read

Aya 72 – 75: Wahajiri Na Ansar

Maana

Aya hizi zimewagawanya waumini kwenye mafungu; na zikaonyesha muungano wa kusaidiana ulioko baina yao kwa sababu ya imani na Hijra. Pia Aya zimeonyesha muungano wa makafiri na mirathi ya wenye udugu.

Ufafanuzi ni kama huu ufuatao:

1. Hakika wale waliaomini na wakahajiri na wakafanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao

Hao ni wale wahajiri (wahamiaji) wa kwanza. Mwenyezi Mungu amewasifu kwa imani, kuhama mji na kufanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa hali na mali.

Ni kwa kujitolea huku, sio imani tu, ndipo Qur’an ikawasifu na kuzungumza mengi ya kumwitikia kwao Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Utauliza: Ilivyo ni kuwa wahajiri waliingia Madina wakiwa hawana kitu ndio maana Ansar waliwakaribisha majumbani mwao wakawapa chakula na mavazi, wakiwatanguliza wao kuliko wenyewe; kama asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Na wale waliokaribisha,’ sasa walitoa wapi mali waliyoijitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu?

Jibu: Kwanza wahajiri walikuwa wakiwasaidia mafukara waislamu kabla ya Hijra. Pili, wao waliacha majumba yao na mashamba yao yaporwe na washirikina, kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. Hakuna kitu kikubwa kama mtu kuacha nyumba yake, na ardhi yake na yote aliyoyachuma kwa ajili ya maisha yake na watoto wake.

2. Na wale waliokaribisha na kusaidia hao ndio wanaosimamiana wao kwa wao.

Hao ni Ansar. Mwenyezi Mungu (swt) amewasifu kuwa wao walimkaribisha Mtume na walioahama naye katika majumba yao, wakawapendelea kuliko nafsi zao na watoto wao.

Na kwamba wao walimpa amani aliyewapa amani wahajiri na kuwa hasimu waliowafanyia uhasimu. Kwa hali hiyo ndipo, Mwenyezi Mungu akawapa sifa hii mpaka likawa neno ‘Answar’ (wasaidizi) ndio nembo yao siku zote.

Kauli yake Mwenyezi Mungu hao ndio wanosimamiana ni kuashiria Wahajiri na Answar kwa pamoja; na kwamba kila mmoja anamsimamia mwenzake kama anavyojisimamia kimsaada na kiulinzi. Kuna Hadith isemayo: “Mfano wa waumini katika kuhurumiana na kupendana; ni kama mfano wa mwili, kiungo kimoja kikiwa na tatizo, basi huacha mwili mzima ukeshe na kuwa na homa.”

Baadhi ya wafasiri wamewatofautisha Wahajiri na Answar, wakawafanya bora hawa kuliko hao. Ama sisi tuko katika upande wa kuwa wote wako sawa. Hilo lafahamishwa na Aya tuliyo nayo, vile vile Aya isemayo:

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ {10}

“Na waolitangulia wametangulia.” (56:10)

Hawa waliwatangulia wenzao kwa imani na kuhama na wale wakawatangulia wenzao kwa kukaribisha na kusaidia. Yakawa makundi yote ni katika waliotangulia. Mwenyezi Mungu (swt) amewasifu hivyo katika Aya isemayo: “Na waliotangulia wa kwanza katika wahajiri na Answar”

Na wale walioamini na wasihame.

Hawa ni wale walioamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lakini walikataa kutoka mji wa shirki na kuhamia mji wa Uislamu, pamoja na kuwa Qur’an imewaamrisha na kuwahimiza, lakini wao walishikamana na mali zao na kuhofia masilahi yao.

Yametangulia maelezo ya hawa na hukumu ya Hijra katika Juz.5 (4:97)

Mwenyezi Mungu (swt) amebainisha hukumu ya hawa ambao hawakuhama kwa kusema:

Hamna haki ya kuwasimamia hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiwaomba msaada katika dini, basi ni juu yenu kuwasaidia.

Yaani hawa hawazingatiwi kuwa ni sehemu ya jamii ya Kiislamu; wala haiwathibitikii haki yoyote ya waislamu wanaokaa katika mji wa Kiislam. Kwa sababu wao wamechagua hukumu ya shirk na washirikina kuliko hukumu ya Uislamu na waislamu.

Ndio! wakiacha nchi ya washirikina kuelekea nchi ya Uislamu, basi wanayo haki ya kulindwa na kusaidiwa. Vile vile kama akiwachokoza mchokozi kwa ajili ya dini na itikadi yao na kujaribu kuwafitini na Uislamu.Lakini si wajibu kuwasaidia katika yasiyokuwa hayo. Kwa sababu, mfungamano wa dini unamlazimisha kila mmoja kulinda dini ya ndugu yake, hata kama ni fasiki. Kwa maneno mengine ni kuwa kuilinda itikadi ya fasiki ni kulinda dini hasa sio kumlinda fasiki mwenyewe.

Kama kwamba muuliizaji aliuliza: Ikiwa kafiri amemchokoza Mumin ambaye hakuhama: na baina ya kafiri mchokozi na Mumin aliye katika nchi ya Kiislam kuna mkataba, na Mumin aliyechokozwa akataka msaada kwa Mumin aliye katika nchi ya Kiislamu, Je, hapo ni wajibu kumsaidia aliyechokozwa?
Mwenyezi Mungu (swt) akajibu kwa kusema:

Isipokuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mweneyzi Mungu anayaona mnayoyatenda.

Yaani usaidizi haupasi katika hali ya namna hii kwa kulinda mkataba. Kwani Uislamu hauruhusu kwa hali yoyote kufanya hiyana, hata na kafiri.

Jina La Dini Halina Athari

Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao.

Dhahiri ya Aya inaweza kutoa dhana kwamba kushirikiana katika ukafiri kunapelekea kusaidiana. Lakini hali haiko hivyo. Historia ya makafiri wao kwa wao ni historia ya vita na umwagikaji wa damu. Vile vile historia ya waislamu.

Majarabio yamefahamisha kuwa masilahi ndiyo yanayowaweka watu pamoja. Ama matamko tu na majina ya kidini, kama vile Mwislamu na Mkristo, yanaweza kuwa na athari, lakini haifikii kiwango cha kusimami- ana kwa kusaidiana.

Yaani huyu amsimamie mwenzake; kama anavyojisimamia kiasi cha kutoa mhanga masilahi yake yote, hata nafsi yake na watu wake na mali yake! Hapana, ila ikiwa ni kwa ajili ya dini.

Hayo ndiyo yanayokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu. ‘Hao ndio wanaosimamiana’ na pia kauli yake:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَ{71}

Waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao. Huamrishana mema na kukatazana maovu” (9:71).

Yaani mema kwao ndio masilahi Ama makusudio ya kauli yake: ‘Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao” na kauli yake:

وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۖ {19}

“Na hakika madhalimu wanasimamiana’ (45: 19).

Pia kauli yake:

الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُمْ مِنْ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمُنْكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ{67}

Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja. Wanaamrisha maovu na kukataza mema” (9:67)

Makusudio ya Aya hizo tatu ni kuwa makafiri, wanafiki na madhalimu wanakuwa kitu kimoja dhidi ya haki, pamoja na uadui na kupigana baina yao. Kwa sababu masilahi yanawakusanya na kuwaweka safu moja, masi- lahi yenyewe ni kulinda manufaa na faida.

Hilo limekwishafanyika mara nyingi zamani na saa. Katika historia ya saa ni muungano wa wakoloni na wanyonyaji dhidi ya wazalendo na wanamapinduzi; na jinsi mashirika ya kilanguzi yanavyoshindania faida.

Na historia ya zamani ni kuafikiana washirikina wa kiarabu na mayahudi wa Hijaz na wanafiki kwa kauli moja kuupiga vita Uislamu na waislamu. Hakuna lililowapa msukumo huo isipokuwa masilahi ya pamoja; kwani uadui baina ya washirikina na mayhudi, kabla ya Uislamu, ulikuwa umepita kiasi.

Kwa maelezo hayo ndio tunafasiri kauli yakeMwenyezi Mungu: “Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao.” Ama walioyoyaeleza wafasiri wengi kuwa makusudio ni kuwa makafiri wanarithiana, tafsiri hii iko mbali na dhahiri ya tamko.

Tumezungumzia mfano wa Aya hii na masilahi ya pamoja baina ya mayahudi na wakristo wengi hivi sasa, katika Juz.6 (5:51) kifungu cha mayahudi petroli na wakristo.

Msipofanya hivyo itakuwa fitina katika ardhi na ufisadi mkubwa.

Yaani: Enyi Waislamu! Mlioamini msipowasaidia waislamu wenye kuwataka msaada dhidi ya makafiri ambao wanajaribu kuwafitini na dini yao na kuwarudisha kwenye shirki, basi itakuwa chokochoko na ufisadi kwa sababu ya shirki kutawala imani na batili kutawala haki.

Hakika wale waliaomini na wakahajiri na wakafanya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Na wale waliokaribisha na kusaidia hao ndio waumini wa kweli. Wana wao maghufira na riziki njema.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja wahajiri na Ansari kwa tamko hili hili kubainisha wajibu wa hilo kwa kila mmoja juu ya mwenzake katika kumlinda na kumsaidia. Kisha hapo amerudia kwa ajili ya kuwasifu kuwa wao ndio waumini wa kweli na kubainisha alivyowaandalia keshomsamaha na thawabu ambazo amezielezea kwa ibara ya ‘riziki njema.’

Sijasoma ibara fasihi zaidi kushinda wasifu wa Imam Zainul-Abidin (a.s) kwa wahajiri na Ansari huku akimlingani Mola wake na kuwatakia rehema na radhi, kwa kusema: “Ewe Mola! Hasa maswahaba wa Muhammad ambao walikuwa na usuhuba mzuri, wakawa na majaribu mema katika kumsaidia kwake.

Wakamwitikia alipowaaeleza hoja ya ujumbe wake.

Wakapigana na mababa zao na watoto wao ili kuithibisha unabii wake na wakashinda kupitia kwake.

Waliozingirwa na mapenzi wakitarajia biashara isiyo na hasara kwa ajili ya kumpenda kwake.

Wakatengwa na jamaa zao waliposhikamana na kamba yake. Udugu ulikwisha walipotulia chini ya kivuli cha udugu wake.

Basi ewe Mola usiwasahu kwa yale waliyoyawacha kwa ajili yako. Na uwaridhie kwa radhi zako.

Na walikuwa wakilingania kwako pamoja na mjumbe wako.”

Hii ni sehmu ya kwanza ya dua namba nne inayopatikana katika kitabu cha dua kinachoitwa Asswahifatussajjadiyya ambacho Shia wanakiadhimisha na kuitukuza kila herufi yake.

Hili ni jawabu tosha la yule anayesema kuwa Shia wanawavunjia heshima maswahaba.

Na wale walioamini baadaye na wakahajiri wakapigana jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi.

Hawa ni wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wakahamia Madina na kupigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa nafsi zao na mali zao, baada ya wale waliotangulia kwanza. Wote hukumu yao ni moja tu katika wajibu wa kuwasaida na kuwalinda.

Na ndugu wa tumbo wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.

Wafasiri wanasema baada ya Mtume kuwafanyisha ndugu masahaba zake, na yeye akawa nduguye ni Ali; walikuwa wanasaidiana na kustahikiana katika mirathi; yaani warithiane kwa udugu huu sio kwa nasabu na akraba.
Kisha ikafutwa hukumu ya kurithiana huku, kukarudi kurithiana kwa udugu wa tumbo na akraba.

Aya hii wameitolea dalili Shia kwamba aliye karibu na marehemu kinasabu ndiye anayestahiki zaidi mirathi yake kuliko aliye mbali, ni sawa awe na fungu au la; au awe na nasaba au la, Kwa hiyo Binti wa marehemu anamzuia ndugu wa marehemu kurithi kwa vile yuko karibu naye zaidi; na dada wa marehemu anamzuia ami wa marehemu. Kwa sababu hiyo hiyo. Namna hii wa karibu zaidi humzuia wa mbali katika daraja zote.

Tumeyazungumzia hayo na kauli za Sunni na Shia kuhusu jambo hilo; kama tulivyoonyesha kurithiana kwa udugu na sabababu za kurithi wakati wa Jahilia. Yote hayo tumeyazungia katika Juz.4 (4:11)