read

Aya 55 – 63: Kanuni Na Hukumu Katika Amani Na Vita

Maana

Aya hizi zimekusanya kaida na hukumu katika hali ya usalama na ya vita. Tutazifafanua kulingana na mpango ufuatao:-

Hakika wanyama waovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaokufuru, basi hawataamini. Ambao umepeana nao ahadi kisha wanavunja ahadi yao kila mara; wala hawaogopi

Asili ya neno mnyama (Dabba) ni kila anayetembea ardhini. Kisha ikawa neno hilo linatumiwa sana na wenye miguu mine.

Mwenyezi Mungu (swt) anasema kuwa jamaa waliokufuru, ambao imani yao haitarajiwi walielewana na Mtume (saw) kuishi kwa amani na ujirani mwema. Lakini kumbe wamedhamiria uhaini na wakauvunja ahadi zaidi ya mara moja; hawakuogopa balaa wala adhabu itakayotokana na hayo. Mwenyezi Mungu amewataja hawa kuwa ni waovu zaidi kuliko mnyama.

Kuna kundi la wafasiri wamesema kuwa ni Mayahudi wa Bani Quraidha, waliahidiana na Mtume kisha wakavunja ahadi na kusaidiana na washirikina wa Makka siku ya Badr. Mtume (saw) aliposhinda waliomba msamaha, akawakubalia na kuwasamehe.

Kisha wakawaahidiana mara ya pili, wakavunja ahadi siku ya Khandaq. Si ajabu kwa Mayahudi kufanya hiyana na kuvunja ahadi; isipokuwa ajabu ni kuwa na ukweli na uaminifu .

Basi ukiwakuta vitani wakimbize kwa hao walio nyuma yao ili wapate kufahamu.
Maneno haya anaambiwa Mtume (saw). Mwenyezi Mungu anabainisha hukumu ya hawa makafiri wasio na ahadi; kwamba akiwapata awatie adabu kali kabisa; hata wengine wanaotaka kufanya hiyana wapate funzo. Kwa hivyo basi inatubainikia kuwa makusudio ya walio nyuma yao ni wengine.

Na kama ukihofia hiyana kwa watu, basi watupie kwa usawa.

Makusudio ya kuhofia hapa ni kujua; na usawa ni kuwa sawa wewe na wao katika kujua kuvunja ahadi.

Maana ni ikiwa baina yako wewe Muhammad na watu kuna mapatano na ukajua kabisa kwamba wao watavunja ahadi, kwa kuonyesha alama wazi wazi kuwa wao wana dhamira mbaya au hiyana na kuyafanya mapatano ni pazia ya kupanga njama zao, basi yatupilie mbali mapatano yao na uwafahamishe kuwa umevunja mapatano yao; wala usianze kupigana kabla ya kuwafahamisha ili usinasibishiwe uhaini; kwani hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao hiana.

Kwa maneno mengine ni kwamba Uislamu unawajibisha kutekeleza ahadi kwa watekelezao ahadi. Ama wale wanaofanya ahadi ni nyenzo ya uhaini basi Uislamu unaamrisha kuivunja, kwavile hiyo si ahadi bali ni vitimbi.

أَنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي كَيْدَ الْخَائِنِينَ {52}

“… Hakika Mwenyezi Mungu haongozi vitimbi vya wahaini.” (12:52).

Imam Ali (as) anasema: Kuwatekelezea ahadi wavunja ahadi ni kuvunja ahadi na kuvunja ahadi kwa wavunja ahadi ni kutekeleza ahadi.”

Wala wale waliokufuru wasifikirie kwamba wao wametangulia; kwa hakika wao hawatashinda.

Maana ya wametangulia ni wameponyoka. Na hawatashinda, ni hawatanishinda mimi. Maana ya Aya kwa ujumla ni kuwa asifikirie yeyote kwamba Mwenyezi Mungu anapitwa na jambo.

Na waandalieni nguvu kama vile muwezavyo na kwa farasi waliofungwa.

Aya zilizotangulia zimeonyesha mfungamano wa mapatano na hukumu ya anayeyavunja. Katika Aya hii, Mwenyezi Mungu (swt) anawaamrisha Waislamu kujianda kwa nguvu na kukamilisha maandalizi dhidi ya adui.

Makusudio ya nguvu ni chochote kile kinachotia nguvu. Katika kumkabili adui, iwe ni Mkuki, Roketi, au chochote. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja Farasi, kwa sababu wakati huo ndio ilikuwa silaha ya kutegemea. Imepokewa hadith kutoka kwa Mtume (saw) kwamba yeye alisoma Aya hii na kusema:

“Tambueni kwamba nguvu ni kurusha.” Alilikariri mara tatu. Makusudio ni kubainisha umuhimi wa kurusha na athari yake katika vita.

Historia imethibitisha umuhimu wa nadhari hiyo aliyoitamka Mtume (saw) kiasi miaka elfu moja na mia tatu; ambapo hakukua na makombora wala mizinga. Wataalamu wameelekeza akili zao kila mara kukaza nguvu za kurusha kuanzia mishale hadi risasi; na kutoka kwenye mizinga hadi mabomu ya Atomic na Haidrogeni. Waislamu walitumia, pamoja na Mtume, teo katika vita ya Khaibar.

Ili mumtishe adui wa Mwenyezi Mungu na adui yenu, na wengineo msiowajua nyinyi, Mwenyezi Mungu anawajua.

Mwenyezi Mungu (swt) amewagawanya maadui aina mbili: Aina iliyo dhahir ambayo waislamu waliwajua na aina isiyodhahiri ambayo waislamu hawakuwajua uadui wao; nao ni kila anayetamani uislamu ushindwe, kwa kuhofia utawala wao; yakiwemo mataifa ya jirani; kama vile Fursi na Roma ambao baadae walishindwa na waislamu ulipopata nguvu.

Nguvu Za Kujilinda Na Nguvu Za Uchokozi

Hebu tusimame kidogo kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: “Ili mumtishe adui wa Mwenyezi Mungu na adui yenu.” Kwa sababu ina- fungamana na msingi wa kuilinda jamii ya binadamu kutoka na vurugu, na kuwazuia mataghuti kuchezea maisha ya binadamu na kuwakandamiza.

Msingi huu ni kupatikana nguvu, kwa watu wa haki na uadilifu, itakayoweza kuwazuia madhalimu na wavunjaji na kuwafanya wawe chini ya hukumu na sharia ya Mwenyezi Mungu inayowataka watu wote waishi kulingana na kanuni ya maisha na desturi yake, wala asikengeuke yeyote. Akitamani tu kupotoka basi nguvu hiyo imzime na kumrudisha kwenye desturi hiyo.

Lau mabingwa na wenye akili watafanya utafiti wa sababu ya matatizo ya maisha na maangamivu ni kudhoofisha nguvu ya kukinga maovu na kuipa ubabe nguvu ya uchokozi.

Mfano mzuri wa hilo ni ni nguvu wanazomiliki Marekani na kuzitumia katika uporaji na unyang’anyi bila ya pingamizi wala kizuizi, isipokuwa kutapatapa kwa wananchi wasiokuwa na silaha.

Anasema Nicholas Sparekman “Sisi Wamerekani tunaweza kutekeleza matakwa yetu na kuyalazimisha kwa wale wasiokuwa na nguvu kwa njia yoyote ile, ikiwemo kutumia nguvu; kama vile vita vya kubomoa.”

Vile vile Leon Walsh anasema katika kitabu chake American strategic in world politics (Mbinu za Marekani katika siasa za ulimwengu)

“Wajibu wetu ni kutekeleza maongozi yetu ya sawa kwa nguvu duniani, kisiasa kiuchumi na kijamii. Na hilo sio jambo lenye muda maalum tu bali ni lazima kuendele haifai kuliacha.”

Hakuna siri ya kujifaharisha huku kwa maadui wa Mwenyezi Mungu na kudhihirisha uchokozi kwa waja wa Mwenyezi Mungu bila ya kujali, isipokuwa kutohofia nguvu yoyote ya kujikinga ambayo italiinua neno la Mwenyezi Mungu na kuiweka chini batili.

Viongozi wa Marekani wametekeleza yaliyoandikwa katika Kitab hicho na kukichikulia kama ni Injil yao takatifu badala ya Kitab cha Mwenyezi Mungu.

Wametekeleza njia zote za nguvu na za kuumiza, ikiwa ni pamoja na vita vyenye kuangamiza ili watekeleze matakwa yao kwa wale wasiokuwa na nguvu; wakatupa makombora ya kuunguza kwa watoto, vikongwe na waja wazito na wakatupa mabomu ya sumu kwenye nyenzo za riziki na uhai, wakiwemo wanyama na mimea ili waliobaki wafe kwa njaa.

Ni kwa lengo hilo ndipo Marekani ikaanzisha ngome za mauti katika ardhi yake, wakaanzisha humo uchunguzi wa kutafuta mikrobu kali zitakazoma- liza maisha ya binadamu, wanyama na mimea, na kwa ajili ya kutafuta gesi inayoondoa akili na kulemaza mishipa.

Kuna ajabu gani baada ya hayo yote kwa Marekani kuanzisha ngome ya mauti na kuweka silaha za kuharibu katika ardhi ya Palestina na kuipa jina la taifa la Israil? Hapana ajabu! Isipokuwa ajabu ni kwa madola, yakiwemo mataifa madogo yaliyo dhaifu, kuitambua ngome hii iliyosimamishwa kwa msingi ya uadui kwa binadamu wote, na kuwa na mwakilishi anyeitetea na kuangalia masihi yake katika Umoja wa Mataifa.

Pamoja na yote hayo, sisi hatukati tamaa kabisa kuwa iko siku haki itashin- da na batili itashindwa, Hicho kilio dhidi ya wachokozi kinasikika kila mahali ulimwenguni; hata katika Amerika. Huyu hapa mwananchi wa Vietnam ameiangamiza haiba ya Wamerekani, na kuua maelfu ya wanajeshi wao na kuwalazimisha kupoteza mabilioni ya dola zao1.
Na chochote mtakachotoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, mtarudishiwa, wala nyinyi hamtadhulumiwa.

Hii ni kuhimiza kutoa mali ambayo hapana budi kuitoa ili kuandaa nguvu na kujikinga. Yametangulia malezo katika Juz.2 (2:196) na mwanzo wa Juz.4 (3:92)

Na kama wakielekea kwenye amani, nawe ielekee, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ni mwenye kujua.

Amani ni ya ujumla, ikiwa ni pamoja na kusimamisha vita na suluhu, kutoa kodi na kusilimu. Kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu kumwambia Mtume wake ‘nawe ielekee’ ni amri ya lazima ya kumpa amani mwenye kutaka amani, vyovyote atakavyokuwa, ila kukiwa na dalili mkato kuwa amani yake ni vitimbi na maandalizi ya uvamizi na kuvunja mkataba.

Ni lazima ifahamike kuwa makusudio ya amani katika Aya hii ni amani ya wote, mwenye kupigana na asiyepigana. Wala sio amani ya pande zinazozana tu; kama vile kuishi kwa amani baina ya Urusi na Marekani ambako nyuma yake kuna mipango ya njama na mapinduzi katika mataifa yasiyofungamana na upande wowote, na kupinga ukombozi katika Asia,

Afrika na Latin Amerika, ili wazidishe faida katika mashirika yao ya kilanguzi kupitia damu ya wazalendo, chakula chao na mustakbali wao.

Utauliza: Mwenyezi Mungu (swt) katika Aya anasema: ‘Wakielekea kwenye amani nawe ielekee, na katika Aya nyingine anasema:

فَلَا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنْتُمُ الْأَعْلَوْنَ وَاللَّهُ مَعَكُمْ {35}

“Basi msilegee na kutaka amani na hali nyinyi mko juu, na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi” (47:35)

Je, kuna wajihi gani wa kujumuisha Aya hizi mbili?

Jibu: Hakuna kupingana baina ya Aya hizi. Aya ya kwanza inawaamrisha waislamu kumpa amani mwenyewe kutoa amani na Aya ya pili inawataka wawe na moyo wa kupigana wakazane na wasilegee wakamkimbia adui. Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi’.

Kwa hiyo Aya hii: “Basi msilegee” ni sawa na Aya isemayo:

وَلَا تَهِنُوا فِي ابْتِغَاءِ الْقَوْمِ ۖ إِنْ تَكُونُوا تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمُونَ ۖ وَتَرْجُونَ مِنَ اللَّهِ مَا لَا يَرْجُونَ ۗ {104}

Wala msilegee katika kuwafuatia hao watu. ikiwa mnaumia basi na wao wanaumia kama mnavyoumia nyinyi. Na nyinyi mwataraji kwa Mwenyezi Mungu ambayo wao hawayataraji”
Juz.5 (4:104)

Na kama wakitaka kukuhadaa, basi Mwenyezi Mungu atakutoshelezea. Yeye ndye aliyekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.

Mtume anaambiawa kuhusu hao walioelekea kwenye amani; kuwa kama wanakupangia njama za uhaini nyuma ya mwelekeo wao wa amani, basi usiogope njama zao. Wewe uko katika amani ya Mwenyezi Mungu na atakutosheleza na shari yao naye amekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.

Utauliza: Punde tu, yamepita maelezo ya kauli yake Mwenyezi Mungu akimwamrisha Mtume wake kuvunja mapatano ikiwa anahofia kwao hiyana na hadaa. Na katika Aya hii anamwamrisha kuwakubalia wakitaka amani bali hata kama wanataka kufanya hiyana. Je, kuna wajihi gani?

Jibu: Kule Mwenyezi Mungu, alimwamrisha kuvunja mapatano akiwa na yakini na kujua hiyana zao, kwa kumdhihirikia alama. Na, hapa ameamrishwa kuwapa amani hata kama wanakusudia hiyana, ikiwa hakuna dalili mkato za njama zao isipokuwa uwezekano tu wa hilo. Katika hali hii Mtume atachukulia dhahiri na kuamiliana nao kulingana na dhahiri. Kwani dhahiri ni ya watu na batini ni ya Mwenyezi Mungu.

Na akaziunganisha nyoyo zao; lau ungelitoa yote yaliyomo ardhini usingeliweza kuiunganisha mioyo yao, lakini Mwenyezi Mungu amewaunganisha. Hakika yeye ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.

Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeunganisha nyoyo za masahaba baada ya kuwa na uhasama uliozoeleka; hasa baina ya Ausi na Khazraj ambao uliendelea kiasi cha miaka 120.

Vile vile hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu (swt) hupitisha mambo kulingana na desturi, kanuni, sababu na visababishi vyake. Sababu ya kuunganisha nyoyo za masahaba wa Mtume Muhammad ni Uislamu na imani yao kinadharia na kimatendo. Na, Uislamu unatoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo imesihi kunasibishiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Tumesema katika kufasiri Aya ya pili ya Sura hii kwamba dini haioteshi ngano isipokuwa inaotesha penzi na ikhlasi. Mfano wa Aya hii, tunayoifasiri, ni kama Juz.4 (3:103). Huko utakuta tafsiri yake kwa ufafanuzi.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ {64}

Ewe Mtume! Mwenyezi Mungu anakutosheleza wewe na wale waliokufuata katika waumini.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلَى الْقِتَالِ ۚ إِنْ يَكُنْ مِنْكُمْ عِشْرُونَ صَابِرُونَ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ ۚ وَإِنْ يَكُنْ مِنْكُمْ مِائَةٌ يَغْلِبُوا أَلْفًا مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَا يَفْقَهُونَ {65}

Ewe Nabii! Wahimze waumini wende vitani; wakiwepo miongoni mwenu ishirini wenye subira, watashinda mia mbili; na kama wakiwa mia moja miongoni mwenu watawashinda elfu moja katika waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu.

الْآنَ خَفَّفَ اللَّهُ عَنْكُمْ وَعَلِمَ أَنَّ فِيكُمْ ضَعْفًا ۚ فَإِنْ يَكُنْ مِنْكُمْ مِائَةٌ صَابِرَةٌ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ ۚ وَإِنْ يَكُنْ مِنْكُمْ أَلْفٌ يَغْلِبُوا أَلْفَيْنِ بِإِذْنِ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ مَعَ الصَّابِرِينَ {66}

Sasa Mwenyezi Mungu amewahafifishia na anajua kuwa kuna udhaifu miongoni mwenu. Kwa hiyo wakiwa mia moja miongoni mwenu wenye subira watawashinda mia mbili, na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu watawashinda elfu mbili kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.
  • 1. Kumbuka mwandishi aliandika kitabu hiki katika miaka ya sitini