read

Aya 67 – 71: Kateka

Maana

Haimfalii Nabii yoyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda sawa-sawa katika ardhi.

Wameafikiana wafasiri kwamba Aya hii imeshuka kuhusu mateka wa Badr. Dhahir ya mfumo inafahamisha hivyo. Wametofautiana katika tafsir yake, nasi tutaileta kwa njia ya swali na jawabu:

Ikiwa kuna vita baina ya Waislamu na waabudu masanamu. Na, Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mwislamu kwa kafiri, je, ni wajibu kwa Mwislamu kumuua kafiri huyo? Au inajuzu kumchukua mateka? Na kama akimchukua mateka, je iko hiyari kwa Mtume baina ya kumuua na kumwacha kwa fidia? Na kumwacha bila ya fidia?

Jibu ni lazima lifafanuliwe katika hali mbili: Kwanza, ni kutokea vita baada ya dini kuwa na nguvu katika ardhi na watu wake kuwa na nguvu kwa namna ambayo hila na vitimbi vya maadui haviwadhuru, kwa kuwa ipo nguvu ya kujikinga.

Katika hali hii, Mwislamu anayepigana, anahiyarishwa baina ya kuua na kuchukua mateka. Na akichukua mateka itakua hiyari kwa Mtume baina ya kuua mateka na kumwacha kwa fidia au bila ya fidia. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

فَإِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا فَضَرْبَ الرِّقَابِ حَتَّىٰ إِذَا أَثْخَنْتُمُوهُمْ فَشُدُّوا الْوَثَاقَ فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً {4}

“Basi mnapokutana vitani na wale waliokufuru wapigeni shingo mpaka mkiwashinda sawa sawa, hapo wafungeni pingu. Baadae waacheni kwa ihsani au kwa kujikomboa.” (47:4).

Siri katika hilo iko wazi, nayo ni kupatikana nguvu ya kujikinga.

Hali ya pili ni kutokea vita kabla dini haijamakinika vizuri na kuwa na nguvu katika ardhi. Hapo Mwislamu anayepigana, akimmudu kafiri anayepigana naye amuue sio kumchukua mateka. Siri ya hili ni kutia hofu moyo wa kila anayejaribu kutangaza vita dhidi ya waumini.

Haya yanafahamika kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Haimfalii Mtume kuwa na mateka mpaka ashinde sawasawa’ Yaani hakuna kuchukua mateka wa kikafiri mpaka dini iwe na nguvu kamili ya kujihami ambayo makafiri na mataghuti watakuwa chini yake.

Mnataka vitu vya dunia

Maneno haya yanaelekezwa kwa mwenye kuteka mateka kwa kukusudia ngawira na kuchukua fidia bila ya kujali kuharibika maisha yake katika ardhi.

Na hali Mwenyezi Mungu anataka Akhera.

Mwenyezi Mungu anawatakia waja wake malipo ya akhera kwa sababu ndiyo bora na yenye kubaki kuliko mapambo ya dunia.

Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

Anawapa nguvu waumini hata kama hawana mateka; na ni mwenye hekima katika kupanga mambo yake na amri yake na makatazo yake.
Lau isingelikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka ingeliwapata adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.

Ilitangulia hukumu ya Mwenyezi Mungu kuinusuru dini yake na Mtume wake pamoja na watu wachache aliokuwa nao Badr, na kuteswa makafiri, pamoja na wingi wao, kwa kuuliwa na kutekwa kwa mikono ya waumini.

Lau si kupitisha kwake huku Mwenyezi Mungu, wangeliadhibiwa waumini ambao waliwachukua mateka maadui wa Mwenyezi Mungu kwa tamaa ya kupata fidia. Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka jihadi na amali iwe ni kwa ajili yake yeye Mwenyezi Mungu tu.

Kuna hadith isemayo “… ambaye hijra (kuhama) yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hijra yake ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ambaye hijra yake ni kwa ajili ya kupata dunia au kuoa mwanamke, basi hijra yake ni kwa lile alilolihajira.”

Ilivyo ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hakubainisha aina ya adhabu ambayo angeliwapa wachukuaji mateka katika masahaba, lau si kupitisha alivyopitisha. Je, ilikuwa ni adhabu ya kidunia au ya kiakhera.

Utauliza: Ikiwa kuchukua mateka kulikuwa ni haramu kabla ya kushamiri dini yake Mwenyezi Mungu juu ya dini zote, ilikuwaje kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuwaruhusu masahaba siku ya Badr na akakubali kuchukua fidia kabla ya ushindi kamili? Na vita vya Badr vilikuwa ndio vya kwanza na kukafuatiwa na vita vilivyoendelea hadi mwaka wa kuchukuliwa Makka?

Wafasiri na wengineo wamedangana katika kujibu swali hili au mushkeli huu; na yakagongana maneno yao. Wengine wakajiachia na kusema ‘Mtume sio maasum aweza kukosa. Lakini hapana, hayuko hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye hatamki kwa hawa yake

Tunalotilia nguvu ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) alivua uharamu wa kuchukua mateka kwa kila mateka aliyeachwa huru na Mtume (saw) siku ya Badr. Wengi wao walisilimu na kuwa watu wazuri; bali hata walikuwemo waliochukuliiwa vitani kwa kulazimishwa.

Ibn Athir katika Tarikh yake J2 katika kifungu, vita kuu ya Badr, anasema: “Mtume (saw) aliwaambia sahaba zake siku hiyo: “Ninajuwa watu katika Bani Hashim na wengineo wametolewa kwa kulazimishwa. Kwa hiyo atakayekutana na yeyote katika Bani Hashim asimwue.”

Miongoni mwa mateka alikuwemo Suhail bin Amr. Umar bin Al-Khattab akasema. “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Acha nimwue asije akakuudhi.”

Mtume akasema: “Mwache atakuwa na jambo utakalomsifia.” Mateka mwingine alikuwa Abul As bin Rabii mume wa Zainab binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).

Zainab akapeleka fidia ya kumkombolea mumewe ukiwemo mkufu wa mama yake Khadija. Mtume alipouona aliingiwa na huruma nyingi sana, na kuwaambia Waislamu: “Kama mtaonelea ni vyema kumwachia na kumrudishia vitu vyke basi fanyeni” Basi Waislamu walimwachia na kumrudishia mkufu. Abul As akasilimu baada ya hapo.

Mtume (saw) aliua, miongoni mwa mateka waovu ambao haitarajiwi heri kwao, na wala hakukubali fidia yao. Ibn Athir anasema: “Miongoni mwa mateka alikuwemo Nadhr bin Harith na Uqba bin Abi Muiti. Mtume akaamuru wauliwe akasema Uqba: “Je, mimi si kama mateka hawa?” Lakini Mtume hakujali kauli yake hiyo, kwa vile anajua uovu wake na uhaini wake, na kwamba maisha yake ni shari na ufisadi katika ardhi.

Kwa hiyo kuwaachia huru baadhi ya mateka na kuwaua wengine, kunafahamisha kuweko masilahi kwa Uislamu na Waislamu katika kuwaacha walioachwa; nayo yalidhihiri, baadae, kama tulivyoelezea. Kwa ajili hii ndipo ikasihi kuvua hukumu ya uharamu katika mateka wa Badr.

Basi kuleni katika vile mlivyoteka ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Maneno yanaelekezwa kwa waliopigana vita Badr pamoja na Mtume. Yana madhumuni ya kuidhinisha kula walivyochukua ngawira katika vita, iwe ni fidia au ngawira yenyewe. Hii ni dalili kwamba kuchukua mateka katika Badr kuliruhusiwa. Kwa sababu kuruhusu moja ya badali mbili (kitu na thamani yake) ni kuruhusu ya Pili; yaani ikiruhusiwa thamani ndio imeruhusiwa mali yenyewe. Kuna Hadith isemayo: “Mwenyezi Mungu akiharimsha kitu basi pia huharamisha thamani yake.”

Ewe Nabii! Waambie wale mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi Mungu akijua heri yoyote nyoyoni mwenu, basi atawapa bora kuliko vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Baada ya Mtume kuchukua fidia kutoka kwa mateka aliamrishwa kuwaambia hao mateka kuwa ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu atawapa badali bora kuliko fidia, duniani na akhera.

Wafasiri wanasema kuwa baadhi ya mateka walidhihirisha Uislamu, ndipo Mwenyezi Mungu akamwaamrisha Mtume wake kuwaambia kuwa ikiwa mliyoyasema ni haki basi Mwenyezi Mungu anajua na atawapa badali bora kuliko vile vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na ikiwa ni unafiki basi mmekwisha kufuru na mkafanya vitimbi kabla ya hapo na Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mtume wake juu yenu.

Kisha wakaendelea kusema wafasiri, akiwemo Razi na Tabrasi, kwamba Mtume (saw) alimwambia ami yake, Abbas: Jikomboe wewe na watoto wawili wa nduguyo, Aqil na Naufal. Abbas, akasema: Nilikuwa Mwisilamu wakanilazimisha kutoka. Mtume akamwambia Ikiwa uyasemayo ni kweli, basi Mwenyezi Mungu atakulipa. Abbas akasema: Sina chochote. Mtume akasema: Iko wapi ile dhahabu uliyompa mkeo,

Ummul Fadhi na kumwambia: Nikitokewa na lolote basi ni yako na watoto wako?1 Abbas akashangaa na kumuuliza: Ni nani aliyekuambia?

Mtume akasema: Mwenyezi Mungu ndiye aliyeniambia. Abbas akasema: Nashuhudia kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu; Wallahi hakujua habari hii yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu. Baada ya hapo Abbas alisema: Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika Mwenyezi Mungu alinibadilishia ziada nyingi baada ya kutoa fidia.

Na kama wanataka kukufanyia hiyana, basi walikwishamfanyia hiyana Mwenyezi Mungu kabla, na akakupa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

Dhamir katika kama wanataka, inawarudia mateka ambao aliwaacha huru Mtume (saw). Maana ni kuwa usiogope hiyana ya mateka uliowaachia, kwani wananini wakitaka kufanya hiyana? Walikupiga vita kabla na haikuwa lolote:

وَمَنْ عَادَ فَيَنْتَقِمُ اللَّهُ مِنْهُ ۗ وَاللَّهُ عَزِيزٌ ذُو انْتِقَامٍ {95}

“Na atakayerudia, Mwenyezi Mungu atampa adhabu; na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye kuadhibu.” Juz.7 (5:95)

Hii ni dalili nyingine kuwa Mwenyezi Mungu aliwahalilishia waislamu mateka katika vita vya Badr.

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu amewajibisha kuwaua washirikina katika vita yao na waumini ikiwa vimetukia kabla ya dini kuwa na nguvu; isipokuwa katika vita vya Badr.

Kwani Mwenyezi Mungu alihalalisha kwa Mwislamu anayepigana kuchukua mateka kwa masilahi ya Uislamu na waislamu.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَالَّذِينَ آوَوْا وَنَصَرُوا أُولَٰئِكَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يُهَاجِرُوا مَا لَكُمْ مِنْ وَلَايَتِهِمْ مِنْ شَيْءٍ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا ۚ وَإِنِ اسْتَنْصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ إِلَّا عَلَىٰ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ مِيثَاقٌ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {72}

Hakika wale walioamini na wakahajiri na wakapigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao; na wale waliokaribisha hao ndio wanaosimamiana wao kwa wao. Na wale walioamini na wasihame, hamna haki ya kuwasimamia hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiwaomba msaada katika dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipokuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

وَالَّذِينَ كَفَرُوا بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ إِلَّا تَفْعَلُوهُ تَكُنْ فِتْنَةٌ فِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ {73}

Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao; msipofanya hivyo itakuwa fitina katika ardhi na ufisadi mkubwa.

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَالَّذِينَ آوَوْا وَنَصَرُوا أُولَٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَهُمْ مَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ {74}

Na wale walioamini waka- hajiri na wakafanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale waliokaribisha na kusaidia, hao ndio waumini kweli, wana wao maghufira na riziki njema.

وَالَّذِينَ آمَنُوا مِنْ بَعْدُ وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا مَعَكُمْ فَأُولَٰئِكَ مِنْكُمْ ۚ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّهِ ۗ إِنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {75}

Na wale walioamini baadaye wakahajiri na wakapigania jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi. Na ndugu wa tumbo wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika Kitab cha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.
  • 1. Akil bin Abu twalib alisilimu kabla ya vita ya Badr, lakini washirikina walim- lazimisha kwenda vitani kupigana na binamu yake Muhammad (s.a.w).