read

Aya 71 – 72: Na Waumin Wanaume Na Waumini Wanawake

Maana

Na waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao.

Makusudio ya walii hapa ni kusaidiana. Baada ya Mwenyezi Mungu (swt) kutaja wanafiki na uchafu wao, anawataja waumin kwa fadhila zao; na kwamba wanasaidiana. Yeyote anayedai kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala asimsaidie ndugu yake katika imani hii basi yeye ni mnafiki aliyetajwa na Aya iliyotangulia, iliyowashukiwa wanafiki.

Huamrishana mema na kukatazana maovu Kinyume na wanafiki ambao wanaamrisha maovu na hukataza mema. Na husimamisha swala kiuhakika, sio ria kama wanafiki.

Na hutoa zaka Wala hawafanyi ubakhili kama wanafiki.

Na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake

Na wanaendelea na utiifu huo vyovyote iwavyo.

Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu

Ama wanafiki amewalaani na kuwaandalia moto wa Jahannam hali ya kudumu humo.

Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

Mwenye uwezo wa kuwapa nguvu waumini na kuwadhalilisha wanafiki na makafiri.

Amewaahidi Mwenyezi Mungu waumini wanaume na waumin wanawake bustani (Pepo) zipitazo mito chini yake; hali ya kudumu humo na maskani mema katika mabustani ya milele. Na radhi za Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi

Kila anayemridhisha Mwenyezi Mungu katika amali zake na makusudio yake, basi Mwenyezi Mungu atamridhia.

Huko ndiko kufuzu kukubwa

Huko ni ishara ya huko kupata bustani na makazi mema. Umetangulia mfano wake katika Juz.(3:15).

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ ۚ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ {73}

Ewe Mtume! Pambana na makafiri na wanafiki na uwawekee ngumu. Na makazi yao ni Jahanamu, nayo ni marejeo mabaya.

يَحْلِفُونَ بِاللَّهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ وَهَمُّوا بِمَا لَمْ يَنَالُوا ۚ وَمَا نَقَمُوا إِلَّا أَنْ أَغْنَاهُمُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ مِنْ فَضْلِهِ ۚ فَإِنْ يَتُوبُوا يَكُ خَيْرًا لَهُمْ ۖ وَإِنْ يَتَوَلَّوْا يُعَذِّبْهُمُ اللَّهُ عَذَابًا أَلِيمًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَمَا لَهُمْ فِي الْأَرْضِ مِنْ وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ {74}

Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu, hawakusema na hakika wamekwisha sema neno la kufuru. Na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Wakajihimu kufanya wasioyoweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila ni kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kwa fadhila zake. Wakitubia, itakuwa heri kwao; na kama wakikengeuka, Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu iumizayo duniani na Akhera. Hawana mlinzi katika ardhi wala msaidizi.