read

Aya 60: Wanastahiki Zaka

Maana

Makusudio ya sadaka hapa ni zaka ya wajibu. Mafakihi wameizungumzia zaka, hukumu zake, sharti zake, vitu ambavyo ni wajibu vitolewe zaka na wenye kustahiki kupewa. Sisi tumezungumzia kwa ufafanuzi katika Kitab Fiqhul-Imam Jaffer Assadiq J2. Katika Juz. 3 (2:272) tumeizungumzia zaka kama msimamo uliothibitishwa na Uislamu.

Hapa tutazungumzia aina nane za wanaostahiki kupewa zaka kulingana na Aya tukufu:

1. Hakika Sadaka Ni Ya(Hawa) Tu. Mafukara:

Shia Imamia wanasema: Fukara wa kisharia ni yule asiyemiliki gharama yake ya mwaka na ya watoto wake. Hanafi wanasema ni yule anayemiliki chini ya kiwango cha zaka. Shafii na Hambal wanasema mwenye kupata nusu ya mahitaji yake hahisabiwi kuwa fukara. Shia Imamia, Shafii na Hambal wanasema: Mwenye kuweza kuchuma si halali kwake zaka, lakini Hanafi na Malik wamesema ni halali.

2. Na Masikini.

Wamesema jamaa, kuwa neno fukara na maskini yakiwa pamoja kila moja linakuwa na maana nyingine; na yakiwa mbali mbali basi yanakuwa na maana moja. Wakasema tofauti ni kuwa fukara haombi na maskini huomba. Vyovyote iwavyo la kuzingatia ni haja, na wote ni wahitaji.

3. Na Wanaozitumikia.

Ni wale wanaokusanya zaka, waliowekwa na Imam au naibu wake, kusimamia kukusanya zaka na kuihifadhi; kisha kuitoa kwa atakayeigawanya kwa anayestahiki. Kile wakichukuacho wakusanyaji kinazingatiwa kuwa ni malipo ya kazi yao, sio sadaka. Kwa hiyo wanapewa hata kama ni matajiri.

4. Na Wanaotiwa Nguvuu Nyoyo Zao.

Ni wale wanaovutiwa kwenye Uislamu au wanatakiwa msaada na Waislamu kwa manufaa ya Uislamu.

5. Na Kuwakomboa Watumwa.

Yaani inatolewa zaka kwa ajili ya kuwakomboa watumwa wawe huru. Mambo haya hayako siku hizi.

6. Na Wenye Madeni

Ni wale walio na madeni yanayowashinda kuyalipa watapewa zaka, kwa sharti yakuwa wawe hawakutumia madeni hayo katika dhambi.

7. Na Katika Njia Ya Mwenyezi Mungu

Njia ya Mwenyezi Mungu ni kila analoliridhia ambalo hutakiwa kujikurubisha kwake, kwa namna yoyote itakavyo kuwa, kama vile kutegeneza njia, kujenga zahanati au vyuo. Bora zaidi ni kutoa katika kupigania dini na nchi.

8. Na Mwana Njia

Huyo ni msafiri aliyeishiwa njiani, atapewa kiasi kitakachomfikisha kwao; hata kama ni tajiri, kwa sharti ya kuwa safari yake isiwe ya maasi.

وَمِنْهُمُ الَّذِينَ يُؤْذُونَ النَّبِيَّ وَيَقُولُونَ هُوَ أُذُنٌ ۚ قُلْ أُذُنُ خَيْرٍ لَكُمْ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَيُؤْمِنُ لِلْمُؤْمِنِينَ وَرَحْمَةٌ لِلَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ ۚ وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ رَسُولَ اللَّهِ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {61}

Na miongoni mwao wako wanaomuudhi Mtume na kusema: Yeye ni sikio tu. Sema: ni sikio la heri kwenu. Anamwamini Mwenyezi Mungu na ana imani na waumini. Na ni rehema kwa wale wanaoamini miongoni mwenu. Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu wana adhabu iumizayo.

يَحْلِفُونَ بِاللَّهِ لَكُمْ لِيُرْضُوكُمْ وَاللَّهُ وَرَسُولُهُ أَحَقُّ أَنْ يُرْضُوهُ إِنْ كَانُوا مُؤْمِنِينَ {62}

Wanawaapia Mwenyezi Mungu ili wawaridhishe na hali Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha, ikiwa wao ni waumini.

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّهُ مَنْ يُحَادِدِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَأَنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدًا فِيهَا ۚ ذَٰلِكَ الْخِزْيُ الْعَظِيمُ {63}

Je, Hawajui kuwa anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata moto wa Jahanamu adumu humo? Hiyo ni hizaya kubwa.