read

Aya 61-63: Wanasema Yeye Ni Sikio Tu

Maana

Na miongoni mwao wako wanaomuudhi Mtume na kusema: Yeye ni sikio tu.

Mtume (saw) alikuwa akiwachukuliwa wote kwa dhahiri yao, bila ya kumtafuta mtu undani wake, kwa kuchukulia msingi wa kuwa dhahiri ni ya watu na undani ni wa Mwenyezi Mungu.

Hiyo ni miongoni mwa misingi ya Kiislamu ya sharia inayochukuliwa hukumu nyingi. Waliitumia wanafiki; wakawa wanaepuka kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakitoa udhuru na Mtume akiwakubalia.

Ajabu ni kwamba wao walitumia fadhila hii kuwa ni njia ya kumtukana na kumnasibisha kuwa anakubali haraka kila analolisikia bila ya kufikiria na kupambanua lipi la kukubalia na lipi la kukataa.

Lau kama Mtume angeliwakubalia kwa uwongo wao na unafiki wao, na kuwapa adhabu inyostahili, basi ingelikuwa shari kwao na wangelisema ni mwenye moyo mgumu na mwenye hasira.

Hiyo ndiyo ajabu kumwaibisha na lile lenye manufaa yanayowarudia wao! Lakini mwenye kulaumu hilo si ajabu kwake. Kwa vile anaangalia kila kitu kwa kioo cha nafsi yake kilicho cheusi; hata yule anayemfanyia wema pia.Amesema kweli yule aliyesema: “Asiyejua kizuri si mzuri yeye”.

Sema: ni sikio la heri kwenu.

Hili ni jibu la Mwenyezi Mungu kwa hao wanafiki. Kwa ufupi ni kwamba mtume ni sikio la heri sio la shari. Anawakubalia yale yasiyo na mad- hara kwa mtu na anakataa yaliyo na madhara; kama vile kusengenya na kufitini.
Anamwamini Mwenyezi Mungu na ana imani na waumini.

Yaani anawasadiki wakweli, kusadiki kwa kukinai. Ama wanafiki anawasadiki katika ambayo hapana madhara kuyasadiki.

Na ni rehema kwa wale wanaoamini miongoni mwenu.

Haya yanaungana na sikio la heri. Hiyo ni katika kuunganisha jumla kwenye mahsusi. Kwa sababu sikio la heri ni rehema vile vile.

Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu wana adhabu iumizayo.

Kwa sababu mwenye kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu ndio amemuudhi Mwenyezi Mungu.

Wanawaapia Mwenyezi Mungu ili wawaridhishe na hali Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha, ikiwa wao ni waumini, kama wanavyodai.

Maneno ya wanawaapia na kuwaridhisha yanaelekezwa kwa Mtume na waumini. Mwenyezi Mungu amewapa habari katika Aya hii kwamba wanafiki walipojua kuwa mmewagundua waliwahofia; wakakimbilia viapo vya uwongo. Afadhali wao wangemridhisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa toba na ikhlasi.

Kuna hadith isemayo: “Mwenye kuapa kiapo cha uwongo, akiwa anajua kuwa yeye ni mwongo, basi amejitokeza kupambana na Mwenyezi Mungu”.

Ibara ya kusema ‘ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha’, badala ya ndio wenye haki zaidi ya kuwaridhisha,’ ni kufahamisha kua kumridhisha Mtume ndio kumridhisha Mwenyezi Mungu; kama ambavyo kumuudhi ndiko kumuudhi yeye pia.

Je, Hawajui kuwa anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata moto wa Jahanamu adumu humo? Hiyo ni hizaya kubwa.

Aya hii ni msisitizo wa Aya iliyotangulia. Sheikh Ismail Haqi anasema, katika tafsiri yake Rawhul Bayan: “Kila Mtume aliudhiwa kiasi kisichosemeka, na Muhammad (saw) alikuwa ni zaidi; kama alivyosema mwenyewe: Hakuudhiwa Mtume kama nilivyoudhiwa mimi.”

Kwa kuwa kuudhiwa ni sababu ya kuimarika, basi maana ni kuwa hakuna Mtume aliyeimarika kuliko yeye. Hasan alipewa sumu na Husein akachinjwa kwa sababu ukamilifu ulikuwa ukiwakabili kwa kufa shahidi.

Mtume (saw) alikuwa anaweza kuwaokoa kwa kuwaombea, lakini aliona ukamilifu wa daraja yao ulikuwa na nguvu kuliko kuokolewa; kiasi ambacho Mtume alimpa mmoja wa wakeze chupa mbili na kumwambia, kama moja ikiwa rangi ya njano, basi Hasan atakuwa amekufa shahidi kwa kupewa sumu; na kama nyingine ikiwa nyekundu basi Husein atakuwa shahidi kwa kuchinjwa. Na kweli hayo yakawa”.

يَحْذَرُ الْمُنَافِقُونَ أَنْ تُنَزَّلَ عَلَيْهِمْ سُورَةٌ تُنَبِّئُهُمْ بِمَا فِي قُلُوبِهِمْ ۚ قُلِ اسْتَهْزِئُوا إِنَّ اللَّهَ مُخْرِجٌ مَا تَحْذَرُونَ {64}

Wanaogopa wanafiki kuteremshiwa sura itakayowatajia yaliyomo nyoyoni mwao. Sema: Fanyeni mzaha tu, hakika Mwenyezi Mungu atayatoa mnayoyaogopa.

وَلَئِنْ سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنْتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ {65}

Na ukiwauliza, kwa hakika watasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na kuchezea tu. Sema: Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Mwenyezi Mungu na Aya zake na Mtume wake?

لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُمْ بَعْدَ إِيمَانِكُمْ ۚ إِنْ نَعْفُ عَنْ طَائِفَةٍ مِنْكُمْ نُعَذِّبْ طَائِفَةً بِأَنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ {66}

Msitoe udhuru, mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu. Tukisamehe kundi moja miongoni mwenu tutaliadibu kundi jingine kwa vile wao walikuwa wakosefu.