read

Aya 50 – 54: Lau Ungeona

Maana

Na lau ungeliwaona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakipiga nyuso zao na migongo yao na (kuwaambia) ionjeni adhabu iunguzayo.

Maneno yanaelekezwa kwa kila mwenye kuona, kwa sababu makusudio ni mawaidha na mazingatio. Makusudio ya wale waliokufuru ni kila kafiri, kwa kuchukulia dhahiri ya tamko kama lilivyo. Imesemekana kwamba makusudio ni kuwahusu makafiri wa Kiquraish waliopigana na Mtume (saw) katika vita vya Badr, kwa kuchukulia mfumo wa maneno. Kwa sababu bado maneno ni ya tukio la Badr.

Kupiga nyuso na migongo yao ni fumbo la adhabu wanayoipata makafiri wakati wa kufa. Inawezekana kuwa ni kupiga hasa kwa kiuhakika, hata kama hakuonekani. Vyovyoote iwavyo ni kwamba makafiri wanahizika wakati wa kufa na baada ya kufa; wala hatuna umuhimu wa kutaja aina ya hizaya yenyewe.

Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyokwishatangulizwa na mikono yenu.

Na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.

Vipi adhulumu naye anaikataza dhuluma na kuiwekea adhabu? Sunni wanasema kuwa akili inajuzisha kwa Mwenyezi Mungu mtukufu amwadhibu mtiifu na kumpa thawabu mwasi. Vile vile akili inajuzisha Mwenyezi Mungu ahalifu ahadi yake. Tazama Mawaqif 8 sehemu ya 5 na sita. Na Madhahibul-Islamiya cha Abu Zuhura uk. 104.

Shia wanasema: Akili haijuzishi kwa Mwenyezi Mungu amwaadhibu mtiifu na inajuzisha kumpa fadhila mwasi. Kwa sababu mwadilifu hamwadhibu mtiifu na mkarimu mpole humsamehe mwenye kumfayia uovu.

Ni kama ada ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; walizikufuru ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa sababu ya makosa yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mkali wa kuadhibu.

Yaani yaliyowapata washirikina siku ya Badr, kuuliwa na kutekwa, ni kwa sababu wao walimkadhibisha Muhammad (saw). Yaliyowapata hawa yanafanana na yaliyowapata washirikina waliotangulia. Kwa sababu wali- wakadhibisha Mitume wao; kama watu wa Firaun na waliokuwa kabla yao.
Hiyo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizowaneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo nafsini mwao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.

Dhahiri ya neema hapa ni riziki na kuibadilisha ni kuiondoa.
Hapa linajitokeza swali kuwa dhahir ya Aya inafahamisha kwamba watu aliowaneemesha Mwenyezi Mungu kwa riziki hubakia kwao maadamu ni watiifu. Wakiasi hunyang’anywa. Lakini tunavyoona ni kuwa waasi wengi, kila wanavyozidi uasi ndivyo wanavyozidi utajiri wala hakibadili kitu kwao je ni vipi?

Jibu: Aya haikutaja tamko la maasi wala ukafiri. Lililofahamisha Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu haondoi neema kwa watu wake ila wakibadilisha yaliyomo nyoyoni mwao, lakini Mwenyezi Mungu hakubainisha aina ya mabadiliko. Mfano wake ni Aya isemayo:

إِنَّ اللَّهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنْفُسِهِمْ ۗ {11}

“Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyomo nafsini mwao.. (13:11).

Watu wa Firaun, aliowatolea mfano Mwenyezi Mungu katika Aya iliyotangulia, walikuwa washirikina kabla na baada. Wao walizidisha kupetu- ka mipaka baada ya Musa kuwajia.

Kwa hiyo tutachukulia Aya tuliyonayo, kwenye maana ya kuwa Mwenyezi Mungu hawaangamizi watu duniani ila ni baada ya kuwapelekea Mtume na kuwalingania kwa Mwenyezi Mungu ana kwa ana; kisha waukatae mwito wake; kama vile watu wa Firaun na waliotangulia; wakiwemo watu wa Nuh, Lut na wengineo. Na kama hakuwapelekea Mtume, basi huchelewesha adhabu yao mpaka siku ya hisabu na malipo. Ama kuhusu Aya (13:11) tuna maoni katika tafsir yake tutayabainisha huko inshallah.

Ni kama hali ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; wal- izikadhibisha ishara za Mola wao, kwa hiyo tukawaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, na tukawazamisha watu wa firaun.

Umepita mfano wake katika Juz.3 (3:11)

Na wote walikuwa madhalimu.

Yaani kila mmoja katika watu wa Firaun ambao walimkadhibisha Musa (as) na makafiri wa Kiquraish ambao walimkadhibisha Muhammad (saw). Wamejidhullumu wao wenyewe na wakawadhlumu watu kwa kuwazuilia njia ya Mwenyezi Mungu.

إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِنْدَ اللَّهِ الَّذِينَ كَفَرُوا فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ {55}

Hakika wanyama waovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaokufuru, basi hawataamini.

الَّذِينَ عَاهَدْتَ مِنْهُمْ ثُمَّ يَنْقُضُونَ عَهْدَهُمْ فِي كُلِّ مَرَّةٍ وَهُمْ لَا يَتَّقُونَ {56}

Ambao umepeana nao ahadi kisha wanavunja ahadi yao kila mara; wala hawaogopi.

فَإِمَّا تَثْقَفَنَّهُمْ فِي الْحَرْبِ فَشَرِّدْ بِهِمْ مَنْ خَلْفَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ {57}

Basi ukiwakuta vitani wakimbize kwa hao walio nyuma yao ili wapate kufahamu.

وَإِمَّا تَخَافَنَّ مِنْ قَوْمٍ خِيَانَةً فَانْبِذْ إِلَيْهِمْ عَلَىٰ سَوَاءٍ ۚ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْخَائِنِينَ {58}

Na kama ukihofia hiyana kwa watu, basi watupie kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao hiana.

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا سَبَقُوا ۚ إِنَّهُمْ لَا يُعْجِزُونَ {59}

Wala wale waliokufuru wasifikirie kwamba wao wametangulia; kwa hakika wao hawatashinda

وَأَعِدُّوا لَهُمْ مَا اسْتَطَعْتُمْ مِنْ قُوَّةٍ وَمِنْ رِبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدُوَّ اللَّهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِنْ دُونِهِمْ لَا تَعْلَمُونَهُمُ اللَّهُ يَعْلَمُهُمْ ۚ وَمَا تُنْفِقُوا مِنْ شَيْءٍ فِي سَبِيلِ اللَّهِ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنْتُمْ لَا تُظْلَمُونَ {60}

Na waandalieni nguvu kama vile muwezavyo na kwa farasi waliofungwa ili mumtishe adui wa Mwenyezi Mungu na adui yenu, na wengineo msiowajua nyinyi, Mwenyezi Mungu anawajua. Na chochote mtakachotoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, mtarudishiwa, wala nyinyi hamtadhulumiwa.

وَإِنْ جَنَحُوا لِلسَّلْمِ فَاجْنَحْ لَهَا وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {61}

Na kama wakielekea kwenye amani, nawe ielekee, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ni mwenye kusikia mwenye kujua.

وَإِنْ يُرِيدُوا أَنْ يَخْدَعُوكَ فَإِنَّ حَسْبَكَ اللَّهُ ۚ هُوَ الَّذِي أَيَّدَكَ بِنَصْرِهِ وَبِالْمُؤْمِنِينَ {62}

Na kama wakitaka kukuhadaa, basi Mwenyezi Mungu atakutoshelezea. Yeye ndiye aliyekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.

وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ ۚ لَوْ أَنْفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مَا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ ۚ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {63}

Na akaziunganisha nyoyo zao; lau ungelitoa yote yaliyomo ardhini usingeliweza kuiunganisha mioyo yao, lakini Mwenyezi Mungu amewaunganisha. Hakika yeye ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.