Mungu (swt) amewatoa wengine kwa kauli yake. ‘Na wengi wao ni mafasiki?’

Jibu: maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu na wengi wao ni mafasiki ni kwamba makafiri wengi huendelea na ukafiri na ufasiki wao, wala hawatarajiwi kuongoka kwa hali yeyote.

Na wako wachache miongoni mwao wanaoacha upotevu wao. Kwa hiyo makusudio ya ufasiki hapo ni kuendelea na kutouacha. Aina ya ibara kama hii ni nyingi katika Qur’an.

اشْتَرَوْا بِآيَاتِ اللَّهِ ثَمَنًا قَلِيلًا فَصَدُّوا عَنْ سَبِيلِهِ ۚ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {9}

Wamenunua thamani ndogo kwa ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wakazuilia na njia yake. Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya.

لَا يَرْقُبُونَ فِي مُؤْمِنٍ إِلًّا وَلَا ذِمَّةً ۚ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُعْتَدُونَ {10}

Hawaangalii kwa Mumin ujirani wala ahadi; na hao ndio warukao mipaka.

فَإِنْ تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ ۗ وَنُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ {11}

Kama wakitubu na wakasi- mamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini na tunazifafanua Aya kwa watu wanaojua

وَإِنْ نَكَثُوا أَيْمَانَهُمْ مِنْ بَعْدِ عَهْدِهِمْ وَطَعَنُوا فِي دِينِكُمْ فَقَاتِلُوا أَئِمَّةَ الْكُفْرِ ۙ إِنَّهُمْ لَا أَيْمَانَ لَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَنْتَهُونَ {12}

Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi piganeni na viongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana viapo (vya maana). Ili wapate kukoma.

أَلَا تُقَاتِلُونَ قَوْمًا نَكَثُوا أَيْمَانَهُمْ وَهَمُّوا بِإِخْرَاجِ الرَّسُولِ وَهُمْ بَدَءُوكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ ۚ أَتَخْشَوْنَهُمْ ۚ فَاللَّهُ أَحَقُّ أَنْ تَخْشَوْهُ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {13}

Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumtoa Mtume nao ndio waliowaanza mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope ikiwa nyinyi ni waumin.

قَاتِلُوهُمْ يُعَذِّبْهُمُ اللَّهُ بِأَيْدِيكُمْ وَيُخْزِهِمْ وَيَنْصُرْكُمْ عَلَيْهِمْ وَيَشْفِ صُدُورَ قَوْمٍ مُؤْمِنِينَ {14}

Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe, na awanusuru muwashinde na avipoze vifua vya kaumu ya waumin.

وَيُذْهِبْ غَيْظَ قُلُوبِهِمْ ۗ وَيَتُوبُ اللَّهُ عَلَىٰ مَنْ يَشَاءُ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {15}

Na aondoe hasira ya nyoyo zao Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi, mwenye hekima.
  • 1. Mfunguo Pili, Mfunguo tatu, Mfunguo nne na mfunguo kumi (Rajab)