read

Aya 58 – 59: Wanapopewa Huridhia

Maana

Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka.

Dhamir ya miongoni mwao inawarudia wanafiki. Maana ni kuwa baadhi ya wanafiki walikuwa wakimsema Mtume (saw) na kumtia ila katika kugawa kwa kudai kuwa anapendelea.

Katika Tafsir Tabari imepokewa kutoka, kwa Said Al-Khudri, amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipokuwa akigawa mafungu, alijiwa na Ibn Dhulkhuwayswara Tamimi, akasema: Fanya uadilifu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume akasema: Ole wako! Ninani atafanya uadilifu ikiwa mimi sikufanya? Umar akasema: Niruhusu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nikate shingo yake. Mtume (saw) akasema: Mwache yeye ana wenzake ambao mmoja wenu atadharau kuswali nao na kufunga nao, watachomoka katika dini kama unavyochomoka mshale kwenye upinde; alama yao ni mtu mweusi1, moja ya mikono yake ni kama titi la mwanamke” Ndipo ikashuka: ‘Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka’.

Anaendelea kusema Abu Said: Ninashuhudia kuwa mtume alisema haya na nashuhudia kuwa alipouawa Ali (rehema za Mwenyezi Mungu ziwe kwake) aliletwa mtu aliyekuwa na sifa hizo”

Na wanapopewa katika hizo huridhika, na wasipopewa katika hizo huchukia.

Mtume alikuwa akigawanya sadaka, kama alivyobainisha Mwenyezi Mungu. Waumin walikuwa wakiridhia na wanafiki wakichukia na kumlaumu katika kugawanya kwake.

Aya inamchanganya kila asiyeridhia fungu lake. Lau watu wote wangeliridhia wanayostahiki, watu wote wangeliishi katika amani na raha.

Na lau wangeliridhia kile alichowapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila zake, na Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu kututoshea na sadaka na mengineyo ya kuwahitajia watu.

Aya hii inahimiza mtu kujizuilia na vilivyo mikononi mwa watu, kumtege- mea Mwenyezi Mungu na kula jasho lake.
Imam AIi (as) anasema: “Utajiri mkubwa ni kutokuwa na tamaa na vilvyo mikononi mwa watu”.
Sijui kama kuna anayestahiki kudharauliwa kuliko yule anayetarajia watu na huku anaweza kujitosha nao japo kwa subira.

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِنَ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {60}

Hakika sadaka ni ya (hawa) tu: Mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao Na kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na mwana njia. Ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua mwenye hekima.
  • 1. Ieleweke kuwa mtu mweusi si lazima awe mwafrika, hata kwa warabu na wengineo pia kuna weusi -Mtarjumu