read

Aya 64 – 66: Anakutosheleza Mwenyezi Mungu

Maana

Ewe Mtume! Mwenyezi Mungu anakutosheleza wewe na wale waliokufuata katika waumini.

Imesemekana kuwa maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu anakutosha wewe Muhammad na pia anawatoshea waumini waliokufuata. Ama sisi tunaelemea kwenye kauli ya aliyesema kuwa maana yake ni: Ewe Muhammad! Anakutosha Mwenyezi Mungu na waumini kwa Utume wako. Dalili yetu katika hilo ni Aya iliyotangulia (62): Basi Mwenyezi Mungu atakutoshelezea.

Yeye ndiye aliyekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.” Aya hii inaeleza wazi kuwa Mwenyezi Mungu na waumini walimsaidia Muhammad, basi ni hivyo hivyo “Anakutoshelezea wewe Mwenyezi Mungu na wale waliokufuata katika waumini.”

Vyovyote iwavyo, makusudio ni kumtuliza Mtume kwamba vita vyake na makafiri vimedhaminiwa katika hali yoyote ile. Kwa sababu nguvu inayomsaidia haishindiki.

Ewe Nabii! Wahimze waumini wende vitani; wakiwepo miongoni mwenu ishirini wanaosubiri, watashinda mia mbili; na kama wakiwa mia moja miongoni mwenu watawashinda elfu moja katika waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Mtume wake washujaishe na vita Ewe Muhammad, watu wako, na uwape habari kwamba wao ni kufu ya maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zao, hata kama watazidi zaidi ya mara kumi. Hilo ni kwa kuwa waumini wanafahmu amri ya Mwenyezi Mungu na wanaitakidi siku ya mwisho; na kwamba heri itapatikana kwa jihadi na kufa shahidi. Kwa hiyo wanakwenda kwa nia njema. Ama makafiri hawafahmu amri ya Mwenyezi Mungu wala hawaitakidi ahadi. Kwa hali hii wao wanabania maisha yao.

Sasa Mwenyezi Mungu amewahafifishia na anajua kuwa kuna udhai- fu miongoni mwenu. Kwa hiyo wakiwa mia moja miongoni mwenu wenye subira watawashinda mia mbili, na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu watawashinda elfu mbili kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

Wafasiri na mafakihi wamerefusha maneno kuhusu Aya hii. Kuna waliosema kuwa Aya hii ni Nasikh (inayofuta hukumu) ya Aya iliyotangulia ambayo imemlazimisha Mwislamu asiwakimbie watu kumi. Wengine wakasema ilikuwa uzito kwa Waislamu kukabili mmoja kwa kumi, ndipo ikaja tahfifu hiyo. Mafakihi nao kwa kutegemea Aya hi wamefutu kuwa ni haramu kukimbia vitani ila ikiwa idadi ya jeshi la adui ni maradufu ya idadi ya jeshi la Waislamu.

Katika kufasiri Aya 15 katika Sura hii, tumebainisha kuwa mafakihi hawana fatwa katika suala hili; na kwamba anachiwa suala hili, kamanda mkuu peke yake mwenye ujuzi na mwaminifu.

Kwa ajili hii tunatilia nguvu kuwa Aya mbili hizi na ile iliyo kabla yake, hazikuja kubainisha hukumu ya kukimbia, isipokuwa zinahusika na Mtume na sahaba zake tu; na Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi wa makusudio yake.

مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَنْ يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ ۚ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّهُ يُرِيدُ الْآخِرَةَ ۗ وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {67}

Haimfalii Nabii yoyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda sawasawa katika ardhi. Mnataka vitu vya dunia Na hali Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

لَوْلَا كِتَابٌ مِنَ اللَّهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ {68}

Lau isingelikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka ingeliwapata adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.

فَكُلُوا مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلَالًا طَيِّبًا ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {69}

Basi kuleni katika vile mlivyoteka ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لِمَنْ فِي أَيْدِيكُمْ مِنَ الْأَسْرَىٰ إِنْ يَعْلَمِ اللَّهُ فِي قُلُوبِكُمْ خَيْرًا يُؤْتِكُمْ خَيْرًا مِمَّا أُخِذَ مِنْكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {70}

Ewe Nabii! Waambie wale mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi Mungu akijua heri yoyote nyoyoni mwenu, basi atawapa bora kuliko vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

وَإِنْ يُرِيدُوا خِيَانَتَكَ فَقَدْ خَانُوا اللَّهَ مِنْ قَبْلُ فَأَمْكَنَ مِنْهُمْ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {71}

Na kama wanataka kukufanyia hiyana, basi walikwishamfanyia hiyana Mwenyezi Mungu kabla, na akakupa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.