read

Aya 53 – 57: Sadaka Za Wanafiki

Maana

Sema: toeni kwa kupenda au kuchukia haitakubaliwa kwenu.

Baada ya Mtume (saw) kujiandaa kwa vita vya Tabuk, mnafiki mmoja alimtaka amruhusu asiende kwenye jihadi, akatoa kitu kidogo katika mali yake.

Mwenyezi Mungu akamwamuru Mtume wake amwambie mnafiki huyu na mfano wake kuwa Mwenyezi Mungu haana haja na mali zenu na zichukueni wenyewe, hata kama mmetoa kwa kupenda au kutopenda.

Utauliza: Tunajua njia ya kukataa ikiwa kutoa ni kwa kutopenda; sasa kuna wajihi gani wa kukataa ikiwa kutoa ni kwa kupenda?

Jibu: Wao hawakutaka kutoa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa walitaka umashuhuri na jaha. Hakuna tofauti kati ya kutoa kwa lengo hili na kutoa kwa kutopenda kwa kuhofia kutojulikana hakika yao – yote mawili ni kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akawaambia:

Hakika nyinyi mmekua watu mafasiki.

Na, kuwaita mafasiki kunaashiria kuwa ufasiki ndio sababu ya kutokubaliwa.

Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao, ila ni kwamba wao wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake,

Wanafiki walitoa mali zao ili tu waambiwe kuwa nao wametoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na huku wanamkanusha . Na, unafiki huu na ria hii ndio sababu ya kutokubaliwa wanachokitoa.

Lau wangelitoa kwa ubinadamu tu, kama vile mlahidi anapomlisha mwenye njaa, ingeliweza kusemwa: ‘Hakuna malipo ya hisani ila hisani.’ Lakini unafiki ni uovu; na mwenye kufanya uovu atalipwa . Kwa maelezo zaidi angalia Juz.4 (3:177) Kifungu cha ‘Kafiri na amali ya Kheri’

Wala hawaiendei swala ila katika hali ya uvivu, wala hawatoi ila kwa kuchukia.

Hali hiyo ndiyo natija ya ukafiri kwa sababu kuswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kutoa kwa ajili yake ni matawi ya imani.

Basi zisikushangaze mali zao wala watoto wao. Hakika Mwenyezi Mungu anataka tu kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia.

Unaweza kuuliza kuwa mali na watoto inaweza kuwa ni sababu ya adhabu ya Akhera, ambapo watu wengi, siku za shida wamewahi kuahidi wema, lakini wanapojiwa na fadhila za Mwenyezi Mungu hupetuka mpaka na kufanya uovu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

كَلَّا إِنَّ الْإِنْسَانَ لَيَطْغَىٰ {6}

أَنْ رَآهُ اسْتَغْنَىٰ {7}

“Hakika binadamu hupetuka mpaka kwakujiona ametajirika” (96:6-7)

Na akasema:

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ {28}

“Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna.” Juz.9 (8:28)

Lakini kuwa mali na watoto ni sababu ya adhabu katika dunia, hilo ni kinyume; hasa mali iliyotafutwa chini ya ardhi na ndani ya bahari na wa kati ambapo teknolojia imeendelea kufikia kuitafuta mwezini na kwengineko. Zaidi ya hayo, kauli hii haiafikiani na kauli isemayo:

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ {46}

“Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia” (18:46)

Na kama itakuwa mali ni sababu ya adhabu katika maisha haya, basi adhabu haitahusika na wanafiki tu, bali itawaenea watu wote.” Sasa itakuwaje?

Jibu: Ni kweli huu ni mushkel, lakini ikiwa Aya inawahusu wote. Ama ikiwa inakusudia tukio maalum, basi hakutakuwa na mushkeli wowote.

Mfumo wa maneno ulio kabla ya Aya hii na iliyo baada yake, unafahamisha waziwazi kwamba dhamiri katika ‘Anataka kuwadhibu”, inarudia kuhusisha wanafiki waliokuwa wakati wa Mtume na kuwahusu hasa wale waliojitoa katika vita vya Tabuk ambao walikuwa kiasi watu themanini na kitu, kama ilivyosemekana, na walikuwemo wenye mali nyingi na watoto wengi.

Ili isisemwe kuwa vipi watu hawa ni wafasiki na Mwenyezi Mungu amewaneemesha kwa mali na watoto. Ndipo Mwenyezi Mungu akasema: Hakika tu Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia”.

Na, kweli Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa watoto wao. Kwani watoto wao walikubali Uislam na wakawa na ikhlasi, kinyume na mababa zao. Hakuna hasara mbaya kwa mzazi kuliko kuwa mwanawe ana dini nyingine na itikadi nyingine. Mwana wa Abdallah bin Ubayya, alisilimu na kupendekeza kwa Mtume (saw) amuue baba yake, mkuu wa wanafiki, lakini Mtume akakataa.

Vile vile aliwaadhibu kwa mali zao, kwa vile wao walikuwa na yakini kuwa itawageukia wale ambao hawako katika dini yao na njia yao.

Kwa hiyo Aya inahusika na wanafiki waliokuwa katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Na kwa hali hiyo basi hakuna wajihi wowote kwa waliyoyataja wafasiri, kwamba kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu kwa mali zao ni kutabika kuitafuta, na kwamba kuadhibiwa kwa wototo wao ni kuona uchungu wakiugua na wakiwakosa. Kwani tabu hiyo na machungu hayo hayahusiki na wanafiki peke yao, bali ni kila mwenye mali na familia.

Na roho zao zitoke na hali wao ni makafiri.

Yaani watakufa wakiwa makafiri na Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa kufuru yao huko Akhera, kama alivyowaadhibu kwa mali zao katika dunia.

Tabrasi katika Majmaul-bayan anasema: “Matakwa ya Mwenyezi Mungu yamefungamana na kutoka roho zao sio ukafiri wao; kama kusema: Nataka kumpiga akiwa asi. Hapa kutaka kumefungamana na kupiga sio kuasi.”

Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, na wala wao si katika nyinyi.

Kuna faida gani ya kiapo hiki na Mwenyezi Mungu ameshuhudia kwamba wao wamesilimu kwa kuhofia, sio kwa kukinai.

Lakini wao ni watu wanaogopa

Nyoyo za wanafiki zilijazwa na hofu kwa nguvu ya waislamu

Lau wangelipata pa kukimbilia au mapango au mahali pa kuingia wangeligeukia huko kwa kasi sana.
Yaani wangelikimbilia huko kwa kasi sana. Wanafiki hawakuweza kutoka Madina, pia hawakuthubutu kudhihirisha ukafiri kwa vile Uislamu ulikuwa umeingia katika kila nyumba ya Aus na Khazraj. Kwa hiyo wakalazimika kusilimu kwa ncha za ndimi zao wakiwa ni makafiri nyoyoni wakingoja fursa ya kuufanyia vitimbi Uislamu.

وَمِنْهُمْ مَنْ يَلْمِزُكَ فِي الصَّدَقَاتِ فَإِنْ أُعْطُوا مِنْهَا رَضُوا وَإِنْ لَمْ يُعْطَوْا مِنْهَا إِذَا هُمْ يَسْخَطُونَ {58}

Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka. Na wanapopewa katika hizo huridhika, na wasipopewa katika hizo huchukia.

وَلَوْ أَنَّهُمْ رَضُوا مَا آتَاهُمُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّهُ سَيُؤْتِينَا اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ وَرَسُولُهُ إِنَّا إِلَى اللَّهِ رَاغِبُونَ {59}

Na lau wangeliridhia kile alichowapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila zake, na Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu.