read

Aya 64 – 66: Wanaogopa Wanafiki

Maana

Wanaogopa wanafiki kuteremshiwa sura itakayowatajia yaliyomo nyoyoni mwao. Sema: Fanyeni mzaha tu, hakika Mwenyezi Mungu atayatoa mnayoyaogopa.

Wanafiki hawakuogopa hasa kushukiwa na wahyi kuwahusu wao, isipokuwa walidhihirisha hadhari kwa njia ya dharau na stihzai – walikuwa wakimbeza Mtume (saw) huku wakiambizana kwa dharau: Angalieni, msije mkateremshiwa Sura!

Kwa upande mwingine wanafiki hawaamini wahyi, vipi watauogopa kiuhakika? Wafasiri wengi wamesma kuwa dhamiri katika ‘kuteremshiwa’, inawarudia waumini, na ile ya nyoyoni mwao inawarudia wanafiki. Lakini hayo yako mbali kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, waumini hawakutajwa katika Aya na kwamba waliotajwa wazi- wazi ni wanafiki; kama ambavyo Aya iliyotangulia imewataja wao tu.

Pili, katika kufasiiri hivi, itabidi kuweko kutopatana dhamiri jambo amba- lo halina dalili.

Kwa ajili hii tunatilia nguvu kauli ya anayesema kuwa dhamiri zote zinawarudia wanafiki. Kwa hiyo maana yanakuwa wanaogopa kwa dharau, wanafiki kuteremshiwa Sura itakayofichua uadui wao kwa Uislamu na waislamu.

Mwenyezi Mungu naye akawapa kiaga cha kuwa Sura itakyowafichua itashuka tu, na itawakabili wao ana kwa ana; waombe msamaha usifae msamaha wao.

Na ukiwauliza, kwa hakika watasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na kuchezea tu.

Jamaa katika wanafiki walisema yale yasiyostahiki kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Alipowauliza walisema tulikuwa tunafanya mchezo tu.

Wafasiri wametofautiana kuhusu majina ya walio sema hayo na aina ya maneno waliyoyasema. Aya haidokezi chochote katika hayo; nasi tunanya- maza kama alivyowanyamazia Mwenyezi Mungu.

Sema: Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Mwenyezi Mungu na Aya zake na Mtume wake?

Kusema kwao kuwa tulikuwa tukichezea ni kubaya zaidi kuliko dhambi waliyoitakia msamaha. Je, Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka ukuu wake ni wakufanyiwa mchezo? Je, amewatuma Mitume wake waje wachezewe? Aya inafahamisha kwamba kila mwenye kuifanyia mchezo dini na huku- mu yake yenye kuthibiti kwa uwazi basi huyo ni kafiri.

Msitoe udhuru, mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu.

Utauliza: Je, si hii inafahamisha kuwa wao walikuwa waumin kabla ya kufanya mzaha; na kwamba sababu ya kuyawajibisha ukafiri wao ni istihzai; na inajulikana kwamba wao walikuwa makafiri kabla; na huo ukafiri wao ndio sababu ya mchezo wao?

Jibu: Kabla ya kukiri kwao kuifanyia mchezo dini walikuwa ni makafiri kwa hali halisi, lakini walikuwa ni waislamu kihukumu. Kwa sababu wao walidhihirisha Uislamu. Kwa hiyo zikawapitia hukumu za waislam ambazo zinaangalia dhahiri sio hali halisi.
Mara tu baada ya kukiri kwao kuifanyia mchezo dini wamekuwa ni makafiri kwa hali halisi na kwa kihukumu, wakiwa sasa kwenye hukumu ya waliortadi.

Tukisamehe kundi moja miongoni mwenu tutaliadhibu kundi jingine kwa vile wao walikua wakosefu.

Wanafiki walikuwa aina mbili: Viongozi wanaofuatwa ambao wana utakia mabaya Uislamu, kumfanyia vitimbi Mtume wake na kumchezea. Kundi jingine ni wale madhaifu wanaofuata.

Ndipo akamwamrisha Mwenyezi Mungu (swt) Mtume wake mtukufu kuwasamehe hao wanyonge kwa unyonge wao na kuwaadhibu wale wengine.

Kwa sababu wao ndio sababu. Inasemekana kuwa Mwenyezi Mungu aliwasamehe waliotubia na kuwaadhibu waliog’ang’ania ukafiri na unafiki.

الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُمْ مِنْ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمُنْكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ وَيَقْبِضُونَ أَيْدِيَهُمْ ۚ نَسُوا اللَّهَ فَنَسِيَهُمْ ۗ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ هُمُ الْفَاسِقُونَ {67}

Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja. Wanaamrisha maovu na kukataza mema na wanafumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu na yeye amewasahau. Hakika wanafiki ndio mafasiki.

وَعَدَ اللَّهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْكُفَّارَ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ هِيَ حَسْبُهُمْ ۚ وَلَعَنَهُمُ اللَّهُ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُقِيمٌ {68}

Amewaahidi Mwenyezi Mungu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahanam hali ya kudumu humo.Ni tosha yao. Na Mwenyezi Mungu amewalaani. Na wana wao adhabu ya kudumu.

كَالَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ كَانُوا أَشَدَّ مِنْكُمْ قُوَّةً وَأَكْثَرَ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا فَاسْتَمْتَعُوا بِخَلَاقِهِمْ فَاسْتَمْتَعْتُمْ بِخَلَاقِكُمْ كَمَا اسْتَمْتَعَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ بِخَلَاقِهِمْ وَخُضْتُمْ كَالَّذِي خَاضُوا ۚ أُولَٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ {69}

Ni kama wale waliokuwa kabla yenu. Walikuwa na nguvu zaidi kuliko nyinyi na mali nyingi na watoto. Basi walistarehea sehemu yao, na nyinyi mwastarehea sehemu yenu kama walivyostarehe kwa sehemu yao wale waliokuwa kabla yenu na mkazama (katika batili) kama walivyozama. Hao zimeporomoka amali zao katika dunia na akhera. Na hao ndio waliopata hasara.

أَلَمْ يَأْتِهِمْ نَبَأُ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ قَوْمِ نُوحٍ وَعَادٍ وَثَمُودَ وَقَوْمِ إِبْرَاهِيمَ وَأَصْحَابِ مَدْيَنَ وَالْمُؤْتَفِكَاتِ ۚ أَتَتْهُمْ رُسُلُهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ ۖ فَمَا كَانَ اللَّهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَٰكِنْ كَانُوا أَنْفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ {70}

Je, hazikuwafikia habari za wale walio kuwa kabla yao, kaumu ya Nuh na Ad na Thamud na kaumu ya Ibrahim na watu wa Madyan na miiji iliyopinduliwa. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.