read

Aya 67 – 70: Wanafiki Wanaume Na Wanawake

Maana

Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja.

Hilo ni fumbo la kufanana kwao kisifa na kimatendo. Kisha akabainisha jinsi walivyofanana, kwa kauli yake:

Wanaamrisha maovu na kukataza mema na wanafumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu na yeye amewasahau.
Maovu waliyoyamrisha ni ukafiri na unafiki; na wema walioukataza ni imani na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ama mikono yao wameifunga kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kumsahau Mwenyezi Mungu ni kuacha kwao kumtii; na yeye kuwasahau ni kuwanyima rehema yake.

Hakika wanafiki ndio mafasiki wenye kuacha njia ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema na kufuata njia ya shetani.

Amewaahidi Mwenyezi Mungu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahanam hali ya kudumu humo.

Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu (swt) maovu ya wanafiki, aliwa- pa kiaga na kumpa kiaga kila kafiri moto wa Jahanam.

Ni tosha yao

Yaani malipo yanatoshana na matendo yao

Na Mwenyezi Mungu amewalaani Amewaweka mbali na rehema yake. Na wana wao adhabu ya kudumu Haipungui wala kukatika

Ni kama wale waliokuwa kabla yenu. Walikuwa na nguvu zaidi kuliko nyinyi na mali nyingi na watoto. Basi walistarehea sehemu yao, na nyinyi mwastarehea sehemu yenu kama walivyostarehea sehemu yao wale waliokuwa kabla yenu na mkazama (katika batili) kama walivyozama.

Mwenyezi Mungu (swt) anawambia: Enyi wanafiki mlio wakati wa Muhammad! Ni sawa na wanafiki waliopita. Walistarehe na maraha ya dunia, tena walikuwa na nguvu, mali na watoto kuliko nyinyi; basi na nyinyi stareheni na mmezama katika batili kama walivyozama.

Hao zimeporomoka amali zao katika dunia na akhera.

Yaani mema yao yamebatilika, ikiwa wanayo, kama vile kuishi kwa jasho lao. Kubatilika katika akhera ni kutolipwa hayo. Ama kubatilika kwake duniani ni kwamba hilo si chochote kwa makafiri na manafiki mbele za watu wenye mwamko na imani.

Na hao ndio waliopata hasara

Kwa vile wao wamejichokesha kupanga njama kwa waumini wema, kisha ubaya wa dunia na akhera ukawarudia wao. Kwa ufupi ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) aliwaaambia wanafiki waliokuwa wakati wa Mtume (saw). Acheni ukafiri na unafiki na chukueni funzo kwa wale waliokuwa kabla yenu kabla ya kuchukua funzo watakao kuja baada yenu.

Je, hazikuwafikia habari za wale walio kuwa kabla yao, kaumu ya Nuh na Ad na Thamud na kaumu ya Ibrahim na watu wa Madyan na miiji iliyopinduliwa.

Watu wa Madyan ni kaumu ya Shuaib, na wa miji iliyopinduliwa ni kaumu ya Lut.

Mwenyezi Mungu (swt) anawakumbusha wanafiki kuhusu watu hawa, kwa sababu miji yao ilikuwa karibu na miji ya waarabu; nao walikuwa na mali nyingi na watoto:

Watu wa Ibrahim waliangamizwa kwa kunyang’a nyangwa neema, wa Adi kwa upepo, wa Nuh kwa gharika, wa Thamud kwa ukelele, na wa Madyan kwa adhabu ya wingu, na wale wa miji iliyopinduliwa ni kwa kupinduliwa juu chini. Yametangulia maelezo ya hayo katika sura ya 7.

Basi Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe kwa kung’anga’ania kwao makosa na dhambi.

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّهُ ۗ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {71}

Na waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao. Huamrishana mema na kukatazana maovu. Na husimamisha swala. Na hutoa zaka. Na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

وَعَدَ اللَّهُ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ۚ وَرِضْوَانٌ مِنَ اللَّهِ أَكْبَرُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ {72}

Amewaahidi Mwenyezi Mungu waumini wanaume na waumin wanawake bustani (Pepo) zipitazo mito chini yake; hali ya kudumu humo na maskani mema katika mabustani ya milele. Na radhi za Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi. Huko ndiko kufuzu kukubwa.